Mwinyi aunda kamati dhidi ya unyanyasaji

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi (katikati) akiongoza Mkutano wa wadau wanaohusika na masuala ya udhalilishaji mjini Zanzibar jana.

Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameshauri kuundwa kamati maalumu itakayowashirikisha wadau mbalimbali ili kulitafutia ufumbuzi tatizo la udhalilishaji wa kijinsia lililokithiri katika jamii.

Dk Mwinyi ametoa ushauri huo jana katika mkutano uliojadili masuala ya udhalilishaji wa kijinsia na namna ya kukabiliana na uhalifu huo na kuwashirikisha wadau wa ngazi zote, uliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul-Wakil, Kikwajuni, Zanzibar.

Alisema kutokana na ukubwa wa tatizo la udhalilishaji hapa nchini, kuna umuhimu wa kuunda kamati maalumu itakayowashirikisha wadau mbalimbali, likiwemo Jeshi la Polisi, mahakama na Ofisi ya mwendesha mashtaka.

Alisema kamati hiyo itafanya kazi kwa kuzingatia hadidu za rejea na kuyapatafutia ufumbuzi matatizo mbalimbali, ikiwemo yale yatokanayo na wao wenyewe.

Rais Mwinyi alisema miongoni mwa majukumu ya Kamati hiyo itakuwa ni kufuatilia kesi zilizoko mahakamani, kuangalia haja ya marekebisho ya sheria, uimarishaji wa maeneo ya kupima waathirika wa matukio ya udhalilishaji na kuimarisha madawati ya polisi.

Alieleza kuwa suala la udhalilishaji ni kubwa na limekuwa likiitia aibu nchi pamoja na kuleta maumivu makubwa kwa waathirika, hivyo, akataka itambulike kuwa ni vita ya kitaifa na kila mmoja pale alipo atapaswa kutoa ushirikiano ili kumaliza tatizo hilo.

Kiongozi huyo alisema suala la rushwa ni miongoni mwa changamoto zinazokwaza utoaji haki katika vyombo vya sheria, hivyo, taasisi za polisi, mahakama na hospitali zijitathmini na kuondokana na mambo hayo.

Alisema sasa ni wakati wa Wizara ya Afya kuimarisha sehemu za upimaji wa waathirika wa matukio ya udhalilishaji pamoja na kuwa na vifaa vya kazi vya kutosha, ili jamii iweze kuondokana na usumbufu.

Mapema, mada tano ziliwasilishwa katika mkutano huo, ambapo Mkurugenzi wa jinsia na watoto, Nasima Haji Chum alisema suala la udhalilishaji ni mtambuka linalohitaji mashirikiano kati ya jamii na vyombo vya sheria.

Kwa upande wake, Mrajisi wa Mahakama Kuu Zanzibar Mohamed Ali Mohamed alisema miongoni mwa changamoto zinazofanya kukosekana ufanisi ni mashahidi kushindwa kufika mahakamani kutokana na nasaba za kifamilia na hivyo kesi nyingi hatimaye kuishia kwa usuluhishi.