Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwanamke auawa kwa madai ya wivu wa mapenzi Bahi

Leah Mazengo wakati wa uhai wake

Muktasari:

  • Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera, amethibitisha kifo hicho, akisema kwa sasa wanamtafuta mwanaume huyo aliyetoroka baada ya tukio hilo.

Dodoma. Polisi Mkoa wa Dodoma imethibitisha kifo cha Leah Mazengo (48), anayedaiwa kuuawa na mumewe katika Kijiji cha Lamaiti, Wilaya ya Bahi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera, akizungumza na waandishi wa habari, amethibitisha kutokea kwa kifo hicho huku akieleza kuwa chanzo kinadaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi.

Amesema Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka mtuhumiwa aliyetoroka baada ya kutekeleza tukio hilo.

“Ni kweli kuwa jana, Julai 20, 2026, mwili wa mwanamke Leah uliokotwa shambani kwake katika mazingira yaliyoashiria kuwa yametokana na wivu wa mapenzi. Kwa sasa tunamtafuta mumewe kwa ajili ya uchunguzi zaidi,” amesema Hyera.

Awali, Mwenyekiti wa Kijiji cha Lamaiti, Wilaya ya Bahi, Paul Mkonongo, amekiri kuwepo mauaji hayo na kwamba wanaendelea na taratibu za mazishi kijijini hapo.

“Ni kweli kuna mauaji kijijini kwangu, tena huyu Leah Mazengo alikuwa ni mjumbe wangu katika Serikali ya Kijiji, na tukio hili limetuumiza sana,” amesema Mkonongo.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, jana mwanamke huyo aliaga na kuelekea shambani, lakini hakurudi hadi jioni walipoukuta mwili wake shambani, ukidhaniwa amenyongwa.

Amesema baada ya kwenda shambani, mumewe (jina linahifadhiwa) alikwenda kwa baba mkwe wake (baba wa Leah), akaomba baiskeli na kwenda shambani.

“Baadaye kidogo alituma ujumbe mfupi kwa simu ya mkewe, akiwataka watoto wampe baba yao huyo mlezi kiasi cha Sh300,000 kwamba kuna jambo analifanya, na alipofika nyumbani watoto walitekeleza,” amesema Mkonongo.

Mkonongo amesema baada ya mtuhumiwa kupokea fedha hizo, alirejesha baiskeli kwa baba mkwe wake, kisha akarudi nyumbani haraka, akafungasha nguo zake na kukodi pikipiki iliyompeleka Bahi Mjini.

Amesema watoto walipoona hali hiyo walipatwa na hofu na kuanza kumpigia simu mama yao pamoja na baba yao, lakini simu zao hazikupatikana.

Kwa mujibu wa mwenyekiti, watoto hao baada ya kutoa taarifa kwa viongozi wa kijiji, wananchi walikwenda shambani ambako waliukuta mwili wa Leah na kisha kutoa taarifa kwa polisi waliofika eneo la tukio kwa ajili ya kufanya uchunguzi.

Mkonongo amesema Leah na mtuhumiwa walikuwa wakiishi pamoja kama mke na mume bila kufunga ndoa. Leah alikuwa mjane baada ya mumewe kufariki dunia na alikuwa ameacha watoto wanne.

Katika tukio lingine, Kamanda Hyera, amesema Jeshi la Polisi linamshikilia Maria Joseph kwa tuhuma za kuwafanyia ukatili watoto wake wawili, Yakobo Lukasi (6) na Aisha Abdul (1).

Hyera amesema Maria anadaiwa kumshambulia Yakobo sehemu mbalimbali za mwili kwa kutumia mwiko, kwa tuhuma kuwa aliiba mboga, huku Aisha akidaiwa kuchomwa na kijiko cha moto kwenye makalio, kisha kuwafungia ndani ya nyumba hadi majirani walipowanusuru na kuwapeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, ambako wamelazwa hadi sasa.