MwanaFA, AY waendelea kupata ushindi kortini

Dar es Salaam. Harakati za kampuni ya Mic Tanzania Limited kujinasua na utekelezaji wa hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Ilala inayowataka kuwalipa fidia ya Sh2.1 bilioni wasanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya, Hamisi Mwinyijuma (MwanaFA) na Ambwene Yesaya (AY) zinazidi kugonga mwamba.

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imelikataa ombi la kampuni hiyo kukata rufaa Mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi wa mahakama hiyo iliyolitupa ombi lake la kusimamisha utekelezaji wa hukumu hiyo.

Mahakama ya Wilaya ya Ilala katika hukumu ya mwaka jana iliiamuru kampuni hiyo iwalipe fidia ya kiasi hicho cha fedha wasanii hao kwa makosa ya ukiukwaji wa hakimiliki.

Mahakama ilifikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha kuwa Mic ilitumia nyimbo zao kibiashara kama miito ya simu bila makubaliano wala ridhaa yao. Nyimbo hizo ni Usije mjini wa MwanaFA na Dakika moja wa AY.

Kampuni hiyo ilikata rufaa Mahakama Kuu kupinga hukumu hiyo na pia iliwasilisha maombi ikiomba kusimamishwa utekelezaji wa hukumu hiyo hadi uamuzi wa rufaa utakapotolewa.

Wasanii hao kupitia wakili Albert Msando waliweka pingamizi wakiiomba Mahakama Kuu itupilie mbali maombi hayo, wakidai ni batili kwa kuwa yamefunguliwa chini ya kifungu cha sheria kisicho sahihi.

Ijumaa, Mahakama Kuu katika uamuzi uliotolewa na Jaji Isaya Arufani iliyatupa maombi ya kusimamisha utekelezaji wa hukumu hiyo baada ya kukubaliana na hoja za pingamizi za Msando.