Mahakama yatengua kifungo cha maisha kesi ya ubakaji
Muktasari:
- Mahakama ya Rufaa nchini imemwachia huru Baraka Makubi, aliyekuwa amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kukutwa na hatia ya kosa la ubakaji wa mtoto wa miaka mitatu.
Arusha. Mahakama ya Rufaa imebatilisha hukumu ya kifungo cha maisha jela dhidi ya mkazi wa Mto wa Mbu, Wilaya ya Monduli mkoani Arusha, Baraka Makubi, baada ya kubaini kuwa ushahidi uliowasilishwa dhidi yake haukutosha kuthibitisha kosa la kumbaka mtoto wa miaka mitatu bila kuacha shaka yoyote.
Katika hukumu iliyotolewa Julai 17, 2026 na jopo la majaji Lugano Mwandambo, Abraham Mwampashi na Lameck Mlacha, Mahakama ilikubali rufaa ya Makubi na kutengua hukumu za Mahakama ya Wilaya ya Monduli na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha zilizomtia hatiani na kumhukumu kifungo cha maisha jela.
Makubi alikuwa amepatikana na hatia ya ubakaji chini ya vifungu vya 130(1), 130(2)(e) na 131(1) vya Kanuni ya Adhabu katika kesi ya jinai namba 19 ya mwaka 2021.
Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa katika Mahakama ya chini, tukio hilo lilidaiwa kutokea Juni 29, 2021 katika eneo la Mto wa Mbu. Mtoto huyo, aliyetambulishwa kwa herufi AJ kwa ajili ya kulinda utambulisho wake, alidaiwa kubakwa na Makubi, ambaye alikuwa jirani wa familia hiyo na mmiliki wa duka la bidhaa za rejareja.
Mama wa mtoto huyo alidai kuwa mwanaye alirejea nyumbani akilalamika maumivu katika sehemu za siri, na baadaye akamtaja Makubi kuwa ndiye aliyemfanyia kitendo hicho.
Daktari aliyemfanyia uchunguzi aliiambia Mahakama kuwa alibaini sehemu za siri za mtoto zilikuwa nyekundu, zilikuwa na majimaji yaliyobainika kuwa mbegu za kiume.
Ushahidi huo uliifanya Mahakama ya Wilaya ya Monduli kumtia hatiani Makubi na kumhukumu kifungo cha maisha jela, huku Mahakama Kuu ikitupilia mbali rufaa yake mwaka 2023.
Hata hivyo, katika rufaa yake ya pili, Makubi alipinga hukumu hiyo akidai kulikuwa na tofauti katika ushahidi wa mashahidi, kuchelewa kufikishwa mahakamani na kwamba upande wa mashtaka haukuthibitisha shtaka hilo bila kuacha shaka yoyote.
Katika uchambuzi wake, Mahakama ya Rufaa ilibaini kuwapo kwa shaka katika ushahidi wa mashahidi na wa kitabibu.
Mahakama ilieleza kuwa, mtoto huyo alikuwa na umri wa miaka mitatu na aliishi umbali wa takribani 500 kutoka duka la Makubi, huku baba yake akiwa nyumbani wakati tukio hilo likidaiwa kutokea.
Majaji walihoji kwa nini baba wa mtoto hakusikia kilio chochote ikiwa madai ya ubakaji wa nguvu yalikuwa ya kweli, jambo walilosema lingeweza kutarajiwa kutokana na umri wa mtoto na maumivu yanayoweza kusababishwa na tukio la aina hiyo.
Mahakama pia ilibaini kuwa mtoto aliweza kutembea mwenyewe hadi nyumbani na kumweleza baba yake kuwa alikuwa akihisi maumivu, hali iliyoonekana kutolingana na maelezo ya majeraha makubwa yaliyotolewa na daktari.
Aidha, Mahakama ilisema hakuna damu iliyobainika katika uchunguzi wa nyumbani wala katika uchunguzi wa kitabibu.
Kuhusu ushahidi wa daktari, Mahakama ilisema daktari alieleza kuwa mtoto alikuwa ameingiwa kingono zaidi ya mara moja, lakini hakukuwa na maelezo yaliyofafanua ni nani aliyekuwa amefanya kitendo hicho awali, huku ikihoji kwa nini mama wa mtoto, aliyekuwa akimwogesha mara kwa mara, hakuwahi kubaini hali hiyo.
Majaji walihitimisha kuwa Mahakama za chini hazikufanya tathmini ya kina ya ushahidi huo.
Mahakama pia ilisema ushahidi wa mtoto, uliotolewa bila kiapo kutokana na umri wake, ulikuwa mfupi na haukuwa na maelezo ya kutosha kuweza kuwa msingi wa hatia. Katika ushahidi wake, mtoto alidai Makubi alimfanyia kitendo hicho kisha akampa pipi.
Aidha, Mahakama ilisema ushahidi wa mashahidi wengine ulitokana na maelezo waliyopewa na mtoto huyo, hivyo ulikuwa ushahidi wa kusikia ambao haukuthibitisha moja kwa moja madai dhidi ya mshtakiwa.
"Ushahidi wa AJ ulikuwa dhaifu, lakini pia ulikabiliwa na hatari kwamba ulikuwa matokeo ya mafunzo," inaeleza sehemu ya hukumu.
Baada ya kuchambua ushahidi wote, Mahakama ya Rufaa ilihitimisha kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha shtaka la ubakaji dhidi ya Makubi bila kuacha shaka yoyote.
Kutokana na uamuzi huo, Mahakama ilifuta hatia na adhabu ya kifungo cha maisha jela na kuamuru Makubi aachiliwe huru mara moja, isipokuwa kama alikuwa anashikiliwa kwa sababu nyingine halali.