Mwili wa mwanafunzi aliyepotea Januari wapatikana

Muktasari:

  • Ikiwa ni takribani siku 250 baada ya kutoweka katika mazingira ya kutatanisha, mabaki ya mwili wa Levis Mwailemele (16), mwanafunzi wa kidato cha nne yamepatikana katika pori la Nkisyo.

  


Mbeya. Ikiwa ni takribani siku 250 baada ya kutoweka katika mazingira ya kutatanisha, mabaki ya mwili wa Levis Mwailemele (16), mwanafunzi wa kidato cha nne yamepatikana katika pori la Nkisyo.

Mwanafunzi huyo wa Shule ya Sekondari Ikuti mkoani Mbeya alipotea Januari 9 mwaka huu na mabaki yake yamepatikana Septemba 18 ikiwa ni siku 252.

Mabaki hayo ni pamoja na fuvu, mifupa na nguo ambazo zimekutwa katika pori hilo.

Baada ya kupatikana kwa mabaki hayo, ndugu wa marehemu walifuata taratibu za kisheria na kuendelea na shughuli za mazishi katika makaburi yaliyopo katika Kijiji cha Lyenje Kata ya Ikuti.

Imeelezwa marehemu alikuwa akiishi na bibi yake na mara ya mwisho alienda kanisani Jumapili na tangu alipotoka majira ya saa 6:00 mchana hakurejea nyumbani.

Akizungumza na gazeti hili, bibi wa marehemu, Queen Asubisye alisema “kama ilivyo kawaida yake, alikuwa anapenda sana kusali alienda kanisani baada ya ibada hakurejea, juhudi za kumtafuta zilishindikana mpaka tulipo ukuta mwili na nguo alizovaa mara ya mwisho,’’ alisema.

Ndugu wa marehemu, Edward Mwambaghi alisema walipata taarifa za kuwepo mwili wa mtu katika pori la Nkisyo, ndipo walifutilia na kubaini ni mtoto wao aliyetoweka.

Alisema katika uhai wake, marehemu alikuwa na maendeleo mazuri shuleni na aliishi vizuri na jamii, hivyo wameumizwa na tukio hilo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Lyenje, Chuo Mwakasege alisema hawezi kuzungumzia lolote juu ya tukio hilo, analiachia Jeshi la Polisi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kusaga alipoulizwa alisema yupo nje ya mkoa na kwamba atalifuatilia na kujua uhalisia wake.

Akizungumza kwa masharti ya kutoandikwa jina gazetini, mkazi wa kata ya Ikuti alisema hilo ni tukio la tatu kutokea kwa watu kutoweka katika mazingira ya kutatanisha na mabaki ya miili yao kupatikana baadaye .

Aliiomba Serikali kushirikiana na wakiwepo wazee wa mila (machifu) kutoa elimu kwa jamii kupinga matukio hayo.