Ujumbe wa mwisho wa Mungereza kwa msemaji wa Serikali ya Tanzania

Ujumbe wa mwisho wa Mungereza kwa msemaji wa Serikali ya Tanzania

Muktasari:

Msemaji wa Serikali ya Tanzania ambaye pia ni katibu mkuu wa wizara ya Habari,  Dk Hassan Abbas ameandika ujumbe wa mwisho alioupokea kutoka kwa aliyekuwa  katibu wa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA), Godfrey Mungereza aliyefariki dunia jana usiku Alhamisi Desemba 24,  2020 mjini Dodoma.

Dar es Salaam. Msemaji wa Serikali ya Tanzania ambaye pia ni katibu mkuu wa wizara ya Habari,  Dk Hassan Abbas ameandika ujumbe wa mwisho alioupokea kutoka kwa aliyekuwa  katibu wa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA), Godfrey Mungereza aliyefariki dunia jana usiku Alhamisi Desemba 24,  2020 mjini Dodoma.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa  Instagram, Dk Abbas ameandika ujumbe huo, "nimelazwa General (hospitali ya Mkoa wa Dodoma) hapa Dom ila kila kitu kitaenda sawa kuhusu tamasha. Napambana."
Dk Abbas ameeleza kuwa ni  ujumbe wa mwisho alioupokea Jumanne saa tano usiku.

Hakika ni majonzi,  baadhi ya wasanii wamemlilia katibu huyo wa Basata  kupitia kurasa za  mitandao yao ya kijamii.

Msanii  Diamond Platnumz aliandika,  “Dah nakosa  hata cha kuandika.... mkuu si juzi tu tulikuwa Arusha ulikuja kutuunga mkono kwenye tour yetu ya tumewasha na Tigo, leo hii umetangulia....Dah! Inshaallah mwenyezi Mungu akulaze mahali pema peponi Amin.”

Mbunge wa Muheza (CCM)  ambaye pia ni msanii wa muziki wa kizazi kipya,  Mwana FA ameandika,  “nakosa la kusema ndugu yangu Mngereza.Mbele yako nyuma yetu mzee wangu. Ukapumzike kwa amani."

Msanii Barnaba ameandika,  “mzee wangu Mwengeleza nakuita Doh.  Hili ni pigo kwa tasnia aisee. Nashindwa kupokea hakika nakosa kabisa nguvu pole familia nzima na @basata.tanzania  Mungu akufanye mwenye tabasam daimamilele.”

"Wasanii hili ni pigo mzee wetu alikuwa zaidi ya kiongozi! Hapana aisee Mungu tunakushukuru Kwa kila jambo wewe ndo unayejua kila ukubwa wa jambo."

“Babu yangu jamani nimeumia nimeshtuka kwanini jamani.  Mshauri wangu mshauri wa wasaniii wote jamani. Mipangooo yote ileee jamaaan nenda baba nenda kipenzi, " ameandika msanii Nandy.


Naye Kala Jeremiah ameandika,  "pumzika kwa amani kiongozi wangu.  Mungu ailaze roho yako mahala pema peponi twaomba."