Mwanafunzi asimulia namna anavyowalea wadogo zake

Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Ngolo Malenya (kulia) akiwa na watoto na baadhi ya wananchi wa Kijiji Cha Gombe alipofika kwenye familia ya watoto watatu waliotelekezwa na wazazi wao. Picha zote na Lilian Lucas

Muktasari:

“Mama yangu aliondoka kwa mara ya kwanza nikiwa darasa la sita (2017) na kutuacha na baba. Alirudi tena mwezi wa saba mwaka 2018 tukakaa nana ilipofika mwezi wa 11 aliondoka na baba hakukaa nyumbani, wakatuacha peke yetu.”

Morogoro. “Mama yangu aliondoka kwa mara ya kwanza nikiwa darasa la sita (2017) na kutuacha na baba. Alirudi tena mwezi wa saba mwaka 2018 tukakaa nana ilipofika mwezi wa 11 aliondoka na baba hakukaa nyumbani, wakatuacha peke yetu.”

Hii ni sehemu ya simulizi ya Elionida Ulanda (17), mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Celina Kombani.

Akizungumza na Mwananchi, binti huyo alisema amekuwa akifanya vibarua katika mashamba siku za Jumamosi ili aweze kusaidia wadogo zake wawili, mwenye umri wa miaka 13 anayesoma darasa la saba na wa miaka tisa anayesoma darasa la pili.

Elionida anasema anapokwenda shule huwaacha wadogo zake peke yao na chakula hupata kutoka kwa majirani ambao wamekuwa wakiwasaidia.

Anasema wazazi walianza kwa kutoelewana ndipo mama aliondoka na kuwaacha na baba yao na nyakati zote mama yao alikuwa akirudi mara moja moja.

“Baadaye tulihamia kwao mama, tukiwa huko nyumba ilibomoka, tukarudi kwenye nyumba tuliyokuwa tunaishi na baba na mama ambayo tunaishi mpaka sasa.

Anasema mwaka 2020 baba yao alirudi kijiji hapo lakini akawa anaishi kwa mwanamke mwingine na mama yao hawajui alipo kwa sasa.

Mbali na kuwahudumia wadogo zake, mwanafunzi huyo hutembea umbali mrefu kwenda shule. Umbali kutoka Kijiji cha Gombe mpaka shule anayosoma ni takriban kilometa 7.5, hivyo amelazimika kupanga chumba cha Sh5,000 kwa mwezi ili kupunguza umbali wa kutembea kila siku.

Nyumba wanayoishi watoto watatu wanaodaiwa kutelekezwa na wazazi wao katika Kijiji cha Gombe wilayani Ulanga.

Anasema amekuwa akirudi nyumbani Ijumaa kusaidia wadogo zake na kufanya vibarua Jumamosi ili wapate fedha ya kujikimu.

Makamu Mkuu wa shule ya Sekondari Celina Kombani, Edom Mwansyange alisema mazingira ya mwanafunzi huyo ni magumu kutokana na wazazi wake kutomjari na kwamba kitaaluma yuko chini kutokana na mazingira yanayomkabili.

Mwansyange alisema “kwa mwanafunzi anayeishi mazingira hayo ya kutojua atakula nini kwa siku, kitaaluma lazima afanye vibaya na sisi kama shule kuna michango huwa tunamsamehe kutokana na hali yake ilivyo.”


Kiongozi wa familia

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Gombe, Pelegrein Mihonga alisema mwanafunzi huyo amekuwa ndio kiongozi wa familia na mara nyingi wamekuwa wakisaidiwa na majirani kwa chakula ambacho wamekuwa wakipata mlo mmoja kwa siku.

Jirani yao, Hidaya Omary, alisema mara kadhaa alikuwa akiwasaidia watoto hao kwa kuwapatia chakula baada ya kuona wametelekezwa na kwamba yeye aliyeibua tatizo la watoto hao kwenye Shirika la Solidarmed.