Mwelekeo wa uamuzi kesi ya kina Mbowe kesho

Muktasari:

Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu kesho inatarajiwa kuendelea kuunguruma huku mahakama ikitarajiwa kutoa uamuzi katika sehemu ya kwanza ya pingamizi la mshtakiwa mwenza na Mbowe.

Dar es Salaam. Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu kesho inatarajiwa kuendelea kuunguruma huku mahakama ikitarajiwa kutoa uamuzi katika sehemu ya kwanza ya pingamizi la mshtakiwa mwenza na Mbowe.

Mbowe na wenzake hao, Halfan Bwire Hassa, Adamu Hassan Kasekwa na Mohamed Abdillahi Ling’wenya wanakabiliwa na kesi hiyo Mahakama Kuu Devisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, wakituhumiwa kwa makosa ya ugaidi, inayosikilizwa na Jaji Joachim Tiganga.

Kesho mahakama hiyo inatarajiwa kutoa uamuzi katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi, inayohusu maelezo yanayodaiwa kuwa ya mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo, Mohamed Abdillah Ling’wenya, kufuatia pingamizi lililowekwa na mawakili wa mshtakiwa huyo, Fredrick Kihwelo na Dickson Matata.

Upande wa mashtaka unadai kuwa aliyatoa kwa hiyari yake Agosti 7, 2020, wakati akihojiwa na ofisa wa Polisi Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam, alikofikishwa yeye na mwenzake mshtakiwa wa pili Adamu Hassan Kasekwa, baada ya kutiwa mbaroni mjini Moshi kwa tuhuma hizo.

Hivyo upande wa mashtaka kupitia kwa shahidi wa nane, Mkuu wa Upelelezi Wilaya (OC-CID) ya Arumeru, Mrakibu wa Polisi (SP), Jumanne Malangahe, Novemba 9 mwaka huu uliomba mahakama iyapokee maelezo hayo kuwa kielelezo cha ushahidi wake.

Hata hivyo mawakili hao wa mshtakiwa huyo walipinga kupokewa maelezo hayo akitoa hoja mbalimbali huku akiungwa mkono na mawakili wengine wa utetezi.

Pamoja na mambo mengine mawakili wa utetezi lilipinga kupokewa maelezo hayo kwa madai kuwa mshtakiwa huyo hakutoa maelezo kituoni hapo, kwa kuwa hajawahi kufikishwa kituoni hapo na kwamba hakuwahi kutoa maelezo yake popote.

Badala yake wanadai kuwa maelezo hayo alipewa tu asaini yakiwa yameshaandaliwa, akiwa katika kituo cha Polisi Mbweni bila kupewa haki ya kuyasoma, huku akitishiwa na kuwa asiposaini mateso aliyoyapata akiwa Moshi alikokamatiwa na mwenzake kwa tuhuma hizo yataendelea.

Kutokana na pingamizi hilo mahakama ikalazimika kusimamisha kesi ya msingi na kuendesha kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi ili kujiridhisha kama mshtakiwa alitoa maelezo hayo na kama taratibu za kisheria zilizingatiwa, ambapo pande zote ziiita mashahidi.

Baada ya mahakama kusikiliza ushahidi wa pande zote leo inatoa uamuzi kuhusiana na hoja hizo za pingamizim la mawakili wa utetezi zilizoibuliwa chini ya Sheria ya Ushahidi.

Hata hivyo uamuzi wa kesho utaweza kuhitimisha pingamizi la kupokewa kwa maelezo hayo au kuelekeza kufua milango ya kuingia katika sehemu ya pili ya pingamizi hilo, kutegemeana na jinsi itakavyoamua hoja zilizojadiliwa katika kesi hiyo ndogo.

Kama mahakama itakubaliana na hoja hizo pingamizi za upande wa utetezi, basi pinamizi kuhusu kupokelewa maelezo hayo litaishia hapo maana mahakama itatoa amri ya kukataliwa kupokewa maelezo hayo.

Lakini kama mahakama itatupilia mbali hoja za pingamizi za kesho na kukubaliana na usahidi wa upande wa mashtaka, haitatoa amri yoyote ya kuyapokea maelezo hayo.

