Mwanafunzi anusurika kifo, akikatwa mapanga

Mwanafunzi wa shule ya Sekondari Ilenza, Agnes Marco (17) akipatiwa matibabu katika kituo cha afya Kakobe kilichopo wilayani Sengerema Mkoa Mwanza baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana jana Juni 9, 2024.

Muktasari:

  • Agnes Marco amesema wakati wakitoka kufuata kuni msituni, ghafla alitokea mtu asiyemfahamu na kuanza kuwakimbiza na kila moja alitupa mzigo wa kuni na kukimbia, ili kujiokoa.

Buchosa. Mwananfunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Ilenza iliyoko Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza, Agnes Marco (17), amenusurika kifo baada ya kukatwa na panga kichwani na mkononi na mtu asiyejulikana wakati akitoka kuchanja kuni msituni.

Tukio hilo limetokea jana Juni 9, 2024, saa nne asubuhi lililosababisha wenzake 16 waliokuwa naye kukimbia wakihofia kuuawa.

Akizungumza na Mwananchi Digital kwa simu jana usiku Juni 9, 2024 akiwa amelezwa Kituo cha Afya Kakobe, Agnes Marco, amesema wakati wakiwa wanatoka kufuata kuni katika eneo la msitu wa Buhindi, alitokea mtu asiyemfahamu na kuanza kuwakimbiza, hivyo kila moja alitupa mzigo wa kuni na kukimbia, ili kujiokoa.

Amesema kati ya watu 16 yeye ndiye alikuwa mkubwa na mtu huyo alitaka kumbaka, lakini alishindwa baada ya kupambana naye na kufanikiwa kumkata panga kichwani na mkononi.

"Baada ya kupambana naye muda, nilipoona amenikata panga kichwani na mkononi huku nikivuja damu alihisi kuwa ameniua, ndipo akaondoka na mimi nikapata nafasi ya kukimbia,” amesema Agnes.

Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Senyi Ngaga amesema amepata taarifa hiyo na vyombo vya ulinzi na usalama viko eneo la tukio vikifuatilia.

Mganga Mfawidhi Kituo cha Afya, Kakobe Venus Lusangia amesema baada ya kumpokea msichana huyo walimshona majeraha yake na sasa hali yake inaendelea vizuri.

Martine Edward, anayemuuguza msichana huyo amesema kwa sasa kumekuwa na mtindo wa watu wasiojulikana kufanya vitendo vya kihalifu kwenye kata ya Ilenza, hivyo kuviomba vyombo vya dola vikomeshe hali hiyo.