Yaliyojiri siku 93 kesi ya kina Mbowe

Muktasari:

Kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu inatikisa kwa sasa ndani na nje ya Tanzania.

Dar es Salaam. Kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu imekuwa ikifuatiliwa na watu wengi.

Leo tunakuletea baadhi ya yaliyojiri katika mwenendo wa kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Joachim Tiganga katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Washtakiwa

Katika kesi hiyo kuna washtakiwa wanne, Halfan Hassan,  Adamu  Kasekwa maarufu Adamoo, Mohamed Ling’wenya na Mbowe.

Bwire, Kasekwa na Ling’wenya ni makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliokuwa katika kikosi cha makomandoo (92 KJ) kilichopo Ngerengere eneo Sangasanga mkoani Morogoro kabla ya kuachishwa kazi kwa nyakati tofauti kwa sababu za kinidhamu.

Hata hivyo Mbowe ndiye anayeibeba na kuipa umaarufu mkubwa kesi hiyo kutokana na nafasi yake kwa kuwa ni mwanasiasa maaurufu, mbunge wa zamani na kiongozi mkuu wa chama cha Chadema.

Kabla ya Mbowe kukamatwa Julai 21, 2021 na kuunganishwa katika kesi hiyo, ilikuwa imefunguliwa dhidi ya washtakiwa wengine tangu Agosti 19, 2020 na haikuwa maarufu.

Lakini tangu alipopandishwa kizimbani Mbowe kwa mara ya kwanza Julai 26, 2021 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi  Kisutu na kuunganishwa na washtakiwa hao kwa kusomewa mashataka ya ugaidi, kesi hiyo ilipata umaarufu sana na kuanza kufuatiliwa hatua kwa hatua na watu mbalimbali.

Kesi na aina ya mashtaka

Hii ni kesi ya uhujumu uchumi ambayo si mpya nchini maana kumekuwa na kesi nyingi za namna hiyo baada ya kutungwa kwa sheria ya uhujumu uchumi.

Hii ni sheria ya mwaka 1985 sura ya 200 kama ambavyo imekuwa ikifanyiwa marejeo mara kwa mara yakiwemo marejeo ya mwisho ya mwaka 2019.

Katike kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 16 ya mwaka 2021, washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa ya vitendo vya ugaidi ambayo kufuatia marekebisho ya sheria ya uhujumu ya mwaka 2016, iliyafanya makosa yaliyopo chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002 kuwa makosa ya uhujumu uchumi.

Ingawa kesi za uhujumu uchumi ni jambo la kawaida kwa kuwa zimekuwepo tangu enzi ya Baba wa Taifa, lakini aina ya mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao yaani ya ugaidi ni mapya licha ya kwamba sheria ya kuzuia makosa hayo imekuwepo tangu mwaka 2002 ilipotungwa.

Mashtaka haya hayajazoeleka au kusikika sana katika masikio ya Watanzania kwa kuwa hii ni kesi ya pili ya mashtaka ya ugaidi, baada ya kesi iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa mkurugenzi wa usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare na Joseph Rwezaura, Machi 18, 2013.

Lwakatare na mwenzake  waliokuwa wakituhumiwa kula njama, kupanga na kushiriki vikao na kufadhili vitendo vya kigaidi yaani kutaka kumteka na kumdhuru kwa sumu aliyekuwa mhariri wa gazeti la Mwananchi, Denis Msacky.

Ingawa baadaye Mahakama Kuu iliwafutia mashtaka ya ugaidi na kuwabakizia shtaka moja la kula njama na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) akafungua maombi ya mapitio Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu lakini baadaye DPP aliamua kuyaondoa maombi hayo na kuachana na Lwakatere.

Hata hivyo kesi hiyo haikuwa na umaarufu wa kutikisa kama hii kina Mbowe ambayo ni kesi ya pili ya mashtaka ya ugaidi kufunguliwa nchini, kwani inafuatiliwa hata na mataifa ya nje, huku mabalozi na wawakilishi wa baadhi ya mataifa ya Ulaya wakifika mahakamani kufuatilia mwenendo wake.

Kutokana na aina hiyo ya mashtaka ya kina Mbowe, kumekuwa na mjadala mkali katika jamii na hasa katika mitandao ya kijamii.

Mashtaka halisi

Washtakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na jumla ya mashtaka sita ambayo ni mawili ya kula njama ili kutenda vitendo vya kigaidi vinavyodaiwa kutishia amani na usalama kwa lengo la kusababisha hofu kwa wananchi wa Tanzania na kushiriki vikao vya kupanga vitendo vya kigaidi ambayo yanawahusu washtakiwa wote.

Mashtaka mengine ni kufadhiri vitendo vya kigaidi (Mbowe pekee yake), kumiliki  mali za kutekelezea vitendo vya ugaidi yaani silaha  aina ya bastola (Kasekwa) na sare na vifaa vingine vya JWTZ (Bwire).