Hii ni kwa sababu mbali na hoja hizo za pingamizi la kupokewa maelezo hayo zilizoibua kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi (ambazo zilihitaji ushahidi) bado kuna hoja nyingine za pingamizi la kupokewa maelezo hayo zilizoibuliwa na mawakili wa utetezi.

Hivyo kama mahakama kesho itatupilia mbali  hoja hizo za pingamizi zilizojadiliwa katika kesi ndogo, basi uamuzi huo utafungua milango sasa kujadili sehemu ya pili ya pingamizi la upande wa utetezi kuhusiana na kupokewea maelezo hayo.

Hizi ni hoja ambazo zinahusu kutokukidhi matakwa ya Sheria ya Mwenendo wa Jinai (CPA), katika upatikanaji wa hayo yanayodaiwa kuwa maelezo ya mshtakiwa huyo wa tatu.

Tofauti na hoja hizo zitakazoamuriwa kesho, ambazo zilihitaji ushahidi, katika hatua hii sasa itakuwa ni mchuano wa mawakili pekee kuwasilisha hoja zao kwa misingi ya kisheria kuonesha kuzingatia au kutokuzingatiwa kwa sheria ya hiyo ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Baada ya mawakili wa pande zote kuwasilisha hoja zao, kisha mahakama itaandika uamuzi ambao huo ndio utakaoamua kama maelezo hayo yanapokewe au yanakataliwa.


Katika kesi hiyo ya msingi namba 16 ya mwaka 2021, Mbowe na wenzake hao, ambao waliachishwa kazi Jeshi la Wananchi (JWTZ) Kikosi cha Makomandoo, kwa sababu za kinidhamu, wanakabiliwa na jumla ya mashtaka sita.

Mashtaka mawili ya kula njama kutenda vitendo vya kigaidi vinavyodaiwa kutishia amani na usalama wa wananchi kwa lengo la kusababisha hofu kwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, (washtakiwa wote).

Vitendo hivyo ni kulipua vituo vya mafuta na maeneo ya mikusanyiko mikubwa ya watu, Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Kilimanjaro; kumdhuru aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya; maandamano yasiyokoma na kuzuia barabara kwa miti na magogo. 

Mengine ni kushiriki vikao vya vitendo vya kigaidi (washtakiwa wote), kufadhili vitendo vya kigaidi (Mbowe); kukutwa na mali za kutekelezea vitendo vya ugaidi yaani silaha yaani bastola(Kasemwa) na sare na vifaa vingine vya Jeshi la Wananchi (JWTZ) kwa Halfani.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Agosti Mosi na Agosti 5, 2020 katika Hotel ya Aishi wilayani Hai mkoani Kilimanjaro na katika maeneo mbalimbali katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Arusha.


NB:  Hizi ndizo hoja za sehemu ya pili ya pingamizi hilo ambazo zinasubiri kusikilizwa leo iwapo mahakama itatupilia mbali hoja zitakazoamuriwa leo

1: Maelezo hayo yamerekodiwa chini ya sheria isiyokuwepo yaani marekebisho ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), ya mwaka 2018.

2: Mshtakiwa alionywa chini ya sheria isiyo sahihi yaani Sheria hiyo ya mwenendo wa Jinai, Marejeo ya mwaka 2018 na pia Sheria ya Kupambana na Ugaidi (combating terrorism) badala ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi (Prevetion of terrorism).

3: Hakuna onyo kwa kuwa kifungu cha 24 cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi kilichotumika kumuonya, kutokana na kutokuwepo kwa kifungu kidogo cha (2), kunamanya mshtakiwa asijue kuwa anaonywa kwa kosa la kutenda vitendo vya kigaidi wapi (Nje au ndani ya nchi)

4: Nyaraka hiyo (inayodaiwa kuwa maelezo ya mshtakiwa)   haijakidhi vigezo vya kuwa maelezo ya onyo, kwa kuwa anayeonywa anapoanza kukiri anatakiwa apewe onyo la pekee kwa kumpeleka mbele ya Mlinzi wa Amani (hakimu yeyote wa Mahakama ya Mwanzo)