Mwanaume alivyouawa mbele ya familia yake Morogoro

Editha Sailen (kulia) ambaye ni mke wa kijana Henry Charles aliyeuawa na watu wasiojulikana baada ya kuvamiwa nyumbani kwake na kuchomwa kisu shingoni. Picha Hamida Shariff

Muktasari:

  • Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fotunatus Musilimu amesema kuwa ni mapema kuhusisha moja kwa moja tukio hílo na Panya road, kwani uchunguzi bado unaendelea kufanyika.

Morogoro. Hofu imetanda kwa wananchi wa Kata ya Kihonda Manispaa ya Morogoro baada ya watu wasiofahamika kumvamia mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Henry Charles (45) na kumuua kwa kumchoma kisu shingoni na mgongoni kisha kuondoka na simu mbili na kiasi cha fedha ambazo hazijafahamika.

Mauaji hayo yalitokea usiku wa kuamkia jana Novemba 13, huku mke wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Editha Saileni na watoto wao Witness Henry na Wilson Henry wakishuhudia.


Akizungumzia tukio hilo leo Novemba 14, Editha amesema kuwa majira ya saa 4 usiku kundi la watu watatu waliokuwa wameficha nyuso zao kwa vitambaa walivunja mlango na kuingia moja kwa moja chumbani na kuanza kumshambulia mume wake huku wakimtaka atoe pesa alizoweka kwenye suruali.

Editha amesema watu hao waliwaonya na watoto wasipige kelele hivyo alichukua suruali yenye pesa na kumpa.

"Wakati mwanangu anatoa suruali kumbe tayari wale watu walishamchoma kisu mume wangu na kumburuza hadi nje ya nyumba na kisha kukimbia.

“Nilipotoka nje na watoto nikakuta mume wangu kaanguka chini damu nyingi zikiwa zinamtoka huku akiniambia kwa kurudiarudia mke wangu nakufa," amesema Editha.

Amesema baada ya kupiga kelele majirani walitoka na wakampeleka majeruhi kwenye zahanati ya jirani hata hivyo waliwapa barua ua kwenda hospitali ya rufaa na alipofikishwa daktari alithibitisha kuwa tayari amekwishafariki dunia.

"Mume wangu mpole hana ugomvi na mtu shughuli zake ni za gereji, yaani nashindwa kujua ameuawa na kina nani na kisa nini maana hapa sebureni kulikuwa na baadhi ya vitu vya thamani kama luninga, king'amuzi lakini hawajachukua hata kimoja," amesema Editha.

Amesema kuwa baada ya mauaji hayo binti yake ambaye ameanza mitihani ya kumaliza kidato cha nne alichukuliwa na baadhi ya jamaa kwa ajili ya kumnasihi ili aweze kufanya mitihani yake.

"Naumia sana mwanangu ameshuhudia baba yake akishambuliwa kwa kisu hadi kupoteza maisha na leo hii yuko kwenye chumba cha mtihani sijui kama ataweza kufanya vizuri ni tukio lisilofutika kwenye akili zetu na wanangu," amesema Editha.

Kwa upande wake mama mzazi wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Roza Sengo amesema kuwa Mara ya mwisho kuzungumza na mwanaye ilikuwa ni wiki mbili zilizopita ambapo alimpigia simu na kumwambia kwamba atamtumia pesa kwa ajili ya kununua mahitaji mbalimbali ya nyumbani.

"Aliniambia mama kuna hela nitakutumia siku mbili hizi ikusaidie kidogo matumizi nikamwambia nitashukuru mwanangu baada ya hapo sikupokea simu yake tena mpaka jana nilipopewa taarifa kuwa mwanangu ameuawa," amesema Roza.

Amesema mwanaye huyo aliyeuawa ni wa watano kati ya watoto wake 15 aliowazaa na kwamba alikuwa akingumza naye mara kwa mara na kwenda kumuona kijijini Gairo.

Mama huyo ambaye anakadiriwa kuwa na umri zaidi ya miaka 80 ameliomba jeshi la Polisi kuhakikisha wanawapata waliohusika kumuua mwanaye ili nao wachukuliwe hatua za kisheria.

"Najua adhabu yoyote watakayopata haiwezi kufuta uchungu nilionao lakini walau itanipa imani kwa Serikali yangu, mimi umri wangu huu siwezi kulima, siwezi kufanya kazi yoyote tegemeo langu ni watoto akiwemo huyu aliyekatishwa uhai wake, namuomba Rais wangu mama Samia Suluhu Hassan na polisi hawa waliomua mwanangu wapatikane," amesema Roza.

Ally Mohamed ambaye ni jirani wa marehemu, amesema rafiki yake alikuwa akifanya kazi kwenye gereji moja iliyopo maeneo ya Modeko na alikuwa karibu mcheshi na asiyependa ugomvi hivyo mauaji yake yameacha maswali mengi kwake.

Hata hivyo amesema kuwa kwa sasa Kama wananchi wa mtaa huo wameingia hofu kwa kuwa siku ilipotokea mauaji hayo pia yalitokea matukio mengine mawili ya watu kuvamia nyumba na kuiba mali za ndani.

"Siwezi kusema tukio hili limefanywa na Panya road lakini tuna wasiwasi kwamba huenda matukio haya yakawa ndio muendelezo, maana juzi yametokea matukio mawili na hili la tatu na zamani kulikuwa na hakuna matukio kama haya," amesema Mohamed.

Naye Aisha Seif amesema akiwa amelala na mume wake alisikia kelele za marehemu akiomba msaada na walipotoka walimkuta marehemu ameanguka chini huku damu zikimtoka shingoni.


"Kelele tulizisikia lakini mwanzoni tukajua labda walevi wanagombana lakini kadri tulivyokuwa tunasikiliza tukagundua kuwa ni jiraji yetu Henry na ndipo nilipomwambia mume wangu tutoke tukashuhudie, na tulipotoka tukamkuta akiwa na hali mbaya," amesema Aisha.

Amesema kutokana na hofu iliyopo kwenye mtaa huo kwa sasa wamekuwa wakifunga milango usiku na mchana na watu wamekuwa wakirudi kwenye shughuli zao mapema.

Mwenyekiti wa mtaa huo Mazimba John amesema kuwa alipata taarifa za tulio hilo kutoka kwa balozi wake na alifika eneo la tukio alimkuta Henry akiwa anavuta pumzi nzito huku damu nyingi zikimtoka eneo la shingoni.

Akithibitisha tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fotunatus Musilimu amesema kuwa ni mapema kuhusisha moja kwa moja tukio hílo na Panya road, kwani uchunguzi bado unaendelea kufanyika.

Hata hivyo, amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu alikuwa anafanya biashara ya mafuta ya dizeli ya kupima maarufu kama videbe.

Kamanda Musilimu pia amefika eneo la tukio na kuzungumza na wafiwa na kuwasihi wawe na uvumilivu wakati Polisi wakiendelea na uchunguzi wa tukio hilo.