Askari mstaafu JWTZ aliyefutiwa kesi ya kina Mbowe atoa ushahidi

Muktasari:

  • Mmoja wa washtakiwa waliofutiwa mashtaka katika kesi ya uhujumu Uchumi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu amepanda kizimbani kumtetea mahtakiwa wa tatu katika kesi hiyo, Mohamed Abdillahi Ling'wenya.


Dar es Salaam. Mmoja wa washtakiwa waliofutiwa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu amepanda kizimbani kumtetea mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo, Mohamed Abdillahi Ling'wenya.

Mshtakiwa huyo aliyefutiwa mashtaka, Gabriel Mhina (34) amepanda kizimbani katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, kutoa ushahidi akiwa ni shahidi wa tatu wa upande wa utetezi, katika kesi ndogo ndani ya kesi ya ugaidi, inayohusu uhalali wa maelezo yanayodaiwa kuwa ya mshtakiwa wa tatu Ling'wenya.

Mhina ambaye pia ni Askari mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Kikosi maalum (Kikosi cha Makomandoo 92 KJ, Sangasanga, Ngerengere Morogoro) alikuwa ni miongoni mwa washtakiwa katika kesi hiyo ya awali namba 63 ya mwaka 2020 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu.

Hata hivyo yeye na wenzake wawili walifutiwa mashtaka na Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP).

Lakini leo Desemba Mosi, 2020 Mhina ambaye pia mwaka 2014 alikwenda kwenye operesheni ya kutunza amani Sudan, amepanda kizimbani kutoa ushahidi wa utetezi kwa ajili ya Ling'wenya, katika kesi hiyo ndogo.

Mpaka sasa shahidi huyo ambaye kwa sasa ni mkulima mkoani Tabora baada ya kuacha Jeshi kwa tatizo la uwezo wa akili, anaendelea na ushahidi wake.