Mwanafunzi afariki dunia akiogelea kwenye shimo
Muktasari:
- Mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Mbabani kata ya Mtakuja Wilaya ya Geita, Dominanti Masumbuko (13) amepoteza maisha wakati akiogelea kwenye shimo la moram lililopo karibu na makazi yao.
Geita. Mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Mbabani, kata ya Mtakuja, wilaya ya Geita, Dominanti Masumbuko (13) amefariki dunia wakati akiogelea kwenye shimo la moram lililopo karibu na makazi yao.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita, Hamis Dawa akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 8,2024 amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema mtoto huyo alifikwa na mauti wakati akiogelea.
Amesema shimo hilo lililopo kwenye makazi ya watu lilichimbwa kwa ajili ya kutoa moram ya kutengenezea barabara, lakini kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha limejaa maji na mwanafunzi huyo alikuwa akiogelea kabla ya kuzidiwa na maji na kupoteza maisha.
“Tunawasihi wazazi kwenye kipindi hiki cha mvua wachukue tahadhari kwenye mashimo yaliyojaa maji, wahakikishe watoto hawaendi maeneo hayo, tunawasiliana na wenye mamlaka ikiwezekana shimo hili lifukiwe ili lisiendelee kuleta madhara kwenye jamii,” amesema.
Ngeleja Masalu ambaye ni kaka wa marehemu, amesema saa 11 jioni alipigiwa simu akielezwa mdogo wake ametumbukia kwenye shimo na kwa juhudi za majirani walifanikiwa na kuingia kumtoa, lakini akawa tayari amepoteza maisha.
“Naiomba Serikali ifukie shimo hili ili lisilete matatizo kwa watoto wengine, eneo hili ni la makazi ya watu hata mzazi anaweza kutoka kwenda kazini na mtoto akaja kuogelea na kuzidiwa na maji kama huyu aliyezidiwa na kupoteza maisha,” amesema Masalu.
Amesema shimo hilo hutumiwa na wananchi kuchota maji kwa shughuli ndogondogo za nyumbani lakini lipo eneo hatarishi ambalo linaweza kusababisha madhara kwa jamii.
Mwenyekiti wa mtaa wa Mbabani, Daud Zakayo amesema shimo hilo ni la muda mrefu lakini kutokana na mvua za mwaka huu kuwa nyingi, maji yamekua mengi na mwanafunzi huyo amepatwa na mauti wakati akiogelewa na kuzidiwa na maji.
Amesema tukio hilo ni la pili kutokea kwenye eneo hilo ambapo Oktoba, mwaka jana mtoto mwingine alipoteza maisha baada ya kutumbukia kisimani.