Mwinyi ashtukia watendaji kukejeli Mfumo wa Sema na Rais

Unguja. Wakati mfumo wa Sema na Rais (SNR) ukitimiza miaka miwili, malalamiko 10,434 yamepokewa kutoka kwa wananchi wakiwa na kero mbalimbali.
Mfumo huo ulionzishwa na Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi lengo lake ni wananchi wapate fursa ya kuwasilisha changamoto zao zinazowakabili katika taasisi za serikali na binafsi na kupatiwa ufumbuzi.
Akizungumza leo wakati wa kikao kazi katika kuadhimisha miaka miwili ya SNR, Rais Mwinyi amesema licha ya mafanikio yanayopatikana kupitia mfumo huo bado kuna watendaji wanaotoa lugha za kejeli na kudharau mfumo huo kwa madai haupo kisheria.
“Sisi tunajaribu kujenga anatoka mtu mmoja anazungumza maneno ya kifedhuli anadhani sisikii, kuna vitu vichache tu ambavyo sivipati na yapo mengine ambayo sichukui hatua.
“Sio kwa sababu sijasikia natumia ubinadamu tu lakini ikifika mtu anadhalilisha mamlaka huyo hafai kuwepo ndani ya utendaji wa serikali,” alisema.
Ametumia fursa hiyo kuwataka makatibu wakuu na wakuu wa taasisi za Serikali kuhakikisha wanachukua hatua kwa maofisa wa SNR ambao hawataki kuwajibika na sio kumsubiria achukue hatua yeye bali ni kuona watendaji hao wanamuwajibisha mtendaji haraka kwani ndio maana ameweka viongozi katika kila wizara na taasisi kwa lengo la kumsaidia.
Naye Mratibu wa SNR, Haji Khamis Makame, amesema mfumo huo ulianzishwa kwa matakwa ya wananchi kupata fursa ya kuwasilisha changamoto zao zinazowakabili katika tasisi za serikali na binafsi na kupatiwa ufumbuzi.
Amesema tangu kuanzishwa kwa mfumo huo Febuari 27 mwaka 2021 jumla ya malalamiko 10,434 yamepokelewa na malalamiko 8,306 sawa na asilimia 79.6 yamaepatiwa ufumbuzi na malalamiko 2,128 sawa na asilimia 20.4 yanaendelea kufuatiliwa ili kupatiwa ufumbuzi.
Amebainisha kwamba mfumo huo umeunganishwa kwa taasisi 62 na kuongeza taasisi nyingine tano kutoka Pemba.
Amesema ili kujenga uelewa wa mfumo huo kitengo cha SNR Ikulu kinachosimamia na kuratibu mfumo huo kimewapatia semina elekezi ya mfumo watendaji 778 wa SMZ na SMT kwa Unguja na Pemba.
Ofisi zilizofanya vizuri ni Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa ambao wamepokea malalamiko 810 na kutatua 804 wameyapatia ufumbuzi sawa na asilimia 99.2, Wizara ya Elimu malalamiko 782, mamlka ya maji malalamiko 605, shirika la umeme malalamiko 593 na Wizara ya Ujenzi malalamiko 559.
Taasisi ambazo hazikufanya vizuri alisema ni Manispaa Magharibi A, Manispaa Mjini, Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Kamisheni ya Ardhi na Jeshi la Polisi.