Mwasisi wa Chadema afariki dunia

Sylvester Masinde enzi za uhai wake.

Muktasari:

  • Mmoja wa waasisi wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Sylvester Masinde amefariki dunia leo, Machi 15, 2023.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamizi ya Chadema, Sylvester Masinde amefariki dunia katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza alikokuwa anapatiwa matibabu.

 Taarifa ya tanzia iliyotolewa leo Machi 15, 2023 na Chadema na kusainiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mrema imeeleza Masinde amefariki dunia leo saa 11:25.

“Tunatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, wajumbe wa bodi ya udhamini, marafiki, viongozi na wanachama wa Chadema kwa msiba huu,” imeeleza taarifa hiyo.

Hata hivyo, taarifa hiyo imesema taratibu zaidi zitaelezwa baada ya kikao cha familia.

Masinde alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini hiyo, Novemba 19, 2021 akichukua nafasi ya Arcado Ntagazwa ambaye pia alifariki.

Masinde ni miongoni mwa waasisi wa Chadema ambao bado walikuwepo ndani ya chama hicho.