Mwanamke aliyekunywa sumu baada ya kufumaniwa azikwa
Muktasari:
- Mkazi wa kijiji cha Kibaoni, wilayani Rombo Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Shirima (26) aliyejiua kwa kunywa sumu ya kuulia magugu (Parasnow) baada ya kufumaniwa na mume wake aitwaye Riziki Shirima (22), amezikwa leo Desemba 15 nyumbani kwao baada ya mwili wake kukaa mochuari takribani siku 11.
Rombo. Mkazi wa kijiji cha Kibaoni, wilayani Rombo Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Shirima (26) aliyejiua kwa kunywa sumu ya kuulia magugu (Parasnow) baada ya kufumaniwa na mume wake aitwaye Riziki Shirima (22), amezikwa leo Desemba 15 nyumbani kwao baada ya mwili wake kukaa mochuari takribani siku 11.
Anna alifariki dunia Desemba 5 mwaka huu wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Huruma iliyopo wilayani humo baada ya kunywa sumu hiyo ya magugu iliyosababisha kifo chake.
Kattika tukio hilo, mumewe Anna (Riziki Shirima) anadaiwa kumuua mwanaume aliyemfumania na mkewe aliyejulikana kwa jina la Juvenal Claud kwa kumkata na mapanga baada ya kukutwa ndani nyumba yake na baada ya kumuua alijisalimisha mwenyewe polisi.
Baada ya fumanizi hilo kutokea mwanamke huyo alikimbilia nyumbani kwa wazazi wake ambapo baadaye kutokana na fedheha aliyoipata alikunywa sumu ambayo ilipelekea kifo chake.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa matukio hayo akisema mwanamke huyo anadaiwa kunywa aina hiyo ya sumu kukwepa fedheha aliyokutwa nayo ya fumanizi.
“Marehemu kabla ya tukio hilo la kujiua alifumaniwa na mume wake Disemba 4 mwaka huu ambaye ni mtuhumiwa wa kesi ya mauaji, baada ya kumjeruhi na kumuua Juvenali Claudi ambaye alifariki dunia kwa kumkata kata na kitu chenye ncha kali,” amesema Kamanda Maigwa.
Kamanda Maigwa alisema baada ya mume wa mwanamke huyo kumfumania mkewe alianza kumshambulia mwanaume huyo kwa kumjeruhi na kitu chenye ncha kali ambapo ilipelekea kifo chake na kisha mwenye kujisalimisha polisi.
Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Damian Tesha amesema mwili wa Mwanamke huyo umezikwa nyumbani kwa mumewe huku yeye akiendelea kushikiliwa kituo cha polisi Rombo kwa mahojiano zaidi.
Mwanamke huyo ameacha watoto wawili wadogo.