Mwili wa padre aliyekuwa akitibu kwa miti shamba waagwa Moro

Muktasari:

Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Morogoro, Telesphor Mkude ametumia Ibada ya Misa Takatifu ya kumuaga Padre Sebastian Kuzhupil kuwataka mapadre, waumini na Watanzania kutumia miito wanayopata kutoka kwa Mungu kwa kutoa huduma kwa maskini, wagonjwa na wasiojiweza.

Morogoro. Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Morogoro, Telesphor Mkude ametumia Ibada ya Misa Takatifu ya kumuaga Padre Sebastian Kuzhupil kuwataka mapadre, waumini na Watanzania kutumia miito wanayopata kutoka kwa Mungu kwa kutoa huduma kwa maskini, wagonjwa na wasiojiweza.

Padri huyo maarufu father wa Kihonda ambaye alikuwa akitoa huduma ya matibabu kwa njia ya miti shamba alifariki dunia Juni 26 mwaka jijini Dar es Salaam wakati akipatiwa matibabu.

Akizungumza leo Alhamisi Juni 30, 2022 wakati wa ibada hiyo iliyofanyika katika Seminari ya Mtakatifu Francis De Sales ya mjini Morogoro, Askofu Mkude ametoa rai hiyo akiwataka waumini kutoa huduma kwa watu wenye uhitaji.

Akimzungumzia padri Kuzhupil, amesema wakati wa uhai wake alitumika kama chombo kusaidia maskini, wagonjwa na alitumia karama ya kipekee kwa kuwafanya wakatoliki kuacha kutangatanga katika kutafuta uponyaji.

"Kupitia karama aliyopewa na Mungu nitasikitika kama hatotokea wa kurithi na kuendeleza huduma aliyokuwa anaitoa katika kituo chake kwani bado wapo watu wengi wanahitaji huduma ya uponyaji,"amesema Askofu Mkude.

Amesema katika miaka 25 ya huduma ya upadri alijitambua na kutoa huduma ya matibabu kama wajibu wake, na alitunza Utawa wake.

"Alitajwa kuwa mtu wa moyo safi na mahitaji ya waliowengi, alikubali kutotanguliza matashi binafsi," alisema.

Marehemu Padre Kuzhupil MSFS, alizaliwa nchini India Machi 25 Mwaka 1951 na ametumikia huduma ya upadri mkoani Morogoro nchini Tanzania tangu Mwaka 1997, anatarajiwa kuzikwa kesho Ijumaa katika makaburi ya Shirika la Wamisionari la Fransisco Mkuza, Kibaha.

Katika uhai wake Pardi Kuzhupil aliyekuwa akifahamika kama father wa Kihonda alikuwa akitoa huduma ya matibabu kwa njia ya miti shamba na inadaiwa alikuwa akitibu magonjwa mbalimbali kama sukari, Kifua Kikuu, kansa, moyo, pamoja na waliokuwa wakipata shinikizo la moyo.

Mmoja wa wanafunzi aliyokuwa akiwasomesha (kuwafadhili), Janeth Shija anayesoma shule ya msingi Mount Camel amesema padre huyo aliweza kumtibu ugonjwa wa moyo tangu akiwa mdogo.

Mwalimu wa Biblia Seminari ya Mtakatifu Francis De Sales, Sanford Mahumi amesema Padri Kuzhupil alikuwa akisomesha vijana wengi, akitoa huduma ya matibabu kwa rika na makabila yote bila kubagua, hivyo kama Seminari watafuata na kuendeleza yale yote aliyoyaanzisha.

Mahumi amesema alianza kuugua mwezi Aprili mwaka huu na kuendelea kupata matibabu katika hospitali ya Mtakatifu Francis Dumila na baadae kuhamishiwa hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam ambapo alizidiwa na baadaye kufariki dunia.