Mwelekeo mpya kwa uraia pacha

Mweleko mpya kwa uraia pacha

Muktasari:

  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amesema Serikali inalifanyia kazi suala la uraia pacha na kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha, litakuwa limepatiwa ufumbuzi.


Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amesema Serikali inalifanyia kazi suala la uraia pacha na kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha, litakuwa limepatiwa ufumbuzi.

Pia, alisema wizara yake iko tayari kuwawezesha Watanzania waishio nje ya nchi (diaspora) kupiga kura endapo watapata ridhaa kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa sababu ni rahisi kwa kutumia teknolojia.

Balozi Mulamula alisema hayo katika mahojiano maalumu na wahariri wa gazeti hili alipotembelea Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) jijini Dar es Salaam jana kwa lengo la kuimarisha ushirikiano.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita imetambua suala la uraia pacha linakwenda sambamba na ushiriki wa diaspora; na watu wengi, wakiwamo wabunge wamekuwa wakionyesha utayari wao.

“Tukiwa bungeni kuna mbunge mmoja aliondoa shilingi mpaka tumpe majibu, wakati ule zamani tukienda bungeni walikuwa wanasema ‘bwana wee usituambie habari za diaspora, wanakula kuku kwa mrija, wachague wanataka wapi, huwezi kupata huku ukapata kule’. Sasa mtazamo umebadilika, wao ndio wanaotaka,” alisema Balozi Mulamula.

“Wabunge wengi wametoka diaspora, nikawaambia kama mnalitaka hili basi, na ninyi ni watunga sheria, sisi tunalifanyia mkakati wa kisera, lakini likija kwenye sheria ninyi wabunge ndiyo mtusaidie tuipitishe.”

Balozi Mulamula alisema tangu akiwa balozi, msisitizo wake ni kwamba huwezi kumwondolea mtu haki ya kuzaliwa katika nchi aliyozaliwa.

Alisema Watanzania wengi walio nje ya nchi wamekwenda kutafuta maisha na wako kwenye fani tofauti, ukiwamo udaktari na biashara, hivyo, wana mchango mkubwa kwa maendeleo ya Taifa.

“Ningekuwa na uwezo ningelimaliza hata jana, ingekuwa imenipa amani sana, hasa kukuza ushiriki wa diaspora. Mtazamo umebadilika, si kama huko nyuma, kwa hiyo mimi naamini kabla ya mwisho wa mwaka huu, tutakuwa tumelipatia suluhu hili la uraia pacha,” alisema.

Alisema suala la uraia pacha lilitakiwa lipite katika mchakato wa mabadiliko ya katiba, lakini ilionekana si suala la kuingia kwenye katiba, bali kuliwekea sheria maalumu kama zilivyofanya Ethiopia na India.

“Kubadilisha Katiba ni mlolongo mrefu, lakini ikishaingia kwenye katiba halafu ukaja utawala mwingine hauitaki, unaitoaje? Kwa hiyo kukiwa na sheria inawalinda zaidi.

“Sasa tumesema tunavyoainisha hii sera yetu ya mambo ya nje, tuko kwenye mkakati wa kuweza kuja na programu maalumu wanayoita hati maalumu zinazowatambulisha Watanzania walioko nje,” alisema Balozi Mulamula.

Suala la uraia pacha ni miongoni mwa mambo yaliyoibuliwa na wananchi wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba (CRC) inakusanya maoni ambayo yaliwekwa kwenye rasimu ya pili ya Katiba kisha kupitishwa kwenye Katiba inayopendekezwa.

Ibara ya 72 ya Katiba Pendekezwa inasema: “Bila kuathiri masharti yaliyomo kwenye sura hii, mtu yeyote mwenye asili au nasaba ya Tanzania na ambaye ameacha kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano kwa kupata uraia wa nchi nyingine, atakapokuwa katika Jamhuri ya Muungano, atakuwa na hadhi maalumu kama itakavyoainishwa katika sheria za nchi.”


Wadau wazungumza

Akizungumzia suala la diaspora, mbunge wa viti maalumu, Neema Lugangira alisema aliishauri Serikali bungeni kutunga sera maalumu ya diaspora itakayoondoa changamoto zinazowakabili kama kutoruhusiwa kumiliki ardhi na kurithi mali.

Hata hivyo, alisema suala la uraia pacha lina changamoto, hivyo, alipendekeza Serikali kuja na jambo la haraka la kuwapa hadhi maalumu diaspora kama ambavyo India wamefanya kupitia hati maalumu za diaspora zinazojulikana kama People of India Origin (PIO).

“Kwa kuwa jambo la uraia pacha lina changamoto zake, nilipendekeza tuje na utaratibu wa kuwapa hadhi maalumu, lakini ili liwezekane lazima tuwe na sera ya diaspora,” alisema mbunge huyo anayewakilisha Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGOs).

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema nchi zilizoruhusu uraia pacha duniani kote zimepiga hatua kiuchumi kwa sababu zimewajengea diaspora kujiamini na kupata haki kama raia wa nchi zao.

Mbatia alitolea mfano Kenya akisema mwaka jana fedha zilizotoka kwa diaspora kwenda Kenya zilikuwa ni Dola 4.4 bilioni za Marekani ukilinganisha na Dola 380 milioni ambazo diaspora walirudisha hapa Tanzania.

“Ili kujenga confidence ya diaspora, uraia pacha ni muhimu. Kutojiamini ndiyo sababu ya kuwekea vikwazo suala hili, tuangalie mizania ya kiuchumi zaidi ili tufanye maamuzi sahihi,” alisema Mbatia.

Diaspora kupiga kura

Balozi Mulamula alisema suala la diaspora kupiga kura linahitaji utaratibu na miundombinu, hasa kwa kutumia teknolojia kama zinavyofanya nchi nyingine zilizofanikiwa kwa kutumia mifumo ya kimtandao.