Mwili wa Mngereza kuletwa Dar kwa ndege

Mwili wa Mngereza kuletwa Dar kwa ndege

Muktasari:

Uongozi wa hospitali ya rufaa  Mkoa wa Dodoma umesema mwili wa katibu mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata),  Geofrey Mngereza unatarajia kusafirishwa wakati wowote kwa ndege kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam.

Dodoma. Uongozi wa hospitali ya rufaa  Mkoa wa Dodoma umesema mwili wa katibu mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata),  Geofrey Mngereza unatarajia kusafirishwa wakati wowote kwa ndege kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam.

Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo,   Dk Ernest Ibenzi amesema  kiongozi huyo alifikishwa hospitalini hapo Jumatatu Desemba 21, 2020 akiwa amezidiwa.

“Tulimpokea siku hiyo na kumpeleka moja kwa moja chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu (ICU) na tangu wakati huo hakuweza kupata nafuu na mauti ilimkuta akiwa bado chumba hicho,” amesema Dk Ibenzi.

Mganga huyo amesema madaktari walijitahidi kufanya kila namna ya kuokoa uhai wake  lakini mapenzi ya Mungu yalikuwa juu ya uwezo wao.

Taarifa za kifo cha Mngereza zilisambaa katika mitandao ya kijamii zikieleza kuwa alifariki usiku wa kuamkia Krismasi akiwa jijini Dodoma na haikuelezwa kama alikuja kikazi au kwa shughuli binafsi.

Mngereza atakumbukwa kwa misimamo yake hasa kwa wasanii waliokuwa na nyimbo zilizodaiwa kuwa na maudhui yasiyofaa.