Profesa Mbarawa ataka bandari Kemondo ikamilike Mei 2024
Muktasari:
- Ujenzi wa mradi wa maboresho wa bandari za Kemondo na Bukoba mkoani Kagera umefikia asilimia 25, Waziri Mbarawa aagiza ukimilike Mei mwaka 2024.
Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi Profesa, Makame Mbarawa amesema mradi wa maboresho wa bandari za Kemondo na Bukoba mkoani Kagera utarahisisha shughuli za uchukuzi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, huku akimtaka mkandarasi anayetekeleza shughuli hiyo kuikamilisha Mei mwakani.
Bandari hizo ni miongoni mwa miradi iliyotolewa na maelekezo Novemba 9 na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda aliyekuwa mkoani Kagera ambapo alimuagiza Profesa Mbarawa kuhakikisha anafuatilia kwa ukaribu utelekezaji wake
Taarifa iliyotolewa jana Jumamosi Novemba 25, 2023 na Wizara ya Uchukuzi, imeeleza waziri huyo ametembelea katika bandari hizo na kumtaka mkandarasi wa kampuni ya China Railway Major Bridge Enginnering Limited (CRMBEG) kukamilisha kazi hiyo kwa wakati ili kuruhusu meli ya MV Mwanza kutoa huduma katika bandari hizo.
Akizungumza mara baada ya kukagua miradi hiyo, Profesa Mbarawa amesema kukamilika kwa miradi hiyo kutarahisisha shughuli za uchukuzi baina ya bandari hiyo, mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani zinazunguka mikoa hiyo.
“Nawapongeza kwa hatua iliyofikiwa lakini niwakumbushe kuwa ujenzi wa meli ya MV Mwanza uko katika hatua mbalimbali za kukamilishwa na itakapokamilika itatumia bandari hizi mbili kutoa huduma.
"Lazima tuongeze kasi ya ujenzi hususani kwenye gati angalau moja kwa kila bandari ili kuruhusu meli yetu ya MV Mwanza kutoa huduma," amesema Waziri Mbarawa.
Mbali na hilo, Profesa Mbarawa pia ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha inakuwa na vifaa maalumu vya kuongozea meli vitakavyowekwa katika Victoria ili kuziwezesha kutoa huduma katika hali ya usalama.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Misenyi, mkoani Kagera Kanali Wilson Sakulo amesema mradi huo ukikamilika utachochea ukuaji wa biashara kwa mikoa ya kanda ya Ziwa.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Juma Kijavara amesema miradi inayohusisha maboresho ya bandari ya Kemondo na Bukoba imefikia asilimia 25 na kwamba taasisi hiyo itahakikisha inamsimamia mkandarasi ili aikamilishe kwa wakati.
Naye Mhandisi Mkazi wa Kampuni ya Dar Al Handah Consultants, Joshua Lesha amemuhakikishia Profesa Mbarawa kuwa watahakikisha wanaongeza kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo miwili sababu, akisema sehemu kubwa ya vifaa vya ujenzi vipo kwenye eneo la mradi.