TIA kuwaombea wanafunzi wake mikopo asilimia 10

Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Profesa William Pallangyo, akizungumza na watendaji wa taasisi yake alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba).
Muktasari:
- Mikopo hiyo inayotolewa na halmashauri nchini inalenga kuinua makundi ya vijana, wazee na wenye ulemavu, na sasa inasimamiwa na benki.
Dar es Salaam. Wakati mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu ikianza kutolewa kupitia benki, Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA) kimesema kipo katika mazungumzo na mamlaka za Serikali za mitaa ili wanafunzi wake waweze kukopeshwa.
Hiyo ni baada ya chuo hicho kuwa tayari kubeba dhamana ya wanafunzi watakaokuwa wanakopa, kikilenga kuwawezesha kiuchumi na kuziba pengo kati ya mafunzo ya kitaaluma na mahitaji halisi ya soko la ajira.
Mkuu wa Mpango wa Maendeleo ya Kazi kutoka TIA, Imani Matonya, ameeleza hay oleo, Julai 3, 2025 alipozungumza na Mwananchi katika Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, maarufu Sabasaba, yanayoendelea jijini hapa.
Matonya amesema mfumo wa sasa wa mikopo kwa vijana unawasaidia kulingana na kata wanazotokea, wakati wanafunzi wa vyuo kama TIA wanatoka maeneo mbalimbali nchini, hali inayowanyima fursa ya kupata msaada huo wa kifedha.
“Tunapendekeza Serikali itambue taasisi za elimu kama kata huru, ili mikopo hiyo itolewe kwa kutumia dhamana za kitaasisi. Hii itawawezesha wanafunzi kuomba na kupata mikopo wakiwa vyuoni, huku taasisi ikiwa kama mdhamini wao,” amesema.
Matonya amesema mbinu hiyo inalenga kuwasaidia wanafunzi kupata mikopo ya asilimia 10 ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ili waanzishe biashara au kuendeleza ubunifu wao wakiwa bado masomoni.
“Kwa kufanya hivi, TIA inatarajia kupunguza ukosefu wa ajira kwa vijana na kukuza utamaduni wa ujasiriamali kwa wahitimu,” amesema.
Hili linafanyika wakati ambao TIA pia inaboresha maandalizi ya kitaaluma kwa wanafunzi ili kuwafanya wawe tayari kwa soko la ajira.
Matonya ameeleza kuwa chuo hicho kinaoanisha mafunzo yake na mahitaji ya soko kwa kutoa elimu ya vitendo inayozingatia mifumo ya kisasa na kuwaunganisha wanafunzi moja kwa moja na wataalamu wa sekta mbalimbali.
TIA pia imeingia ubia na mashirika mbalimbali kama Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (Sido), Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) kusaidia wanafunzi kuelewa taratibu za usajili wa biashara, uvumbuzi, pamoja na uzingatiaji wa masuala ya kodi na sheria.
“Hatuwapi tu maarifa, tunawaunganisha na zana halisi na mitandao ya ulimwengu wa kazi,” ameongeza Matonya.
Ubunifu wa wanafunzi pia ni eneo muhimu linalopewa kipaumbele. TIA inatoa msaada kwa kampuni bunifu zilizoanzishwa na wanafunzi, hasa katika sekta za kilimo, ardhi, afya na elimu.
Miongoni mwa miradi hiyo ni Dala Hub, jukwaa la kidijitali linalowaunganisha wapangaji na wamiliki wa nyumba, pamoja na huduma za usafi na mapambo ya ndani.
Katika kilimo, kuna jukwaa jipya linalowawezesha wakulima kutangaza mazao yao moja kwa moja kutoka shambani na kuunganishwa na wanunuzi au vyama vya ushirika papo hapo.
Ubunifu mwingine ni OnlineKimbwete, jukwaa la majadiliano ya mtandaoni linalochochea kujifunza baina ya wanafunzi na kushirikiana na wataalamu.
“Tunataka kuwa zaidi ya chuo, tunataka kuwa injini ya maendeleo kwa vijana,” amesema Matonya.
Mmoja wa waliozungumzia mpango huu, Sadick Manase, ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amesema inaweza kuwa njia nzuri ya vijana kutimiza malengo yao kabla ya kumaliza chuo.
“Hata wale wenye ubunifu wataweza kujiendeleza kwa sababu watakuwa na hela tayari ya kufanya kile walichokianza,” amesema.