Vitendo hivyo vya kigaidi wanavyotuhumiwa kutaka kuvifanya ni kulipua vituo vya mafuta na katika maeneo ya mikusanyiko mikubwa ya watu na kuhamasisha maandamano yasiyo na kikomo katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Morogoro.

Vingine ni kukata miti na kuzuia barabara na kutaka kumdhuru aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro,  Lengai Ole Sabaya.

Kwa pamoja wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Agosti Mosi na Agosti 5, 2020 katika Hotel ya Aishi wilayani Hai mkoani Kilimanjaro na katika maeneo mbalimbali katika mikoa ya Dar es  Salaam, Morogoro na Arusha.

Mwenendo wa kesi

Ni siku 93 tangu kesi kesi hiyo ilipoanza kusikilizwa na siku ya mwisho kusikilizwa mahakamani iliahirishwa hadi Desemba 14, 2021 kwa ajili ya uamuzi wa kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi inayohusu maelezo yanayobishaniwa yanayodaiwa kuwa ylitolewa na mshtakiwa wa tatu ambaye ni Ling’wenya.

Mapingamizi

Kesi hiyo imekuwa ikitawaliwa na mapingamizi ya mara kwa mara ambayo yanaibua mvutano au malumbano makali ya hoja za kisheria baina ya pande mbili za mawakili.

Mapingamizi hayo yapo ya aina mbili, kwanza ni mapingamizi ya hoja za kisheria ambapo mawakili wa pande zote wamekuwa wakitoa hoja za kisheria ama kuhoji uhalali au kukidhi matakwa ya kisheria mwenendo wa shauri au kupinga hoja au maombi hasa ya upokeaji vielelezo.

Katika aina hii ya mapingamizi kumekuwa na jumla ya mapingamizi makubwa kumi na moja huku upande wa utetezi ikiongoza kwa kuweka mapingamizi  tisa dhidi ya upande wa mashtaka ambao wenyewe umeshaweka  mapingamizi mawili tu.

Mapingamizi hayo yanajumuisha mamlaka ya mahakama hiyo kusikiliza kesi, kasoro za ufunguaji mashtaka, upokewaji wa vielelezo mbalimbali na uhalali wa shahidi kutoa ushahidi kizimbani.

Hata hivyo kati ya mapingamizi hayo tisa upande wa utetezi umefanikiwa kushinda pingamizi moja tu huku mapingamizi nane yakitupiliwa mbali.

Mapingamizi ya upande wa mashtaka mawili yanahusu nyaraka ambazo mashahidi wa upande wa utetezi katika kesi ndogo inayohusu maelezo yanayobishaniwa kuwa ni ya Ling’wenya, waliomba mahakama izipokee kama vielelezo vya ushahidi.

Katika hayo upande wa mashtaka umeshinda moja dhidi ya barua ambayo mshtakiwa wa tatu aliomba mahakama iipokee ambayo alimwandikia Kamanda wa Polisi Mko wa kipolisi Ilala.

Katika barua hiyo Ling’wenya akiomba nyaraka mbalimbali za kumthibitisha shahidi wa pili wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo ndogo,  Koplo Msemwa kwamba Agosti 2020 alikuwa anafanya kazi kituo kikuu cha Polisi Dar es Salaam lakini mahakama ilikubaliana na pingamizi la upande wa mashtaka ikaikataa.

Pingamizi la upande wa mashtaka lilikuwa dhidi ya nyaraka mbalimbali ambazo shahidi wa pili wa utetezi katika kesi hiyo ndogo, aliiomba mahakama izipokee.

Nyaraka hizo ni pamoja na hati ya mashtaka na mwenendo wa kesi iliyokuwa ikimkabili shahidi.

Nyingine ni barua ya kuomba hati hiyo ya mashtaka na mwenendo wa kesi hiyo aliyomwandikia hakimu mkazi wa mahakama hiyo aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo pamoja na kitabu cha kupokelea barua.

Licha ya upande wa mashtaka kuzipinga zisipokewe lakini mahakama ilitaoa amri ya kuzipokea huku ikitoa fursa kwa upande wa mashtaka kuonyesha kutokustahili kwake wakati wakimhoji shahidi huyo.

Aina nyingine ya mapingamizi ambayo yametawala katika kesi hiyo ni yale yanayohusu utaratibu za kisheria katika uendeshaji wa kesi hiyo  ambayo Jaji amekuwa akiyatolea mwongozo au uamuzi wa papohapo kwa mdomo bila kulazimika kuahirisha kesi kwenda kuandika uamuzi rasmi.

Mapingamizi haya yamekuwa yakitolewa na kila upande dhidi ya upande kinzani.

Haya yamekuwa yanaibuka wakati wakili anamuongoza shahidi wake kutoa ushahidi au wakati wa madodoso, yaani wakili wa upande kinzani anapomhoji shahidi kuhusiana na ushahidi.

Pia mapingamizi hayo yamekuwa yakiibuka wakati wakili anapomuuliza shahidi maswali kwa lengo la kusawazisha hoja zilizotokana na maswali ya wakili wa upande kinzani.

Mawakili hao wamekuwa wakipinga aina ya swali au namna ya uulizaji swali kuwa ni kinyume cha utaratibu.

Mapingamizi ya aina hizo zote yamekuwa yakiwafanya mawakili kulumbana sana na wakati mwingine kuzungumza kwa hisia kali, kabla ya Jaji kuingilia kati ama kwa kutoa mwongozo au uamuzi baada ya kutoa nafasi na kusikiliza hoja za pande zote.

Majaji kujiondoa

Tangu kuanza kwa kesi hiyo tayari imeshapita kwa majaji wawili na sasa ipo kwa jaji wa tatu.

Kesi hiyo ilianzia kwa Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Elinaza Luvanda lakini alijiondoa ndani ya wiki moja tu  yaani Septemba 6 baada ya washtakiwa kumuomba ajiondoe kwa madai ya kutokuwa na Imani naye kuwa angewatendea haki, hasa baada ya kutupilia mbali mapingamizi yao mara mbili.

Kisha alipangiwa aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mustafa Siyani kuanzia Septemba 10, lakini mwezi mmoja na siku 10 baadaye naye alijiondoa kutokana na kile alichoeleza kuwa na majukumu mengi, baada ya kuteuliwa kuwa Jaji Kiongozi. Na sasa kesi hiyo inasikilizwa na Jaji Joachim Tiganga.

Kesi ndani ya kesi

Wakati kesi ya msingi inaendelea kumekuwa kukiibuka kesi nyingine ndogo ndani ya kesi hiyo ya msingi. Mpaka sasa kumeshakuwa na kesi ndogo mbili ambazo zinatokana na washtakiwa kupinga kupokewa kwa maelezo ambayo yamekuwa yakidaiwa na upande wa mashtaka kuwa ni ya washtakiwa hao.

Ilianza kesi ndogo iliyohusu maelezo ya Kasekwa ambayo hata ilipoamuriwa na Jaji Siyani alitupilia mbali pingamizi hilo na kuyapokea maelezo yake na kuwa kielelezo cha ushahidi upande wa mashtaka.

Kesi nyingine ndogo inahusu maelezo ambayo upande wa mashtaka unadai kuwa ni  Ling’wenya, ambayo bado ndio imepangwa kutolewa uamuzi Desemba 14.

Maswali ya mawakili kwa mashahidi

Mahojiano baina ya mawakili na mashahidi wa pande zote yamekuwa ni kivutio kingine katika ufuatiliaji wa mwenendo wa kesi hiyo. Kuna wakati mawakili wakiwabana mashahidi katika kesi ya msingi na katika kesi hizo  ndogo.

Mawakili wamekuwa wakiwabana mashahidi hao kwa maswali kiasi cha kuwaweka wengine katika wakati mgumu kuyajibu na wengine kujibu ndivyo sivyo au kunyamaza kwa kushindwa kujibu baada ya kujikuta wameingia kwenye mtego au kutoa majibu ambayo wasikilizaji hushindwa kujizuia na kulazimika kuangua vicheko.

Baadhi ya mashahidi japo wachache wamekuwa makini na kukabiliana na maswali ya mawakili na kuwakosoa au kuwasahihisha mawakili katika maswali au maelezo yao pale wanapoona kuwa hayako sawa.

Mahojiano hayo ya mawakili wa mashahidi yamekuwa yakiibua gumzo miongoni mwa wadau wanaofuatilia kesi hiyo, japo kwa mitizamo tofauti huku wengine wakiona kuwa shahidi fulani kashindwa kujibu au kajibu vizuri maswali ya wakili fulani.

Kipoza njaa

Kwa kuwa kesi hiyo huchukua muda inapoanza na kwa kuwa katika eneo mahakama hiyo baadhi ya watu wanaofuatilia kesi hiyo na wengi wao wakiwa ni wanachama na wafuasi wa Chadema wameamua kujiandalia chakula chao.

Awali walikuwa wakichangisha fedha  na mmoja au  baadhi yao wanaandaa chakula na kwenda na mihogo au viazi vya kuchemsha kwenye ndoo ya plastiki ambavyo wakati wa mapumziko wanapoza njaa kabla ya kurudi mahakamani kuendelea na usikilizaji wa kesi hiyo.

Hata hivyo baadaye wameanza kupata wafadhili hata ambao hawafiki mahakamni hapo ambao huwachangia fedha au kuwapelekea vinywaji kama maji na wakati mwingine chakula kama wali na hata mayai.

Usajili wa wasikilizaji

Kila msikilizaji anayefika mahakamani hapo hususan wanachama wa Chadema wamekuwa na utaratibu wa kujiorodhesha katika daftari la mahudhurio kila mhusika akitaja jina na mahali anakotokea pamoja na mawasiliano yake.

Hayo ni baadhi ya mambo yaliyojiri kwenye kesi hiyo tangu ilipoanza kuunguruma.