Warioba, Wasira, Profesa Lipumba wamkumbuka Mwinyi

Muktasari:

  • Mzee Ali Hassan Mwinyi aliyekuwa Rais wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano, amefariki katika  Hospitali ya Mzena, Kijitonyama jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu  akiwa na miaka 98.

Dar es Salaam. Kufuatia kifo cha Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi kilichotokea leo Februari 29, 2024 jijini hapa, Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba amemweleza kiongozi huyo kuwa jasiri aliyepambana kuinua uchumi na mageuzi ya kisiasa.

Mbali na Jaji Warioba, mwanasiasa mkongwe Stephen Wasira na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba nao wamemwelezea kiongozi huyo kuwa jasiri.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo, Jaji Joseph Warioba amesema kiongozi huyo atakumbukwa kwa mambo makubwa mawili, ambayo ni kupigania uchumi na mageuzi ya kisiasa.

“Huu ni msiba mkubwa kwa Taifa. Rais Mwinyi alichukua uongozi wakati nchi ikiwa kwenye matatizo makubwa. Ni kipindi ambacho matukio yaliyotokea yaliifanya hali ya nchi kuwa ngumu sana.

“Wakati huo Jumuiya ya Afrika Mashariki ilikuwa imevunjika, tukalazimika kutumia masharti mengi kuanzisha mashirika mapya. Tulikuwa tumepigana vita ya Kagera ambayo tulichukua fedha zote za nje tulizokuwa nazo, kwa hiyo nchi ilikuwa kwenye matatizo makubwa,” amesema.

Akifafanua zaidi kuhusu mageuzi ya kiuchumi na kisiasa, Warioba aliyekuwa Waziri Mkuu kuanzia Novemba 5, 1985 hadi Novemba 9, 1990 amesema alishirikiana na Mzee Mwinyi kupambana na changamoto za uchumi.

“Nchi haikuwa na uwezo wa kununua vitu, kwa sababu hatukuwa na fedha za nje, kwa mfano, mafuta yalikuwa hayatoshi kwa hiyo kuendesha shughuli za kuzalisha ilikuwa ngumu, nchi ilikuwa na upungufu wa chakula.”

“Wakati huo mwaka 1984 tulikuwa na vuguvugu la kisiasa kwa ndani, lakini kidunia pia kulikuwa na vuguvugu la mabadiliko ya kisiasa, kwa hiyo ilibidi ashughulike nayo mawili,” amesema.

Ametaja sifa za Mzee Mwinyi wakati huo kuwa pamoja na kusikiliza wasaidizi wake.

“Aliteua timu yake ya mawaziri, alitusikiliza sana, alitaka kila mtu atoe mawazo ili tupate njia na tukapata mipango ya kushughulikia haya, lakini uamuzi ulikuwa uwe mgumu na kwa kawaida inabidi awe anafanya Rais,” amesema.  

Amesema licha ya kuonekana kuwa mpole awali, Mzee Mwinyi alikuwa akichukua uamuzi mgumu.

“Katika miaka ile mitano ya kwanza alisimamia hali ya uchumi ikaanza kuwa imara na miaka iliyofuata, alisimamia mabadiliko ya kisiasa na yote yalifanyika katika hali ngumu, akisema umoja wetu na amani yetu isije ikapotea,” amesema.

Kwa upande wake Mzee Stephen Wasira ambaye pia alifanya naye kazi, alimtaja Mzee Mwinyi kuonyesha ujasiri kwa kipindi alichoingia madarakani.

“Mimi nilimfahamu Mzee Mwinyi nikiwa bado kijana mdogo, nilikuja Bunge la Tanzania nikiwa na miaka 25, wakati huo Mzee Mwinyi alikuwa tayari ni Waziri wa Afya katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano katika kipindi cha awamu ya kwanza cha Mwalimu Julius Nyerere,” amesema.

Amesema Mwinyi akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano alimteua kuwa Naibu Waziri wa Serikali za Mitaa na Vyama vya Ushirika akimsaidia Waziri Ngombare Mwiru na baadaye Paul Bomani, halafu akampandisha kuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Ushirika mwaka 1989 hadi 1990.

Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1990, wasira aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani.

“Aliingia katika Serikali wakati nchi ikiwa kwenye hali ngumu na mahitaji ya watu yalikuwa magumu kupatikana. Ndiyo maana alitoa vibali kwa watu kuingiza bidhaa kutoka nje ya nchi.

“Huu ni msiba mkubwa, nimeupokea kwa masikitiko kwa sababu Mzee Mwinyi ametoa mchango mkubwa kwa historia na maendeleo ya Tanzania,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema msiba huo ni mkubwa, kwani Mzee Mwinyi alitoa mchango mkubwa kwa Taifa hili hasa katika kurekebisha uchumi.

Profesa Lipumba aliyewahi kuwa mshauri wa uchumi wa Rais Mwinyi, amesema wakati Rais Mwinyi anaingia madarakani mwaka 1985, hali ya uchumi ya Tanzania ilikuwa mbaya.

“Alianzisha marekebisho ya mfumo wa kisiasa nchini kwa kuteua Tume ya Jaji Francis Nyalali ambayo ilipendekeza tuwe na mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, pamoja na kwamba walipendekeza kufanyika kwa mabadiliko ya kikatiba na hayakufanyika wakati huo, lakini aliwezesha kufanyika marekebisho ya katiba kuruhusu mfumo wa vyama vingi.

“Kwa hiyo, mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi ni mambo ambayo yalianza wakati wa kipindi cha Mzee Mwinyi na alikuwa ni mtu mtulivu, si mtu wa mabavu. Alikuwa ni mtu anayeheshimu haki za binadamu na alikuwa mwepesi kuwasikiliza wananchi,” amesema Profesa Lipumba.

Mwanasiasa huyo mkongwe amesisitiza kwamba Mzee Mwinyi aliweza kuleta umoja wa kitaifa na kwamba akiwa Rais wa Zanzibar, pia, aliwaletea mabadiliko makubwa baada ya Rais Abdul Jumbe kujiuzulu kwa kufanya mageuzi ya kisiasa na kiuchumi na wakati huo Maalim Seif Sharif Hamad alikuwa Waziri Kiongozi wake.

“Tutamkumbuka kama mwasisi wa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi katika miaka ya 1990 na mwasisi wa mabadiliko ya kiuchumi kwa kujenga uchumi wa soko katika nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema.