Mwanasheria wa Airtel atoa ushahidi kesi ya kina Mbowe

Muktasari:

Mwanasheria wa kampuni ya huduma za mawasiliano ya simu za mikononi ya Airtel PLC Tanzania, Gladys Fimbari ametoa ushahidi kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu.

Dar es Salaam. Mwanasheria wa kampuni ya huduma za mawasiliano ya simu za mikononi ya Airtel PLC Tanzania, Gladys Fimbari ametoa ushahidi kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu.

Fimbari ambaye ni shahidi wa tisa upande wa mashtaka ametoa ushahidi wake leo Alhamisi Januari 13, 2022.

Katika ushehidi wake ameieleza mahakama jinsi namba za simu zinazodaiwa kuwa za Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Halfani Bwire Hassan, wanaokabiliwa na kesi hiyo, zilivyotumika katika miamala ya pesa inayohusika katika kesi hiyo.

Mbali na Mbowe washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi, namba 21 ya mwaka 2021, inayosikilizwa na Jaji Joachim Tiganga ni Halfani Bwire Hassan (mshtakiwa wa kwanza) Adamu Hassan Kasekwa (mshtakiwa wa pili) na Mohamed Abdillahi Ling'wenya (mshtakiwa wa tatu).

Baada ya Fimbari kumaliza kutoa ushahidi, mawakili wa utetezi walianza kumuuliza shahidi huyo maswali.

Hata hivyo, Jaji Tiganga ameahirisha kesi hiyo baada ya upande wa utetezi kupitia wakili John Mallya kuomba Jaji aahirishe kutokana na muda kuenda huku akidai kuwa bado ana maswali mengi.

Kesi hiyo imeahirishwa mpaka kesho Ijumaa saa tatu asubuhi ambapo upande wa utetezi utaendelea kumuuliza maswali shahidi wa tisa wa upande wa mashtaka.


Hapa ni sehemu ya kile kilichojiri mahakamani hapo wakati shahidi wa tisa wa upande wa mashtaka akitoa ushahidi wake

Tayari Jaji Joachim Tiganga ameshaingia mahakamani

Mawakili wa pande zote wanajitambulisha.

Wakili Kidando- Shauri Hilo limekuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi na kwa leo tunaye shahidi mmoja, hivyo tupo tayari kuendelea.

Jaji- Upande wa uetetezi mpo tayari kuendelea?

Kibalata: Tupo tayari kuendelea.

Kwa sasa shahidi amefuatwa nje kwenda kuchukuliwa na wakili wa Serikali Tulimanywa Majigo

Wakili anayemuongoza shahidi Anaitwa Jenitreza Kitale Ni wakili wa Serikali Mwandamizi


Jaji: Majina yako Shahidi?

Shahidi: Gladys Fimbari (39) Mwanasheria wa kampuni ya Airtel Tanzania.

Shahidi anaapa.

Shahidi anaongozwa kutoa ushahidi wake na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Jenitreza Kitale

Wakili wa Serikali Mwandamizi Kitale.

Nafanya kazi Airtel Tanzania (PLC), Dar es Salam.

Awali wakati najiunga mwaka 2014 mwezi wa nane, niliajiriwa kama ofisa sheria, lakni Machi, 2021 nilibadilishwa cheo na kuwa meneja kitengo cha sheria.

Aiterl PLC inajihusisha na mawasiliano ikijihusisha na hudma za kupiga simu, internet na kutoa huduma za muamala kupitia Airtel Money.

Shahidi: Ili uweze kupata huduma zetu unatakiwa uwe na simcard ya Airtel.

Ili kuweza kufanya usajili lazima mteja awe amenunua simcard na awe na namba za Kitambulisho Cha Taifa.

Baada ya hapo mtu anayemhudumia atachukua majina yake na kumuunga katika mifumo yetu na kisha mteja atatakiwa aweke dole gumba na msajili wetu atafanya uhakiki kupitia mifumo ya Nida amabayo imeunganishwa na mifumo yetu ya usajili.

Baada ya kufanya uhakiki, atakapopata taarifa kutoka Nida kuhusiana na uhakiki wa namba.

Baada ya kupata uhakikiki, Nida watatoa taarifa za mteja na taarifa zote zitahifadhiwa kwenye mfumo iliyounganishwa na hapo usajili utakuwa umekamilika.

Ofisa Msajili wa Airtel anapata taarifa kutoka Nida kutokana na mifumo yetu imeunganishwa na Nida.

Mteja anapiingiza dole gumba

Shahidi: Mteja anapotoa majina yake pamoja na namba ya Kitambulisho Cha Nida, zile taarifa zinahakikiwa na Ofisa wetu Airtel kwa ajili ya kuhakikia na kwamba mifumo yetu imeunganishwa na Nida.

Majukumu yangu kama meneja wa sheria

kutoa ushauri katika mambo mbalimbali ya kisheria kwa kampuni; kuandaa na kujibu notes za kisheria zinazohusu kampuni na nyaraka nyingine za kisheria; kufuatilia kesi zinazohusu kampuni amabzo zipo mahakamani; natoa taarifa za kichunguzi kwa taasisi zinazoombwa taarifa  na nina ninapokea amri ya mahakama.

Elimu yangu ni shahada ya Sheria kutoka UDSM niliyoipata mwaka 2006

Pia nina certificate basic Skills ya Kompyuta niliipata chuo Kikuu Cha DSM mwaka 2011.

Pia nilipojiunga na Airtel mwaka 2014 nilipata mafunzo ya ziada ikiwemo ujuzi wa mifumo ambayo ninaitumia kwa kazi yangu ya kila siku.

Nilipata taaluma ya kutumia mifumo inayotumika kuhifadhi mifumo ya fedha inayofanywa na mteja, mafunzo hayo niliyapata kwa muda wa wiki mbili

Pia nilipata Mafunzo kuhusiana na mfumo wa business Intelligence (Mfumo unaotunza taarifa za mteja).

Pia mwaka  2019, nilipata Mafunzo ya mfumo wa kutunza taarifa za usajili wa mteja wa kibiometric na katika mafunzo hayo tunafundishwa mambo mbalimbali ikiwemo jinsi taarifa zinavyochukuliwa na kuhifadhiwa katika mifumo hiyo, usalama wa mifumo endapo kunatikea tatizo la kimtandao na la kiteknolojia Nini ambacho tunatakiwa kufanya na utunzaji wa zile taarifa kwa ujumla.

Mfumo huu wa Agile (mfumo wa kutunza taarifa za usajili za mteja kwa njia ya biometric), mtumiaji wa mfumo, mfumo huu unatunza taarifa na miamala pale ambapo mteja anapotuma au kupokea pesa.

 Mfumo wa business Intelligence ni pale ambapo mteja anapofanya mawasiliano akiwa karibu na mnara, yale mawasiliano yake yanachukuliwa na kwenda kutunzwa kwenye server na baada ya hapo unapotaka kuifikia hii taarifa unatumia mfumo huu wa business Intelligence.

Mawasiliano haya ni pale mtaja anapopiga simu, anapopokea simu na hata anapotumia huduma ya internet.

Mifumo hiyo miliwi niliyoitaja nimeitumua tangu nilipojiunga na Airtel mpka sasa, lakini mwaka 2019 ndio nilianza kutumia mfuno wa Agile.

Shahidi: Taarifa ninazotoa za kiuchunguzi kwa taasisi au vyombo vya kiuchunguzi ni Jeshi la Polisi, PCCB, Tume ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya, TCRA na tunatoa kwa FIU (Financial Intelligence Unit) na mteja binafsi pia anaruhusiwa kupewa taarifa.

Vyombo hivyo huwa vinaomba taarifa za miamala ya kifedha, kupiga na kupokea simu pamoja na usajili.

Shahidi: Taratibu za kuomba taarifa za kuchunguzi ni hizi hapa,

Kwanza, chombo au taasisi ya kuomba uchunguzi huwa ina leta barua ya maombi na maombi haya yanawasilishwa katika kampuni ya Airtel kupitia upande wetu wa mapokezi, yakishapokelewa yananakiliwa katika kitabu chetu na kupelekwa kitengo cha sheria na baada ya hapo Mkuu wetu wa Kitengo cha sheria anasaini kuyafanyia kazi maombi hayo.

Baada ya kukamilisha vitu vyote, ofisa Sheria ana hakiki barua hiyo na kiuchunguza vizur ikiwemo anuani husika na nembo husika na kuhakiki ni taarifa gani zimeombwa? Na je taarifa hizo Ni za kiuchunguzi? Na kama taarifa hizi sio za kiuchunguzi hatuwezi kuzifanyia kazi, pia barua hiyo iwe na mhuri kutoka taasisi husika.

Watu wanaoshughulikia maombi haya ya kiuchunguzi ni wawili ambao ni mimi na mwenzangu.

Shahidi: Baada ya kujiridhisha tunaingia katika mifumo niliyoitaja hapo awali.

Ninapoingia katika kompyuta yangu nainginza Username na Password.

Username na Password naipata kutoka Kitengo cha IT ambapo mimi peke yangu ndio nafahamu na baada ya hapo naingia katika mfumo.

Baada ya hapo naingiza namba ya simu ya mteja na muda ninaoangalia hizo taarifa.

Baada ya kuingia katika mfumo huo, nachakata taarifa na kutozitoa huko zilipohifadhiwa na kuzileta kwenye page yangu.

Baada ya kuweka katika page yangu, naanza tena kuzihakiki taarifa zilizotoka katika mfumo na chombo husika na iliposajiliwa kama ni sahihi na kisha na print.

Nikisha print naangalia tena hiyo nakala niliyoprint na kujiridhisha na barua ya maombi na ni sahihi hicho walichoomba kwa ajili ya uchunguzi Kisha nagonga mhuri na kuandaa cover latter kwa ajili ya kuwasilisha.

Kuna kila mfumo, hivyo kama ni mambo ya financial nayakuta huko na Watu wengine katika taasisi yetu ambao wanapewa access ya kuona taarifa za wateja

Wapo wa aina mbili ambao ni customer Service na Call Center. Hawa ndio wana access ya kuona taarifa za wateja kwa ajili ya huduma za majumbani na biashara.

Ambaye anauwezo wa kuona na hana uwezo wa kufanya kitu chochote kwani taarafa hizo zinakuwa katika mfumo wa Read Only (Yaani taarifa hizo ni kwa ajili ya kusoma) na watu hao wa kuona tu ni Customer Service, Agent, Call Center.

Kwenye kundi la pili ambalo ni kitengo cha Sheria, ambapo sisi tuna access ya kuona, kusoma na kuprint lakini haturuhisiwi kurekebisha na hakuna mtu yoyote ambaye anaweza kuingilia mifumo hiyo.

Pia mifumo hii inalindwa na imewekewa mifumo ya usalama (Firewalls) kwa ajili ya kulinda mifumo na taarifa zake.

Shahidi: Mifumo hii imeunganishwa na Airtel nasema kwamba huwezi kutumia kifaa chochote kuaccess na sababu kubwa ni kwa ajili ya usalama.

Usalama uliopo katika mifumo hiyo, kwanza tuna firewalls ambapo kama kuna mtu anataka kuingia tunapata taarifa, pia internet ikiwa down taarifa za wateja haziwezi kuathiriwa kwa njia yoyote na mfumo wetu ni madhubuti na unafanya kazi sawasawa.

But mfumo huu kuna wakati internet inakuwa down na unakupa ishara.

Wakili: Hebu tueleza kipindi network inapokuwa down taarifa mlizotunza kwenye server huwa zinakuwaje?

Shahidi: Network inapokuwa down, haiwezi kuathiri mifumo yetu au taarifa zilizopo ndani ya mifumo huwa haziguswi au kupata changamoto

Wakili Kitale: Umesema hapa mifumo yenu ni Intelligent (uadilifu) hebu ieleze mahakama uadilifu wa mifumo yenu ikoje?

Shahidi: Hakuna mtu wa kuingilia mifumo, unafanya kazi vizuri muda wote na tuna software ambayo tumeweka ili kuangalia usalama wetu.

Wakili Kitale: Mnamifumo ipi?

Shahidi: Tuna mifumo mitatu.

Mfumo wa kwanza unaitwa Mouituity, hiyo ni kuchukua taarifa za mteja na kuhifadhiwa katika server na endapo tunahitaji kupata taarifa za miamala tunaweze kuangalia katika mfumo huu.

Mfumo wa pili ni Agile- ambapo inahusika na usajili na uhakiki wa namba ya mteja.

Mfumo wa watatu ni Business Intelligence.

Wakili Kitale: Unakumbuka Nini mnamo tarehe 2 mwezi wa saba mwaka 2021?

Julai 2, 2021 nilikuwa ofisi za Airtel Morocco nikiwa nafanya majukumu yangu.

Siku hiyo nikiwa ofisini alikuja Mkuu wa Idara ya Sheria wa Airtel, alinielekeza mimi nishughulikie maombi kutoka ofisi ya uchunguzi wa kisayansi ya Jeshi la Polisi.

Maombi hayo yalikuwa yanataka taarifa za miamala ya fedha katika namba 0782 237913 na namba nyingine ilikuwa 0787 555200 na namba ya tatu ilikuwa 0784 779944 pia barua hiyo iliomba niangalie taarifa za usajili za line hizo.

Baada ya hapo, nilihakiki ile barua address yake kama inatoka taasisi husika, niliangalia barua hiyo kama kweli inaaongelea uchunguzi, taarifa zinazoombwa ni za muda gani na kuhakikisha kama kweli line hizo zimesajiliwa.

Baada ya kujiridhisha niliingia katika kituo changu cha kompyuta kisha nikaingia katika mfumo wa Agile na nikaingiza namba moja ya simu ambayo imeombewa taarifa na kisha ikanitolea taarifa inayohusiana.

Shahidi: Nilipata taarifa za usajili wa namba 0787555200, 0782237913 na 0784 779944 na kisha nikaprint nyaraka zote tatu baada ya kupata taarifa.

Katika mfumo wa obiquity ni lazima uingize namba na muda hivyo nilifanya hivyo kwa namba za simu zote tatu.

Barua hiyo ya Polisi iliomba taarifa za line zote tatu kuanzia 1/6/2020 mpaka 31/7/2020.

Baada ya taarifa hizo kuonekana katika mfumo, nilijiridhisha na kuprint taarifa zote.

Baada ya kuprint, nyaraka hizo nilweka mhuri na kuweka sahihi pamoja na tarehe husika.

Pia niliandaa barua kwa ajili ya kuambatanisha taarifa ambazo niliandaa.

Wakili Kitale: Ukiona barua hizo utazitambuaje?

Shahidi: Nitazitambua kwa saini yangu, mhuri wa kampuni ya Airtel PLC, tarehe husika na namba za simu ambazo nimezitolea taarifa ambazo ni 0787 555,200, 0782 237913 na 0784779944.

Kuhusu taarifa za miamala ya fedha ambayo nimeitolea taarifa katika simu hizo, Nitazitambua kwanza namba za simu ambazo zinaonekana katika ile taarifa, mhuri wa kampuni, saini yangu na tarehe.

Wakili Kitale: Shahidi hebu shika nyaraka hizi na utuonyeshe ipi ni taarifa ya miamala ya fedha ipi ni taarifa ya usajili wa namba hizo.

Shahidi amezitambua nyaraka hizi moja baada ya nyingine kwa kuzionyesha mahakaman.




Shahidi: Naomba mahakama ipokee nyaraka hizi zitumike kielelezo katika kesi hii

Upande wa mashtaka wamewapatia nyaraka hizo mawakili wa upande wa uetetezi ili waweze kuzipitia.

Kibatala: Mheshimiwa jaji kwani niaba ya mshtakiwa wa nne (Freeman Mbowe) hatuna pingamizi dhidi ya nyaraka hizi.

Wakili Mtobesya: Kwa niamba ya mshtakiwa wa kwanza (Halfan Bwire)  Hatuna pingamizi.


Wakili Mallya: Kwaniaba ya mshtakiwa wa pili (Adam Kasekwa) hatuna pingamizi.

Wakili Matata: Mheshimiwa Jaji kwa niaba ya mshtakiwa wa tatu (Mohamed Ling'wenya) hatuna pingamizi.

#KesiMbowe #MwananchiUpdates

Jaji- Baada ya upande mashtaka kuomba nyaraka hizi zipokelewe na kwa vile upande wahawajapinga kupokelewa kwa nyaraka hizi, hivyo Mahakama imevipokea vielelezo hivyo kama ifuatavyo

Jaji- Barua ya uchunguzi wa Kisayansi kutoka Jeshi ya Polisi ya tarehe 2/7/2021 imepokelewa na kuwa kielelezo namba 15.

Barua ya Jeshi la Polisi ya tarehe 1/7/2021 itakuwa kielelzo namba 16 chha upande wa mashtaka.

Taarifa ya usajili wa namba 0784 77 99 44 kuwa kielelezo namba 17.

Taarifa ya usajili wa namba 0782 237913 kuwa kielelezo namba 18.

Taarifa ya usajili wa namba 0787 555200, imekuwa kielelezo namba 19.

Taarifa ya print Out ya miamala ya fedha namba 0787 555200 na kuwa kielelezo namba 20.

Taarifa ya print out ya miamala ya fedha namba 0784 779944, imekuwa kielelezo namba 21 cha upande wa mashtaka.

Jaji: Hivyo mahakama inaelekeza nyaraka hizi zisomwe na shahidi.

Shahidi ameanza kusoma nyaraka hizo moja baada ya nyingine kwa kutaja namba hizo za simu na majina yaliyosajiliwa na miamala iliyotumwa katika kesi hizo.

Shahidi: Katika namba 0784 779944 imesajili kwa jina la Freeman Aikaeli Mbowe (Mshtakiwa wa nne) katika kesi hiyo.

Shahidi: Namba 0787 555 200 imesajiliwa kwa jina la Denis Leo Urio.

Shahidi: Namba ya simu 0782 237913, imesajiliwa kwa jina la Halfan Bwire Hassan (Mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo)

Shahidi- Muamala iliyotumwa tarehe 20/7/2020 kwenye namba 0787 555 200, ambayo kwa mujibu wa kielelezo namba 20, namba hiyo imesajiliwa kwa jina la Denis Leo Urio, ilipokea Sh 500,000 kutoka kwenye namba ambayo ni Collection Account 780900174, na mhusika mwenye namba ya Airtel 0787 555200 alikuwa na salio kiasi cha Sh 46, 646 katika simu yake na hivyo akawa na jumla ya kiasi cha Sh 546,646 baada ya kuingizwa Muamala wa Sh 500,000

Shahidi: Pia tarehe 22/7/2020, namba ya simu ya Denis Urio (0787 555 200) ilipokea fedha Sh 199,000 kutoka namba 0780 900244.

Shahidi: Tarehe 31/7/2020 namba 0784 779944, ambayo katika kielelezo namba 21,  imesajiliwa kwa jina la Freeman Aikaeli Mbowe, ilituma fedha kiasi cha Sh80,000 kwenda namba 0782 237913 yenye jina la usajili Halfan Bwire Hassan.

Shahidi: Hiyo Tarehe 20/7/2020 Muamala mwingine uliofanyika kwa namba ya 0787 555200 alituma kiais Cha Sh 300,000 kwenda namba 0785191954.

Wakili Kitale: Mheshimiwa Jaji kwa upande wetu ni hayo tu.

Kibatala: Mheshimiwa Jaji nilikuwa nashauria na wenzangu upande wa mashtaka tuahirishe kwa muda wa dakika 45.

Jaji: Basi kama alivyoomba upande wa utetezi na kukubaliana na wenzao wa upande wa mashtaka, naahirisha kesi hii kwa dakika 45 hadi saa 8:30 mchana itakapoendelea kwa shahidi kuhojiwa na upande wa uetetezi.


Baada ya kuahirishwa kwa muda kwaajili ya mapumziko sasa muda si mrefu kesi hiyo itaendelea tena

 Jaji ameshaingia mahakamani kwa ajili ya kuendelea na kesi na kwasasa ni upande wa utetezi kumhoji shahadi kuhusiana na ushahidi aliotua

Shahidi aanaza kuhojiwa na wakili wa utetezi Jeremiah Mtobesya

Wakili: Shahidi Nilisikia unasema mnafabya audit ya mifumo Ni sahihi?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Ni mifumo ya Nini?

Wakili: Mifumo inayotumika kuhifadhi taarifa.

Wakili: Nitakuwa sahihi nikisema audit unafanya na IT Department na kampuni za audit?

Shahidi: Inategemea

Wakili: Kwenye Ushahidi wako ulielezea kuwa ulifanya kazi kwenye IT Department?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Mheshimiwa Jaji naomba nipatiwe kielelezo namba 15 na 16 vilivyolewa na upande wa mashtaka.

Wakili Mtobesya anapewa vielelezo hivyo na kumpatia shahidi.

Wakili: Mheshiwa Jaji narejea katika kielelezo namba 15 ambayo ni barua ya uchunguzi wa kisayansi kutoka Jeshi la Polisi iliyotumwa Airtel kuomba taarifa za wateja, ieleze mahakama imeandaliwa chini ya kifungu namba ngapi?

Shahidi: Imeandaliwa chini ya kifungu namba 34 chini ya sheria ya makosa ya mtandano.

Wakili: Katika shughuli zako za kila siku ulishawahi kukutana na Sheria hiyo?

Shahidi: Ndio.

Wakili: Huwa mnalindaje taarifa za wateja wenu?

Shahidi: Mteja kwetu ni mtu muhimu hivyo tunayemheshimu na kumlinda na hatuwezi kutoa taarifa ya mteja bila muongozo wowote au court order na ndio maana tunatoa taarifa kwa taasisi husika.

Wakili: Kama kweli mnalinda taarifa za wateja wenu kwanini mmetoa taarifa kwa hawa wateja watatu?

Wakili: Kwa mujibu wa sheria ya makosa ya mtandao, kifungu cha 34 (1) Mheshimiwa Jaji mimi nilitenda majukumu yangu kwa mujibu wa sheria na miongozo mwingine.

Wakili: Sawa mwanasheria, sasa kwanini mlitoa taarifa za wateja wenu?

Shahidi: Mimi nilitekekeza majukumu yangu kwa mujibu wa sheria na miongozo iliyopo na sio kwamba natumia sharia… zipo sheria nyingi ambazo zimetumika hapa kutekeleza majukumu yangu.

Wakili: Kwa maelezo yako, hizi taarifa za wateja zinazosajikiwa na kuingizwa na msajili, je Msajili anaweza kuonekana kwenye hizo taarifa? Yaani kwamba Mtobesya amesajiliwa na mtu flani? Msajili anaweza kuonekana hapo?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Sasa mtu anajuaje?

Shahidi: Kimya

Wakili: Ulileta taarifa hapa, zote hazionyeshi jina la msajili sindio?

Shahidi: Ndio.

Wakili: Niliona unaongea kwa umaridadi sana, ulimueleza Jaji kuwa wewe ulishakuwa msajili wa line?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Unafahamu watu wanaoitwa hackers?

Shahidi: Nina ufahamu nao.

Mtobesya: Unawaelewaje?

Shahidi: Nawaelewa ni wale watu wanaoingilia mifumo ya taarifa.

Mtobesya: Ikiwemo data?

Shahidi: Ndio

Wakili Mtobesya: Ulisema baada ya kukamilisha taarifa hizo, ulienda kuhojiwa Central Polisi Dsm na Inspekta Swilla je ilikuwa ni tarehe gani? Kama unakumbuka.

Shahidi: Sikumbuki kama nitapewa maelezo hayo itakuwa vizuri.

Mtobesya: Unakumbuka ilikuwa tarehe ngapi?

Mtobesya: Mheshimiwa Jaji tunaomba Question statement ya shahidi.

Mtobesya: Haya soma hiyo statement kuanzia kwenye maelezo yako.

Shahidi: Nakumbuka 2/7/2020 nilipokea barua kutoka Idara ya uchunguzi wa Sayansi ya Polisi iliomba niwapatie taarifa ya miamala ya fedha na usajili wa namba.

Mtobesya: Sasa nita refer kwenye hayo maelezo yako, sasa mueleze Jaji kama ulisema katika ushahidi wako asubuhi kuwa wewe access ya kuingia katika mifumo.

Shahidi: Hapana Sikusema.

Mtobesya: Nilisikia ulisema kwenye ushahidi wako kuhusu ubora ya mifumo wakati wa kuprint, je kwenye maelezo yako uliyotoa polisi hayo maneno yapo hapo kwenye hiyo karatasi?

Shahidi: Hapana.

Mtobesya: Ungependa hayo maelezo yako uliyoyasoma sasa hivi yaingie kwenye rekodi za Mahakama?

Shahidi: Ningepewa muda niweze kushauriana na upande wa mashtaka.

Mtobesya: Hutaki?

Shahidi: Nimeshatoa vielelezo, hivyo siwezi kusema chochote.

Mtobesya: Kwa hiyo nyaraka hii nyiingie au ikatae?

Shahidi: Nimeshasema tayari.

Mtobesya: Mheshimiwa Jaji naomba guidance (Muongozo) wa mahakama.

Jaji: Kwani wewe umesikiaje?

Mtobesya: Mimi naomba ajibu swali langu shahidi.

Mtobesya: Mheshimiwa Jaji sisi tunaomba kui' move Mahakama kuwa tunaomba maelezo yake aliyoyatia Polisi yaingie katika taarifa za mahakama kwa kutumia Kifungu cha 154 na Pamoja na 164 (1)C ya Sheria ya Ushahidi.

Mtobesya: Hizi ni taarifa muhimu kwetu, hivyo hazikutakiwa kuwa hold.

Mtobesya: Tena shahidi anafanya hivyo akiwa katika witness box.

Mtobesya: Ukisoma Kifungu Cha 246 cha CPA, Kina sema Mshitakiwa apewe The Whole Substance, there is a reason to that

Mtobesya: Kwa kusema hayo Mheshimiwa Jaji naomba statement iweze kuingizwa ili niweze kuitumia kum contradict.

Mtobesya: Hivyo tunaomba taarifa hizi ziingie kwenye record ya mahakama.

Akijibu hoja ya Mtobesya, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando: Hiyo sio contradiction.

Kidando: Mheshimiwa Jaji, shahidi aliyopo mahakamani ameulizwa mambo manne na katika majibu yake ametanguliwa na neno kuwa sikusema, sasa suala la kujiuliza hapa suala la kuwa hakusema linakinzana vipi na nini?

Kidando: Sisi tunaona wakili Mtobesya ombi alilowasilisha halina mashiko kisheria na ameshindwa kufikia kikwazo hicho cha kuonyesha consistent na ndio maana anaomba statement hiyo aiote kama kielelezo na sisi tunasema hana nafasi ya kuitoa questions statement hiyo ya shahidi kwa Mahakama.

Kidando:  Tunasisitiza huu ni upande wa cross examination, hivyo Wakili msomi Mtobesya angejielekeza katika kuuliza maswali.

Kidando: Hivyo tunaomba ombi hilo likataliwe na tuendelee na cross examination kwa mujibu wa sheria.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Pius Hilla: Mheshimiwa Jaji nina nyongeza kidogo, vifungu alivyotumia wakili msoni Mtobesya sio sahihi.

Hilla: Mheshimiwa Jaji mwenzangu Wakili Chavula nae anataka kuongezwa kujibu hoja hiyo.

Hata hivyo kabla ya Chavula haijaanza kujibu hoja ...amesimama Mtobesya na kusema Mheshimiwa Jaji naomba kuondoa pingamizi hili.

Kidando: Mheshimiwa Jaji sisi tumesha- concede kwa kiasi kikubwa, hivyo tunaomba wao waendelee tu ...Wala wasi- withdraw nyaraka hiyo.

Mtobesya: Mheshimiwa Jaji mimi naomba ku- withdraw sina nia ya kuendelea na pingamizi hilo.

Kicheko mahakamani hahahhahaha.

Kibatala anasimama na kwenda kujadiliana na mawakili wa upande wa mashtaka.

Kibalata: Mheshimiwa Jaji naomba sekunde 30 kujadiliana na wenzangu.

Baada ya majadiliano hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abdallah Chavula anasimama na kuridhia kuwa upande wa mashtaka wamekubaliana kuondoa pingamizi hilo.

Wakili Chavula: Mheshimiwa hatuna pingamizi juu ya wenzetu kuondoa ku-withdraw nyaraka hiyo.

Jaji: Kama walichoomba upande wa utetezi na kuridhia upande wa mashtaka naondoa nyaraka hii.

Mawakili wa pande zote wanasimama na kuinamisha kichwa kwa Jaji kuashiria kuwa wamekubali.

Baada ya Jaji kuondoa pingamizi hilo, ameelekeza wakili Mtobesya kuendelea kumhoji shahidi wa upande wa mashtaka.

Mtobesya: Sasa mliwezaje kulinda taarifa za watu wengine ambao wamefanya miamala kwenye namba za simu hizo?

Shahidi: Taarifa hizi zimeombwa na Mamlaka husika ambayo iko authorized (Jeshi la Polisi) na hakuna namna ambavyo tungefanya kwa kuwa mfumo wetu ulitoa taarifa kuanzia Juni 1, 2020 hadi Julai 31, 2020.

Mtobesya: Kwa taarifa hiyo mnatambua hiyo ni taraarifa ya mtu fulani au hakiwezi?

Mtobesya:  Kupitia mfumo huo wa taarifa hiyo inaweza kueleza  mtu flani alituma hela kwa sababu gani?

Shahidi: Hapana haiwezi

Mtobesya: Mheshimiwa kwa upande wangu ni hayo tu.

Kwa Sasa i zamu ya Wakili Mallya kumuuliza shahidi.

Mallya: Shahidi unafahamu Mbowe anashtakiwa kwa kesi gani?

Shahidi: Sifahamu.

Mallya: Sasa Mimi nakufahamisha Mbowe anatuhumiwa kutumia fedha hao wenzake kwa ajili kufanya matukio ya ugaidi na upo hapa kwa ajili ya hilo.

Shahidi: Kimya

Mallya: Barua ya Julai 2, 2021 kutoka Jeshi la Polisi, iliomba idadi ya miamala ya fedha ya watu wangapi?

Shahidi: Haijafafanua.

Mallya: Muamala wa mwisho inaonyesha ilitumiwa Julai 31, 2020 kiasi cha Sh80, 000 kwenda kwa Bwire, sasa mbona namba nyingine hukuitaja hapa mahakamani?

Shahidi: Oversight

Mallya: Sasa nikwambie tu hiyo namba ya Bwire alikuwa ametuma hela ACP Kingai Sh80, 000 mbona hukutuelezea hapa mahakama wakati unatoa ushahidi? kuhusiana na muamala huo wa Bwire kumtumia Kingai pesa hiyo?

Shahidi: Nilipitiwa

Mallya: Unafahamu kuna miamala ya waziri wa zamani ulinzi alikuwa anamtumia fedha Bwire? kwa sababu wamefanya kazi wote?

Jaji: Mhh

Jaji: Hizo information umezipata wapi?

Mallya: Kutoka kwa watuhumiwa mwenyewe (Bwire)

Jaji: Chini ya kiapo?

Mallya: Kimya

Jaji: Unafikiri mwenyewe atakuja kutoa ushahidi hapa mahakama.

Mallya: Hatuzuiwi Mheshimiwa Jaji kumuita aje kuwa shahidi wetu.

Jaji: Mimi nafikiri ujikite kuuliza maswali kwenye ushahidi uliotolewa hapa mahakakani, kuliko kuongoza vitu ambavyo havipo hapa.

Wakati wa majibishano hayo, wakili Kidando amesimama na kabla ya kuongea.

Jaji anamuelekeza Mallya ajielekeze kwenye ushahidi.

Kidando: Mheshimiwa Jaji tunapinga maswali hayo ya wakili Mallya kumuuliza shahidi hata kama anajua.

Mallya: Sawa mheshimiwa Jaji nashukuru nitajielekeza.

Mallya:  Sasa Shahidi Oversite yako (Yaani kupitiwa) unafikiri nani atakuja ku-cover?

Shahidi: Sifahamu.

Mallya: Je taarifa zenu za usajili (Format) zina fanana

Shahidi: Ndiyo muundo au format unafanana

Mallya: Sasa hapa umesajili watu mmoja anaitwa Mbowe, Katika Kielelezo namba 18 Je unaweza kuona sehemu ya juu imeandikwa Kanda, Je Kanda gani

Shahidi: Morogoro

Mallya ukitizama pia taarifa za Denis Urio, sehemu ya Kanda kwa Denis Urio, ipo au haipo

 Shahidi: Ipo kwa Denis Urio

Mallya:  Sasa angalia kielelezo namba 17 cha Freeman Mbowe kama Kuna sehemu ya kanda au mnapendelea Wanajeshi.. Ukiona Mwambie Mheshimiwa Jaji

Shahidi:  Haionekani

Mallya: Haionekani au haijaandikwa

 Shahidi: Haijaandikwa

Mallya:  Ni sahihi sasa kwa kuwa mtu anaitwa Freeman Mbowe, haina Sehemu imeandikwa Kanda ni sahihi hizo taarifa zipo tofauti

Shahidi: Ndiyo neno kanda halija onekana

Mallya: Ulitoa hiyo Clarification wakati wa Chief Examination

Shahidi: Sikuulizwa

Mallya: Nakushauri jibu ulitoa au hukutoa?

Shahidi: Nimeshajibu

Mallya: Mheshimiwa Jaji naomba ajibu swali langu sasa

Jaji:  Umeelewa swali?

Shahidi: Sikutoa Mheshimiwa Jaji

Mallya: Kwenye kielelezo namba 20 muamala wa tarehe 20 Julai 2020, Ulisema P to P maana yake ni nini

Shahidi: Airtel kwemda Airtel

Mallya: Na hiyo cash in..?

Shahidi: Namba ya muhusika ambayo imepokea?

Mallya: Ilipokea kutoka kwa wakala itaandikaje..?

Shahidi: zote zinaonekana kama Cash In. Mteja Kwa Mteja ni P to P

Mallya:  Sasa mimi Interest yangu ni tarehe 20 Julai 2020, cash in ni Wakala

Shahidi: Kuna ufafanuzi

Mallya: Ufafanuzi utampatia dada yangu Kitale, mie nataka majibu

Mallya:  Katika hawa washitakiwa wanne kuna hata mmoja kasajiliwa kama Wakala?

Shahidi: Mimi sifahamu

Mallya: Mheshimiwa Jaji nina maswali bado kwa shahidi wetu, na muda umetutupa mkono, ningeleta ombi kwako tuhairishe hadi Kesho tuendelee na Mahakama

Kibatala: Mheshimiwa Jaji kabla ya kufunga naomba kutoa tarifa kuwa kutokana na nature ya ushahidi wake tunaweza kesho tukamaliza mapema kuhoji, hivyo tunawaomba wenzetu upande wa mashtaka kama wana shahidi ambaye anaushahidi mfupi wamlete ili tuweze kuendelea naye.

Kidindo: Tunaendelea na mawasiliano na shahidi wetu kwa sababu hadi mchana alikuwa ametupa taarifa kuwa anauguliwa na baba yake mzazi, hivyo tutaendelea kuwasiliana naye ili kujua kama hali yake inaendelea vizuri ili aje.

Jaji: Naahirisha kesi hii hadi kesho, Januari 14, 2022 saa 3:00 asubuhi.

Jaji: Naelekeza shahidi kesho ufikie mahakmani hapa na washtakiwa wataendelea kuwa chini ya usimamizi wa magereza.

Niwatakie jioni njema.