Mwandishi Mwananchi apongeza viongozi kuwahi Hanang, fedha zielekezwe kwa waathirika

Hali ilivyo kwenye mji mdogo wa Katesh wilayani Hanang' Mkoani Manyara baada ya kutokea mafuriko.

Muktasari:

  • Mwandishi Mkuu wa Mwananchi ameipongeza Serikali kwa kujitoa kwao katika kusaidia waathirika wa maafa ya Hanang, aitaka isihie hapo bali iwape makazi ya kudumu waliokubwa na changamoto, pamoja na kuwaomba wadau kujitokeza kutoa mchango.

Dar es Salaam. Mwandishi Mkuu wa Gazeti la Mwananchi, Elias Msuya amefurahishwa na namna viongozi wa Serikali kwa umoja wao walivyojitoa kwenda Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara kulikotokea maafa ya maporomoko ya matope, mawe na miti, yaliosababisha vifo vya watu 69.

Maafa hayo yaliyosababisha majeruhi zaidi ya 100; yalitokea alfajiri ya Jumapili Desemba 3, 2023 katika mji mdogo wa Katesh na vitongoji vya karibu vikiwemo ya Jorodom, Ganana, Katesh na Dumbeta pamoja na vijiji vya Gendabi na Sarijandu.

Chanzo cha maafa hayo ni kumeguka sehemu ya Mlima Hanang yenye miamba dhoofu iliyonyonya maji ya mvua, hivyo kuporomoko na kutengeneza tope lililokwenda katika makazi na maeneo ya biashara.

Msuya ameeleza hayo leo Jumatano Desemba 6, 2023 katika mjadala wa Mwananchi Space uliokuwa na mada ya ‘Kama Taifa, tuna utayari kukabiliana na majanga?

“Viongozi wamesimamia uokoaji na kuwasaidia waathirika wa maafa, tumeona pia mamlaka na mashirika ya kiserikali zikijaribu kurudisha miundombinu iliyoharibiwa. Kwa kiasi fulani Serikali imeonyesha utayari wa kukabiliana hilo la janga ingawa kuna vifo na majeruhi,” amesema na kuongeza;

“Imeonekana kuna uwajibikaji wa haraka ulionyeshwa na Serikali hili janga na la asili ambalo linaweza kutokea katika mataifa mbalimbali yaliyoendelea, hivyo hatuwezi kuilaumua moja kwa moja Serikali.”

Msuya ameipongeza Serikali kwa uharaka wake wa kurekebisha baadhi ya miundombinu iliyoharibiwa ikiwemo barabara kuu ya Manyara hadi Singida, njia za umeme na huduma ya afya.

Hata hivyo, Msuya amesema hiyo pekee haitoshi bali Serikali iende mbele zaidi kwa kuwasaidia waathirika ikiwemo kuwapa makazi maalumu ya kudumu wale wote waliokumbwa na maafa hayo ambao hivi sasa wamewekwa katika kambi za shule.

“Pia, tusiichaie Serikali bali wadau mbalimbali wajitokeza kutoa misaada na michango kuwasaidia waathirika hawa maana ni ndugu zetu. Tuna mashirika ya kimataifa na mabalozi ambao kwa hali hii wanaweza kutoa mchango wao,” amesema

Msuya amesema fedha zitakazopatikana kutoka kwa wadau mbalimbali: “Ziende kuwasaidia waathirika wenyewe na si kujenga miundombinu ya Serikali kama tulivyokwisha kushuhudia huko nyuma.”

Mkazi wa Hanang, Daxo Anania amesema maeneo ya Gendabi mabomba ya maji yameharibiwa akisema hadi sasa hakuna huduma ya maji, ingawa kumekuwa na jitihada kubwa kwa Serikali.

“Tumesikia viongozi wameagiza mji usafishike haraka, wanajeshi wanajitahidi lakini si kazi rahisi kwasababu mpaka sasa bado maji yanatiririka. Bado kunahitajika watu wengi wa msaada wawepo hasa msaada wa chakula, magodoro na wanaojiweza wanaomba hifadhi kwa muda.

“bado kunahitajika msaada tunashkuru na tunazidi kuomba raia wema kama wanatoa msaada kwa njia sahihi,” amesema Anania.

Lakini Peter Kazungu akichangia mjadala huo amekuwa na maoni tofauti akidai hajaona nguvu katika uokoaji hasa wa haraka.