Mwanahabari achaguliwa mwenyekiti ACT Wazalendo Manyara

Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Bara, Dorothy Semu kushoto akiwa na baadhi ya viongozi wa chama hicho Mkoa wa Manyara juzi katika uchaguzi mkuu wa viongozi wa chama hicho mkoa ambapo Mwandishi wa Habari Said Njuki (wanne kutoka kushoto) alishinda nafasi ya Mwenyekiti wa Mkoa huo.

Muktasari:

  • Uchanguzi ngazi ya mikoa ndani ya ACT Wazalendo unaendelea kufanyika nchi nzima ambapo watu wa kada tofauti wamechaguliwa kuongoza chama hicho.

Babati. Mwandishi wa habari mwandamizi, Said Njuki amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa wa Manyara kwa kipindi cha miaka mitano.

Njuki ambaye alikuwa anaandikia magazeti ya Majira na Raia Mwema kabla ya kugombea nafasi hiyo, amewahi pia kugombea ubunge Jimbo la Kondoa mwaka 2015 na 2020 bila mafanikio.

Msimamizi wa uchaguzi huo, Shangwe Mike ambaye Naibu Waziri Kivuli Ofisi ya Rais, Mipango, Uwekezaji na Hifadhi ya Jamii, ametangaza matokeo hayo leo Januari 16, 2024 mjini Babati, kuwa Njuki amepata kura 56 akifuatiwa na mwenyekiti wa zamani wa mkoa huo, Daniel  Kyusilu aliyepata kura 18 na Olais Silas aliyeambulia kura moja.

Miongoni mwa viongozi wengine waliochaguliwa ngazi ya mkoa, ni pamoja na Mwanahamisi Hamisi aliyechaguliwa kuwa katibu.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Njuki amesema Manyara ni moja ya mikoa yenye changamoto nyingi ikiwemo ya migogoro ya ardhi, uharibifu wa mazingira na unyanyasaji wa kijinsia, hivyo ni wajibu wa chama hicho chini yake kusimamia mambo hayo kikamilifu.

“Mkoa wa Manyara ni moja ya mikoa yenye changamoto nyingi ikiwemo ya migogoro ya ardhi, ni wajibu wetu kikatiba kuwatetea wananchi bila kujali itikadi zao na tupo tayari kutetea wananchi wetu kwa ari na mali,” amesema.

Amesema katika kipindi chache atashirikiana na wanachama wa chama hicho na Serikali kuondoa aibu ya mkoa huo kuongoza nchini kwa matukio ya ukatili dhidi ya wanawake.

Awali, makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu ambaye alikuwa mgeni rasmi aliwataka viongozi wapya kuwa wamoja ili kuhakikisha kazi ya ujenzi wa chama na utetezi dhidi ya wananchi vinakuwa rahisi.

Amesema kazi ya kujenga chama ni ya viongozi wa chama, matarajio yake ni kuona Mkoa wa Manyara unakuwa mfano wa kuigwa katika kuvuna wanachama wa kutosha na kutetea jamii katika changamoto mbalimbali.

ACT Wazalendo inaendelea na uchaguzi ngazi ya mkoa baada ya kumaliza majimbo nchini, kabla ya kufanya mkutano mkuu Machi 5 na 6, mwaka huu jijini Dar es Salaam.