Prime
Mwanafunzi mwingine akibwaga chuo kortini
Moshi. Mahakama ya Rufani Tanzania imeamuru kurudishwa chuoni kwa mwanafunzi wa shahada ya kwanza ya elimu katika Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (SEKOMU), James Kusaga aliyeondolewa mwaka 2017.
Hii ni hukumu ya tatu ndani ya kipindi cha miezi mitatu ya wanachuo kuvibwaga kortini vyuo vyao na hukumu ya karibuni ni ya Juni 13, 2023 baada ya mwanafunzi wa chuo kikuu cha Tumaini Dar es Salaam, Mwajuma Malulu kukishinda chuo hicho.
Mwanafunzi huyo alifukuzwa katika chuo hicho maarufu kwa jina la TUDARCo kwa madai ya kufanya udanganyifu wa kufanyiwa mtihani wa majaribio, lakini mahakama ikafuta uamuzi huo kwa kuwa seneti haikumpa haki ya kusikilizwa.
Miezi mitatu iliyopita, wanafunzi wa chuo kikuu St Augustine cha Jijini Mwanza, walishinda kesi baada ya miaka 12 dhidi ya bodi ya wadhamini ya chuo hicho, kilichowafukuza na Mahakama kuamuru walipwe fidia ya Sh30 milioni.
Kwa upande wa mwanafunzi wa SEKOMU aliyekuwa akisomea Shahada ya Elimu (Mahitaji Maalumu), alifukuzwa na seneti ya chuo hicho kwa maelezo alifeli masomo manne kati ya matano aliyokuwa amerudia kufanya.
Hata hivyo, katika uamuzi wake ilioutoa juzi, jopo la majaji watatu la Mahakama ya Rufani katika kikao chake kilichoketi jijini Tanga likiongozwa na Shaban Lila, Ignas Kitusi na Patricia Fikirini, limefuta uamuzi wa kumfukuza mwanafunzi huyo.
Mbali na kufuta uamuzi huo wa seneti ya chuo hicho kwa maelezo kuwa mwanafunzi huyo hakupewa haki ya asili ya kusikilizwa, lakini pia ilifuta uamuzi wa Mahakama Kuu Tanga wa kuyatupa maombi yake ya kuomba marejeo.
Jopo hilo la majaji katika hukumu yake hiyo limesema haki ya kusikilizwa ni haki ya msingi ambayo mahakama inailinda kwa wivu na ni haki inayotolewa na ibara ya 13(6)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Majaji hao walisema katika rufaa hiyo, hakuna uthibitisho kuwa mwanafunzi huyo alipewa hati ya wito (summons) ya kusikilizwa ama Agosti 12, 2017 au Agosti 24, 2017 ama Agosti 24,2021 kama barua hizo zilivyofanyiwa marejeo.
Walisema tarehe ya kusikilizwa kwa suala lake (Agosti 12, 2017) inayotajwa katika barua ya Agosti 17, 2017 na muhtasari wa kikao cha seneti cha Agosti 26, 2017 zote zinaonyesha kikao hicho kilifanyika Agosti 12, 2017.
Kikao hicho kilifanyika baada ya mwanafunzi huyo kushindwa kutokea na kikao kuahirishwa hadi Agosti 24, 2021, lakini mabadiliko hayo hayaonekani katika muhtasari wa kikao cha seneti cha Septemba 4, 2017 kilichomfukuza.
“Kwa hakika, kuna mkanganyiko kuhusu tarehe ambayo mlalamikaji aliitwa na ni lini hasa usikilizaji wa rufaa ya mrufani ulifanyika,” walisema.
Hivyo majaji hao wakafuta uamuzi wa seneti na agizo la kumsitishia mrufani kuendelea na masomo na SEKOMU wakaamriwa kupitia chombo chake cha rufaa na kamati ya ukiukwaji wa kanuni (UAIC) kumpa mrufani haki ya kusikilizwa kabla ya uamuzi wowote dhidi yake kufanywa na vyombo hivyo viwili.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za Mahakama ya Rufani, Kusaga alisajiliwa na chuo hicho mwaka 2014, lakini akiwa mwaka wa pili alisitishiwa kuendelea na masomo kwa madai ya kushindwa kukidhi viwango vya mitihani.