Mwili wa Mzee Mwinyi kuagwa Uwanja wa Uhuru leo

Muktasari:

  • Mzee Mwinyi alifikwa na mauti saa 11.30 jioni ya  jana Alhamisi, Februari 29, 2024 katika Hospital ya Mzena, Kijitonyama, Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya saratani ya mapafu.

Dar es Salaam. Mwili wa Mzee Ali Hassan Mwinyi (98), Rais wa Awamu ya Pili wa Tanzania utaagwa leo Ijumaa, Machi 1, 2024 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Mzee Mwinyi alifikwa na mauti saa 11.30 jioni ya  jana Alhamisi, Februari 29, 2024 katika Hospital ya Mzena, Kijitonyama, Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya saratani ya mapafu.

Rais Samia Suluhu Hassan ndiye alitangaza kifo chake na kutangaza siku saba za maombolezo kuanzia leo Ijumaa na bendera zikipepea nusu mlingoti.

Mwili wa Mzee Rukhsa utazikwa kesho Jumamosi, Machi 2, 2024 Ungunja visiwani Zanzibar.

Kwa mujibu wa ratiba, Mwili wa Rais huyo wa Pili wa Tanzania (1985-1995) utawasili uwanjani hapo saa 5 asubuhi ukitokea nyumbani kwake, Mikocheni m, Dar es Salaa.

Shughuli mbalimbali zitafanyika uwanjani hapo ikiwemo Swala ya Ijumaa na Swala ya Hayati. Kutoa salamu za rambirambi na heshima za mwisho.

Baada ya hapo, Mwili wa Mzee Mwinyi utapelekwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tayari kwa safari ya kwenda Zanzibar leoleo na utazikwa kesho Jumamosi.

Mei 8, 1925, ndio tarehe ambayo Mwinyi alizaliwa. Kijiji cha Kivure, Wilaya ya Mkuranga, Pwani.

Mwinyi akiwa mtoto, alipelekwa Zanzibar kusoma madrasa (elimu ya dini ya Kiislam). Tangu hapo, Mwinyi alikulia na kusoma Zanzibar hadi kufikia daraja kubwa la uongozi.

Amekuwa Rais wa Zanzibar 1984 hadi 1985. Rais wa Tanzania 1985 hadi 1995.

Mwanasiasa mkongwe nchini, Profesa Mark Mwandosya ametumia ukurasa wake wa X kukumbuka kiongozi huyo akisema,"tumepokea tangazo la kifo cha Mzee wetu mpendwa Mhe. Ali Hassan Mwinyi, kwa masikitiko makubwa.

Rais Mwinyi alituvusha katika kipindi kigumu kama Taifa. Daima tutamkumbuka. RIP."

Ujumbe huo wa Profesa Mwandosya umeambatana na picha iliyopigwa Novemba 1990 wakati akiapishwa na Mzee Mwinyi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini.