Nzengo yamlilia mfanyakazi Mgodi wa Geita

Jeneza likiwa na mwili wa aliyekuwa mfanyakazi wa kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu (GGML), Milembe Seleman likiwa nyumbani kwake Kitongoji cha Nyashimbe Kata ya Usagara Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza. Picha na mpiga picha wetu. 

Muktasari:

Aprili 26, 2023 Jeshi la Polisi mkoani Geita lilitoa taarifa ya Milembe Seleman aliyekuwa mfanyakazi wa kitengo cha Ugavi katika kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu (GGML) kuuawa kwa kukatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake na watu wasiojulikana.

Mwanza. Uongozi wa Kitongoji cha Nyashimbe Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza alipokuwa akiishi Milembe Suleman (41) aliyefariki kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali na watu wasiojulikana umesema, kitongoji hicho kitamkumbuka kutokana na michango yake ya kimaendeleo kwenye nzengo.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Aprili 28, 2023 nyumbani kwa Milembe eneo la Nyashimbe Kata ya Usagara wilayani humo, Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Dotto Gabriel amesema marehemu alikuwa akishiriki vizuri shuguli za maendeleo katika kitongoji hicho.

“Michango mbalimbali ya maendeleo, aliwahi kuchangia barabara iliyokatika hapa tulishirikina naye kuweka mulamu na mawe ambapo alitumia gharama zake Sh400,000. Milembe alikuwa hana shida yoyote na jamii ya hapa hata mimi kiongozi nilikuwa nashirikiana naye vizuri tu,”amesema Gabriel

Shemeji wa Milembe, Sospeter Mkakalo amesema familia imepata pigo kuondokewa na mpendwa wao akidai alikuwa tegemeo lao.

“Baada ya kupata taarifa za tukio (za kuawa) tulishtuka sababu hatukutegemea kwamba hili tukio litakuwa hivi na hatukuamini hadi tulipoona mwili wake.

“Katika familia alikuwa ni mtu anayejitoa sana, alikuwa na mchango mkubwa sana kwa ndugu, kwa jamaa, alijitoa kusaidia jamii, kusaidia familia kwahiyo tumempoteza mtu ambaye wa muhimu sana katiak familia,”amesema

Amesema Milembe aliolewa na kubahatika kupata mtoto mmoja wa kike lakini baadaye alitengana na mumewake.

Hatahivyo wakati waandishi wa habari wakiendelea na mahojiano, Kaka wa marehemu aliwafukuza na kumtaka mlinzi aliyekuwa akilinda eneo la nyumba hiyo kuhakikisha hawaingii ndani ya geti na kushiriki ibada ya mazishi iliyokuwa ikifanyika nyumbani kwa Milembe.

Mwili wa Milembe ulifika jana Aprili 27, 2023 nyumbani kwake Kata ya Usagara ili majirani na marafiki kutoa heshima za mwisho kisha kurudishwa Geita mchana ambapo utapumzishwa kwenye nyumba yake ya milele katika kijiji cha Kilombero Jumamosi  Aprili 29, 2023.