Mwananchi yaiibua NEMC kuja na mikakati mipya kudhibiti ongezeko la kelele
Muktasari:
- NEMC hupokea zaidi ya malalamiko 25 kila wiki kutoka kwa wananchi wanaosumbuliwa na kelele kupita kiasi. Sasa teknolojia kutumika zaidi.
Dar es Salaam. Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc) limezindua mikakati mipya yenye lengo la kukabiliana na ongezeko la uchafuzi wa kelele katika miji mikubwa nchini.
Mkakati huo unazinduliwa siku chache baada ya magazeti ya Mwananchi na The Citizen kuripoti mfululizo wa makala maalumu kuhusu kuongezeka kwa tatizo la kelele kwenye masoko, maeneo ya makazi na vituo vya burudani.
Katika Makala hizo, kulikuwa na malalamiko ya wananchi yanayohusishwa na baa, kumbi za starehe, mikusanyiko ya kidini na shughuli za kijamii, hasa katika maeneo ya mijini yanayokuwa kwa kasi.
Makala hizo zilionyesha namna kelele kupita kiasi katika maeneo ya biashara na masoko zilivyoendelea kuwasumbua wakazi na wafanyabiashara, huku zikizua wasiwasi kuhusu afya ya jamii, ustawi wa akili na udhaifu katika utekelezaji wa sheria za mazingira.
Akizungumza mwishoni mwa wiki katika kikao na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya miaka 40 ya NEMC, Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria za Mazingira wa mamlaka hiyo, Elibariki Bajuta alisema baraza hilo hupokea zaidi ya malalamiko 25 kila wiki kutoka kwa wananchi wanaosumbuliwa na kelele kupita kiasi.
Alisema malalamiko hayo yanajitokeza zaidi katika maeneo ya Ubungo, Salasala na sehemu nyingine za Dar es Salaam ambako ukuaji wa haraka wa miji umeongeza migongano kati ya shughuli za makazi na biashara.
“Baraza tayari limeanza kuchukua hatua dhidi ya maeneo yanayokiuka sheria za mazingira, ikiwamo kusimamisha baadhi ya shughuli na kufunga mengine,” alisema.
Hata hivyo, Bajuta alisema utekelezaji wa sheria pekee hautoshi kutatua changamoto hiyo.
“Tumegundua kuwa kufunga maeneo pekee si suluhisho endelevu. Ndiyo maana sasa tumeanzisha elimu kwa umma pamoja na mifumo ya kisayansi ya ufuatiliaji ili kushughulikia changamoto hii kwa ufanisi zaidi,” alisema.
Alibainisha kuwa Serikali imenunua gari maalumu la maabara linaloweza kupima kiwango cha kelele kisayansi na kutoa tathmini zenye ushahidi wa kitaalamu.
Kwa mujibu wake, mfumo huo ulianza kufanya kazi mwezi uliopita na tayari unatumika kufuatilia kelele kupita kiasi katika maeneo mbalimbali ya jiji.
“Tunapomwambia mtu anasababisha uchafuzi wa kelele, sasa tunatoa ushahidi wa kisayansi unaoonyesha kiwango hicho kimezidi viwango vinavyokubalika,” alisema.
Bajuta aliongeza NEMC pia inashirikiana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, mamlaka za serikali za mitaa pamoja na taasisi nyingine ili kuweka mfumo jumuishi wa usimamizi wa kelele.
Alisema wakati mwingine biashara hupata leseni kutoka mamlaka moja kabla ya kupewa vibali vya burudani na taasisi nyingine bila kuzingatia vya kutosha athari za kimazingira.
“Hali hiyo husababisha migongano kwa sababu mamlaka moja inaweza kutoa kibali huku wananchi wakiendelea kuathiriwa na kelele,” alisema.
NEMC imeonya kelele kupita kiasi si usumbufu wa kawaida pekee, bali ni tatizo linaloongezeka la afya ya jamii, hasa kwa watu wenye matatizo yanayohusiana na msongo wa mawazo, magonjwa ya moyo na shinikizo la damu.
“Watu tayari wanakosa muda wa kutosha wa kupumzika kutokana na maisha ya kisasa, halafu mtu anaamua kupiga muziki mkubwa usiku kucha bila kujali ustawi wa wengine,” alisema.
Pia alieleza wasiwasi wake kuhusu mikusanyiko mirefu ya kidini na shughuli za burudani zinazofanyika karibu na maeneo ya makazi, akisema baadhi huendelea kuanzia Ijumaa hadi Jumatatu asubuhi na kuwaacha wakazi bila muda wa kupumzika.
“Mimi ni Mkristo, lakini ibada haipaswi kuwa chanzo cha usumbufu kwa majirani. Kulinda mazingira pia ni kuheshimu ustawi wa watu wengine,” alisema.
Baraza hilo pia limewaomba wanahabari na wananchi kushiriki katika kampeni za uhamasishaji kuhusu burudani zenye uwajibikaji na utunzaji wa mazingira.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tathmini ya Athari za Mazingira na Kijamii wa NEMC, Lilian Lukambuzi, alisema baraza hilo limeimarisha mifumo yake ya ukaguzi wa mazingira kwa kutumia teknolojia ya kidijitali ili kuongeza ufanisi na uwazi.
Lukambuzi alisema ukaguzi uliokuwa ukifanyika kwa njia za kawaida sasa unasimamiwa zaidi kupitia mifumo ya kidijitali, jambo linalosaidia kupunguza ucheleweshaji na kuboresha ufuatiliaji.
“Pia tunatarajia kuzindua mfumo wa kitaifa wa ufuatiliaji wa mazingira kwa njia ya mtandao wakati wa maadhimisho ya miaka 40 ya NEMC mwishoni mwa Mei 29,” alisema.
Kwa mujibu wake, mfumo huo utatoa taarifa za moja kwa moja kuhusu viwango vya uchafuzi wa mazingira, ikiwamo ubora wa hewa, usimamizi wa taka na kiwango cha kelele katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumzia uchafuzi wa kelele, alisema ongezeko la malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu ukiukwaji wa mazingira linaonyesha kuongezeka kwa uelewa wa wananchi kuhusu haki na wajibu wao wa kimazingira.
“Wananchi wanaporipoti ukiukwaji wa mazingira, inaonyesha uelewa unaongezeka. Wajibu wetu sasa ni kuhakikisha malalamiko hayo yanashughulikiwa haraka na kwa ufanisi.”