Mwili wa mtoto Janeth wapatikana ziwani
Nyachuga John (wa pili kulia), ambaye ni mama mzazi wa marehemu Janeth, akisaidiwa na majirani zake baada ya kuona mwili wa mwanaye ukiopolewa kutoka katika mwalo wa Kirumba Mwanza jana. Marehemu Janeth alifariki Alhamisi wiki iliyopita baada ya kusombwa na mafuriko wakati akitoka shule. Picha na Jesse Mikofu
Muktasari:
Mwili huo ulipatikana katika mwalo wa Kirumba, umbali wa kilomita tano kutoka eneo la Mabatini alikosombwa.
Mwanza. Mwili wa mtoto Janeth James (6) aliyesombwa na mafuriko katika Mto Mirongo, Alhamisi iliyopita ulipatikana jana ukielea juu ya maji ndani ya Ziwa Victoria, eneo la Kirumba jijini hapa.
Mwili huo ulipatikana katika mwalo wa Kirumba, umbali wa kilomita tano kutoka eneo la Mabatini alikosombwa.
Kabla ya mwili huo kupatikana, madaftari ya mtoto huyo yalionekana na baadaye watu waliokuwa kwenye mtumbwi wakiutafuta waliuona ukielea.
Janeth alisombwa na maji Januari 14 saa sita mchana baada ya kumponyoka baba yake, aliyekuwa amekwenda kumfuata shuleni siku ya pili tangu aandikishwe darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Mabatini.
Saa chache baada ya kupata mwili huo, ambao ulitafutwa kwa siku tatu mfululizo, ulizikwa eneo la Kisesa wilayani Magu kutokana na kuharibika kwa kukaa majini muda mrefu.
Baba mzazi wa marehemu, James Joseph alisema: “Namshukuru Mungu mwili wa mwanangu umepatikana ili nimzike kwa heshima zote anazostahili. Ingawa tumepata pigo, lakini tumefarijika kumwona kwa mara ya mwisho kuliko mwili ungepotelea ziwani.”
Kabla ya kuupata mwili wa mtoto huyo, ndugu walilazimika kutekeleza mambo kadhaa ya kimila ambayo wanaamini yalisaidia kuupata.
Wakazi wa Jiji la Mwanza walieleza kuwa, mafuriko hayo yalisababishwa na mvua iliyonyesha kwa zaidi ya saa nne kuanzia saa 4.30 asubuhi hadi saa tisa alasiri na hayajawahi kushuhudiwa zaidi ya miaka minne iliyopita.