Idadi vifo Hanang yafikia 69

Eneo la Katesh, Hanang mkoani Manyara lililokumbwa na mafuriko ambayo yamesababisha Mlima Hanang kutoa tope jingi na kusababisha maafa ya watu na uharibifu wa maji. Picha na Mohamed Hamad.

Muktasari:

  • Mfanyabiashara maarufu nchini, Azim Dewji ameahidi kutoa msaada wenye thamani ya Sh10 milioni kuwashika mkono wanawake na watoto walioathiriwa na maporomoko hayo.

Hanang. Vifo vilivyotokana na maporomoko ya tope kutoka Mlima Hanang mkoani Manyara, vimefikia 69 baada ya miili minne kupatikana.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema hayo leo Jumatano Desemba 6, 2023 alipozungumza na waandishi wa habari wilayani Hanang.

Amesema kati ya miili hiyo, wanawake ni wawili na wanaume ni wawili.

Kuhusu majeruhi, amesema idadi ilikuwa 117, mmoja akafariki dunia na kwamba, waliobaki hospitalini hivi sasa ni 45 baada ya wengine kuruhusiwa.

Wakati huohuo, timu ya wataalamu kutoka Dar es Salaam imewasili mkoani Manyara kuchunguza maporomoko hayo.

"Tupo hapa Katesh kwa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan aliyetaka tufanye utafiti wa nini sababu ya Mlima Hanang kutiririsha tope lililosababisha madhara makubwa kwa jamii vikiwamo vifo,” amesema mtafiti Kaya Kimani, kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm).

Kimani amesema, "tumeweka kambi hapa Katesh, tunaendelea na tafiti za Mlima Hanang kisha tutatoa taarifa na kushauri jamii.”

Kwa upande wake, Dk Gama Jeremia kutoka chuo hicho amesema wameshuhudia hali iliyotokea ambayo wanaendelea kuifanyia utafiti kubaini chanzo cha tope hilo.

"Tumeshuhudia tope jingi kutoka Mlima Hanang leo ni siku ya nne wakazi wa Katesh wanahangaika kulitoa nje ya nyumba zao, huku mitaro ikiendelea kuzibuliwa ili maji yapite,” amesema.

Katika hatua nyingine, mfanyabiashara maarufu nchini, Azim Dewji ameahidi kutoa vitu vyenye thamani ya Sh10 milioni kuwashika mkono wanawake na watoto walioathiriwa na maporomoko hayo.

Amesema msaada huo ni kutokana na maombi ya Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania (UWT), unaolenga kusaidia kinamama na watoto waliopata athari katika kadhia hiyo.

Dewji amewahamasisha wanamichezo na wafanyabiashara wengine kuendelea kutoa misaada kwa kile ambacho wamejaliwa.

"Nilizungumza na mwenyekiti wa UWT jana Desemba 5, 2023 sisi kama kampuni tunamuunga mkono kwa kutoa nguo na chakula, msaada wenye thamani ya Sh10 milioni, hadi Ijumaa Desemba 8,2023 nitakuwa nimekabidhi,” amesema.

"Watanzania wote waelewe maafa hayana hodi, hivyo kila mtu ajitolee, wengine nao waguswe."

Kupitia taarifa kwa umma aliyoitoa jana, Desemba 5, 2023, Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi ameainisha mipango inayotekelezwa na Serikali ili kuwasaidia waathirika wa maafa yao.

Matinyi amesema kuna kambi tatu zimewekwa katika shule tatu na wamekuwa wakipatiwa chakula, matibabu na malazi.

Serikali pia imegharimia mazishi ya watu wote waliopoteza maisha na kutoa matibabu bure kwa waathirika wote.

Mbali na hayo, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limetuma salamu za pole kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Taifa kwa ujumla kutokana na maporomoko yaliyotokea wilayani Hanang mkoani Manyara.

TEC pia imeipongeza Serikali kwa hatua ilizochukua haraka baada ya maporomoko hayo.

Akizungumza leo Desemba 6, 2023 jijini hapa, Rais wa TEC na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mbeya, Gervas Nyaisonga amesema wamepokea kwa masikitiko taarifa ya maporomoko hayo yaliyosababisha madhara makubwa.

Askofu Nyaisonga amesema Baraza hilo kupitia kitengo cha maafa linaendelea kuratibu mipango ya kuwasilisha msaada wa vitu mbalimbali kwa walioathiriwa.

"Tunajua mbali na kupoteza Watanzania wenzetu, hata mali zimepotea, hivyo TEC kupitia kamati ya maafa tunaendelea kuratibu msaada kwa ajili ya waathirika. Niwaombe wananchi kuchukua tahadhari katika maeneo yao na hili tulipokee kwa imani kwani Mungu bado anatupenda," amesema.


Imeandikwa na Joseph Lyimo, Mohamed Hamad, Thomas Ng'itu na Saddam Sadick.