Mwanafunzi abaini mbinu ya kuhifadhi matunda kwa njia ya unga
Muktasari:
- Mhitimu wa Chuo cha Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Mkoa wa Arusha, George Wakulima amebaini mbinu inayowawezesha wakulima wa matunda kuyabadili kuwa kwenye mfumo wa unga. Ni katika Maonyesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Ili kusaidia wakulima wa matunda kutopata hasara kutokana na bidhaa zao kukosa soko na kuharibika, Mhitimu wa Chuo cha Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Mkoa wa Arusha, George Nyahende amekuja na mashine inayoweza kukausha na kusaga matunda kuwa katika mfumo wa unga.
Kusangwa kwa matunda hayo na unga wake kuhifadhiwa katika makopo pia kunayafanya kuwa na uwezo wa kukaa kwa muda mrefu tofauti na yakiwa katika hali yake ya kawaida.
Mashine hiyo amekuja nayo katika Maonyesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Nyahende amesema alifikia uamuzi huo baada ya kubaini wakulima wamekuwa wakikumbana na changamoto ya kuharibika kwa mazao kutokana na matunda kutokuwa na uwezo wa kukaa kwa muda mrefu.
Kufuatia suala hilo, wakulima wengi wamekuwa wakipata hasara na kukosa soko la uhakika.
"Unakuta wakulima wanavuna mazao yao ambayo ni ya msimu na ukizingatia kipindi cha msimu matunda yanakuwa mengi hivyo kusababisha mengine kupotea kwa kuharibika na mengine wakulima huamua kuuza kwa hasara kwa kuhofia kuharibika," amesema Nyahende.
"Mashine hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kuokoa fedha za wakulima zinazopotea kwa kuhakikisha wanabadilisha matunda yao na kuyachakata kuwa unga na kuuza katika masoko makubwa," amesema.
Amesema kubadilishwa kwa matunda hayo na kuwa katika mfumo wa unga utamfanya mkulima kuuza mazao yake kwa utaratibu tofauti na awali ambapo huuza kwa haraka kutokana na kuogopa hasara.
Amesema alifikia uamuzi huo baada ya kushuhudia wakulima wa vitunguu mkoani Arusha, walivyokuwa wakipata shida baada ya kuvuna, vingine huoza na wanunuzi wakihitaji kwa bei ambazo zinawanyonya.
"Wanunuzi wakija hawaangalii gharama ya uandaaji, wanajipangia bei zao wenyewe, ila watakapo chakata matunda na kugeuka kuwa unga yanasaidia kuuza kwa utaratibu na kupata faida ambapo itawafanya kuwepo kwenye kilimo chao cha faida kubwa," amesema Nyahende.
Amesema mashine hiyo inauwezo wa kukausha mazao kuanzia Kg100 hadi tani moja kwa wakati mmoja kulingana na ukubwa wa mashine.
Mmoja wa watembeleaji wa maonyesho hayo, Benjamin Njiku amesema uongezaji wa thamani katika matunda hayo unaweza kuwa ni fursa mpya ya kukuza kipato cha mkulima.
"Hii itawaondolea hofu ya matunda kuharibika, itawafanya kufikiria soko la baadaye zaidi badala ya wakati huo, pia soko la nje badala ya kuangalia tu lile la ndani," amesema Njiku.