Mwana FA kutoka kuwa mwanaHip Hop hadi U-naibu waziri
Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Mbunge wa Muheza, Hamis Mohamed Mwinjuma ‘Mwana FA’ kuwa Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Katika taarifa iliyotolewa leo Jumapili Februari 26, 2023 na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka imeeleza kuwa Mwana FA amechukua nafasi ya Pauline Gekul ambaye amehamishwa kuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria.
Mwana FA ambaye ni msanii wa Hip Hop nchini aliingia kwenye siasa na katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 2020 akafanikiwa kushinda nafasi ya ubunge wa Muheza, Tanga kwa kupata kura 47,578 na mshindani wake wa karibu, Yosepher Komba akipata kura 12,034.
Mwana FA ni msanii wa Hip Hop anayeendelea kushika nafasi kubwa ya uongozi nchini.
Baadhi ya wasanii wengine wa Hip Hop ambao wameshika nafasi katika uongozi ni Nickson Simon ‘Nikki wa Pili’ ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ambaye ndiye msanii wa kwanza wa Hip Hop kuingia bungeni kwa kura za wananchi, mwaka 2010 alishinda kiti cha Ubunge Mbeya Mjini.
Mwaka 2015 ndiye mbunge aliyeoongoza kwa kuchaguliwa na wapiga kura wengi kuliko mbunge yeyote kati ya wabunge 257 waliochaguliwa katika uchaguzi mkuu mwaka huo.
Sugu alipata kura 108,566 kati ya 166,256 zilizopigwa.
Novemba 2015 Joseph Haule ‘Profesa Jay’ akaingia kwenye orodha ya msanii mwingine wa Hip hop kushinda ubunge kupitia kura za wananchi wa Mikumi, Morogoro baada ya kupata kura 32,259 huku mshindani wake wa karibu, Jonas Nkya akipata kura 30,425.
Kwa mtiririko huo, utaona kuanzia mwaka 2010 hadi sasa uchaguzi umekuwa ukipeleka wasanii wa Hip Hop bungeni na tumeona mkuu wa wilaya akitokea ndani ya Hip Hop, na sasa Naibu Waziri.