Mwelekeo mpya huduma za WhatsApp

Muktasari:

  • Kampuni ya Meta inayomiliki pia majukwaa ya Facebook, Instagram, imeweka wazi mwelekeo wa maboresho matatu katika jukwaa la WhatsApp ikiwa ni sehemu ya utamaduni wake wa kuhuisha na kuanzisha huduma mpya ikiwamo kutazama video, kusikiliza muziki wakati wa mawasiliano.

Dar es Salaam.  Wewe ni mtumiaji wa programu tumizi ya WhatsApp? Unazingatia matangazo na maelekezo unayotakiwa kuzingatia kwenye huduma hiyo?

 Kwa mwaka 2024, Kampuni ya Meta inayomiliki pia majukwaa ya Facebook, Instagram, imeweka wazi mwelekeo wa maboresho katika jukwaa la WhatsApp ikiwa ni sehemu ya utamaduni wake wa kuhuisha na kuanzisha huduma mpya. 

Kwa sasa programu za Meta zinaruhusu majukwaa yake kuingiliana taarifa. Mfano, taarifa ulioshirikisha Instagram na Facebook ikaonekana Thread au Instagram ikaingia jukwaa la Facebook.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Jarida la Forbes, Meta imefikiria mabadiliko ya kuweka uhuru wa kuchagua kuunganisha taarifa zako na majukwaa yake mengine katika mfumo huo mpya.

Pili, WhatsApp iko kwenye maandalizi ya huduma ya kusikiliza muziki wakati unawasiliana kwa njia ya video na unaweza kumshirikisha rafiki kutazama pamoja video kwa njia ya WhatsApp kupitia link. Kwa sasa huduma hiyo inapatikana katika mfumo wa Android, toleo la WhatsApp 2.23.26.18.

Tatu, ni kuwezesha mtumiaji kuwa na akaunti katika jukwaa la WhatsApp (username). Kila jukwaa la mtandaoni lina akaunti ya kuingia kabla ya kuanza kuwasiliana ikiwamo mtandao wa X, Instagram na Facebook.

Pia huwezi kuanza kuchati katika jukwaa la mshindani wake Telegram bila akaunti. Kutokana na hitaji hilo kwa watumiaji wake, Meta inakusudia kuanzisha huduma hiyo mwaka huu 2024.