Mwinyi: Amani ni neno lenye herufi chache, uzito mkubwa

Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi
Muktasari:
Mwinyi alitoa rai hiyo jana wakati wa mkutano wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi amesema amani ni neno lenye herufi chache lakini lina uzito mkubwa katika uhusiano wa jamii, hivyo viongozi wana wajibu wa kulinda nguzo hiyo kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Mwinyi alitoa rai hiyo jana wakati wa mkutano wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Dar es Salaam.
Baadhi ya viongozi washiriki walisema haijalishi tofauti walizonazo kwenye jamii lakini jambo la msingi ni kuvumiliana na kuungana katika ulinzi wa amani.
Katika mkutano huo, baadhi ya viongozi hao wa dini walizungumzia kuvurugika kwa amani wakisema, moto mkubwa huanza kwa cheche hivyo Serikali haitakiwi kupuuzia cheche zinazoonekana kwa sasa na badala yake iziondoe.
Mzee Mwinyi aliwataka viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani katika majukwaa mbalimbali yaliyopo nchini kwa kuwa ni nguzo endelevu kwa kizazi kijacho.
“Kamati hii haitakiwi kuwa na maneno mengi, kazi yake kubwa ni kuhubiri amani imfikie kila mtu bila kujali tofauti za kiitikadi au hali zao,” alisema.
Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sosthenes alitaja athari za kuharibu amani kuwa ni pamoja na kuathirika kwa wanyonge na kukosa uhuru wa kuwa na mikusanyiko.
Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir aliwaomba viongozi wa dini kutumia majukwaa kuhubiri amani.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Sheikh Alhad Mussa Salum alisema lengo la mkutano huo kufanyika kwa wakati huu ni kutokana na kuwapo kwa viashiria vya uvunjifu wa amani nchini.