Mwarobaini kukabili moshi wa magari barabarani wapatikana

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka nchini Uganda, Dk Monica Musenero akiwa kwenye moja ya mabasi yalizinduliwa leo katika mkutano wa Jukwaa la Kibisahara baina ya Tanzania na Uganda.

Muktasari:

  • Uzinduzi wa mabasi yanayotumia umeme na gesi  unakusudia kuongeza mapinduzi ya usafirishaji Afrika Mashariki

Dar es Salaam.  Katika kukabiliana na uchafuzi wa mazingira unaotokana na moshi wa magari yanayotumia mafuta, mabasi ya umeme na gesi yamezinduliwa ili kuepuka changamoto hiyo.

Mabasi hayo yamezinduliwa leo Ijumaa Mei 24, 2024 katika Jukwaa la Kibiashara baina ya Tanzania na Uganda, linalofanyika jijini Dar es Salaam huku likishirikisha kampuni mbalimbali, mashirika ya uuma, wawekezaji na sekta binafsi.

Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Kiira Motors Corporation (KMC) iliyozindua mabasi hayo, Paul Musasizi amesema mabasi hayo aina ya Kayoola na EVs Model 2024  yanayotumia umeme na gesi, yana uwezo wa kubeba idadi tofauti ya abiria kulingana ukubwa.

“Uzinduzi huu unakusudia kuongeza mapinduzi ya usafirishaji Afrika Mashariki kwa kuwa KMC inalenga kuimarisha ushirikiano endelevu wa mazingira na kuchochea ukuaji wa uchumi katika ukanda,” amesema Musasizi kutoka Uganda.

Amesema kampuni hiyo inakusudia kuongeza maendeleo kwa kupanua soko lake kufika ndani ya Afrika Mashariki na nje.

Musasizi  amesema mabasi yanayotumia gesi makubwa yana uwezo wa kubeba abiria 120 na madogo yanabeba abiria 83 na  yakijazwa vizuri gesi yanasafiri umbali wa kilomita  200-300.

Kwa upande wa mabasi ya umeme ya Kayoola yanabeba abiria 39 kwa mabasi madogo na abiria 63 kwa mabasi makubwa, lakini yakijaa chaji vizuri yana uwezo wa kusafiri kwa umbali wa kilomita 500.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka nchini Uganda, Dk Monica Musenero amesema  kongamano la kibiashara baina ya Uganda na Tanzania linatoa  fursa ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara baina ya nchi hizo mbili.


“Ni matarajio yetu kukuza na kuendeleza kazi za pamoja baina ya mataifa yetu, Jumuiya ya Afrika Mashariki na Afrika kwa jumla,” amesema Dk Musenero.

Pia, amesema Tanzania ni uthibitisho wa soko muhimu kwa magari ya KMC kutokana na uboreshaji mkubwa wa mfumo wa usafiri wa umma hasa kupitia Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart).

Dk Musenero  amesema kaulimbiu ya jukwaa hilo la kibiashara kwa mwaka huu ni:  “Kuimarisha Ubia kwa Manufaa ya Pande zote Mbili."

Hata hivyo, jitihada kubwa ya ujenzi wa miundombinu inayofanywa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) inalenga kuimarisha usafirishaji wa umma kwa kutumia mtandao wa barabara za mabasi, vituo na vituo vikuu.

Kwa mujibu wa Programu ya Tathmini ya Barabara ya Kimataifa (IRAP), mfumo wa Dart, uliyoanza awamu yake ya kwanza mwaka 2016 ukiwa na mabasi 29 tu na vituo vikuu vitano tu, umeleta matokeo makubwa na haraka.

Pia, umeweza kupunguza umbali wa kilomita 20 kutoka saa tatu hadi dakika 45, hivyo kuondoa kutegemea magari binafsi, kupunguza moshi na kutoa ufumbuzi wa safari salama na gharama nafuu kwa wakazi wa Dar es Salaam.