Mwili wa Milembe wa GGM kuzikwa leo

Muktasari:

  • Mwili wa mfanyakazi wa Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Dhahabu Geita (GGML), Milembe Suleman (43) aliyeuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali na watu wasiojulikana, unatarajiwa kuzikwa leo nyumbani kwao Kijiji cha Kilombero wilayani Geita.

Geita. Mwili wa mfanyakazi wa Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Dhahabu Geita (GGML), Milembe Suleman (43) aliyeuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali na watu wasiojulikana, unatarajiwa kuzikwa leo nyumbani kwao Kijiji cha Kilombero wilayani Geita.

Jana, mwili huo wa Milembe (pichani), aliyeuawa juzi ulitolewa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Mkoa wa Geita na kupelekwa nyumbani kwa dada yake Mtaa wa Mseto.

Mwili huo uliagwa na watu wachache, akiwamo mtoto wake kabla ya kuanza safari ya kuelekea jijini Mwanza alikokuwa akiishi.

Dada wa familia, Paulina Seleman alisema wamelazimika kuupeleka mwili wa Milembe nyumbani kwake Mwanza maeneo ya Usagara ambako majirani na marafiki wataungana kutoa heshima za mwisho kisha utarudishwa Geita leo mchana kwa ajili ya kuagwa na wafanyakazi na marafiki.

Alisema baada ya watu kuaga mwili huo utasafirishwa hadi Kijiji cha Kilombero kwa ajili ya maziko yatakayofanyika kesho.

Akimzungumzia marehemu, Paulina alisema ni mtoto wa nne kuzaliwa kati ya watano wa familia na ameacha mtoto mmoja.

Alisema awali alikuwa akiishi naye hadi mwaka 2003 alipoanza kujitegemea na baadaye kujenga nyumba yake maeneo ya Nyamalembo.

“Aliolewa na baba mmoja wa Kinyarwanda, lakini kutokana na vipigo waliachana, baadaye aliolewa na mwanamume mwingine akazaa naye mtoto mmoja ambaye anasoma kidato cha tano, lakini waliachana (na mumewe) na yeye akaendelea na maisha yake,” alisimulia Paulina.

Alisema mdogo wake huyo alikuwa mtu anayesaidia familia yao na watu wengine bila shida na kifo chake kimeacha pengo kubwa kwao.


Viongozi wa dini

Mchungaji wa Kanisa la AICT Geita, John Masanyiwa alisema matukio ya ukatili hasa ya kukata mapanga wanawake mkoani Geita yanaleta hofu kwa jamii.

“Huyu ameuawa ni mwanamke wa tatu kuuawa kikatili ndani ya wiki moja, huu ni ukatili, nasema ni ukatili kwa sababu hata kama kulikuwa na changamoto wangefika kwenye vyombo vya sheria ili haki itendeke,” alisema Masanyiwa.

Aliitaka jamii kuacha visasi kwa kuwa hakuna changamoto isiyo na majibu na kuitaka iwe inafikia maridhiano badala ya kulipa kisasi.

Alisema watu wanapaswa kumjua Mungu kwa kuwa itawawezesha kuishi kwa misingi ya kumpendeza na kuwa na maadili sambamba na kujua thamani ya mtu.

“Kama mwanadamu akiishi kwa kumjua Mungu ukatili huu hatutauona, hatuwezi kuzuia kifo, lakini mambo ya ukatili hayatakuwepo na mtu atakufa kwa kusudio la Mungu na sio kufanyiwa ukatili wa aina hii,” alisema mchungaji Masanyiwa.

Alisema watu wakimkataa Mungu naye huwaacha na mwisho huishi maisha ambayo hayampendezi mwanadamu wala Mungu.

Pia, aliwataka wananchi wenye taarifa za ukatili kutoa taarifa kwenye vyombo vya usalama ili kuisaidia Serikali kudhibiti matukio hayo yanayotia doa Geita.

Sheikh wa Mkoa wa Geita, Yusuph Kabaju alisema watu kutokuwa na hofu ya Mungu ni moja ya sababu zinazochangia kufanyiana ukatili.

“Viongozi wa dini tunazungumza mara kwa mara, mikoa hii ya kanda ya ziwa kuna waganga wengi wa kienyeji na hawa wanachangia kuleta mambo haya, hasa kwenye kanda hii ambayo inaamini sana waganga,” alisema Sheikh Kabaju.

Akizungumzia malalamiko yaliyotolewa dhidi ya waganga wa kienyeji wanaodaiwa kuchangia mauaji kwa kupiga ramli chonganishi, Mwenyekiti wa Waganga Mkoa wa Geita, Bujukano John alikana waganga kuchangia mauaji hayo akisema zamani walishirikiana na Serikali kuzuia ramli chonganishi, lakini sasa wameachwa kando na Serikali imekuwa ikikutana na wazee na viongozi wa dini pekee.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juzi, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Berthaneema Mlay alisema Milembe aliuawa kwa kukatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake na watu wasiojulikana.

Alisema polisi walipofika walikuta mwili wake ukiwa umekatwa maeneo mbalimbali ikiwamo kichwani, usoni na mikononi huku kiganja kimoja cha mkono kikiwa kimeondolewa.

“Kwa mujibu wa polisi waliofika kwenye tukio, alikuwa amekatwa sehemu za kichwani, usoni na kwenye mikono yote miwili na mkono wa kulia kiganja kiliondolewa kabisa, hayo ndio maeneo yaliyojeruhika zaidi,” alisema Kamanda Mlay.

Kufuatia tukio hilo, watu wanne wanashikiliwa kwa uchunguzi.