Mwisho wa enzi kwa Balozi John Rupia

Pichani ni Paul Milyango Rupia (kulia) enzi za uhai wake, akivishwa Nishani Daraja la Pili ya Kumbukumbu ya miaka 50 ya Muungano na Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete. Picha na mtandao

Muktasari:

  • Katibu Mkuu Kiongozi wa zamani, Balozi Paul Rupia amefariki nchini Afrika Kusini alikokuwa akipatiwa matibabu. Balozi Rupia aliyekuwa na umri wa miaka 86, alifariki jana asubuhi nchini humo, hata hivyo taratibu za mazishi bado hazijawekwa wazi.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu Kiongozi wa zamani, Balozi Paul Rupia amefariki nchini Afrika Kusini alikokuwa akipatiwa matibabu. Balozi Rupia aliyekuwa na umri wa miaka 86, alifariki jana asubuhi nchini humo, hata hivyo taratibu za mazishi bado hazijawekwa wazi.

Taarifa za kifo chake zilithitibishwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine ambaye hata hivyo hakutaka kuzungumzia zaidi kifo hicho.

“Taarifa hizo ni za kweli, amefariki akiwa Afrika Kusini,” alisema Balozi Sokoine kwa kifupi.

Rais Samia Suluhu Hassan aliandika katika ukurasa wake wa Twitter akieleza kusikitishwa na kifo cha Balozi Rupia akimwelezea kama kiongozi aliyetoa mchango mkubwa katika masuala ya kidiplomasia.

“Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Paul Rupia. Tumeondokewa na mtu aliyetoa mchango mkubwa katika masuala ya kidiplomasia, mageuzi ya kiuchumi na utumishi wa umma, na aliyeweka mbele masilahi ya Taifa. Mungu amweke mahali pema. Amina,” ameandika Rais Samia.

Akizungumza na gazeti hili kuhusu kifo cha Rupia, Balozi Ami Mpungwe alisema anamfahamu marehemu kama kiongozi mlezi, ambaye alipenda kusaidia wengine na alikuwa na mweledi katika kazi yake na alizingatia maadili katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Kwa kweli ni mshituko mkubwa sana, Balozi Rupia ni mtu ambaye nimefanya naye kazi nikiwa kijana.

“Hawa ndiyo walitufundisha kazi na kutuongoza na kusema kweli, Balozi Rupia hakuwa tu kiongozi alikuwa kaka yetu na mtu mweledi, mwenye maadili akisaidia hata matatizo mengine ambayo sio ya kazi,” alisema.

Balozi Mpungwe alisema Balozi Rupia alikuwa kiongozi na mlezi katika maisha yake ya kazi: “Mimi na wengine tumepitia malezi ya kiongozi huyo.


Balozi Rupia ni nani?

Paul alizaliwa katika Hospitali ya Kolandoto mkoani Shinyanga Julai 21, 1938 akiwa mtoto wa John Rupia na Lois Rupia.

Kwa nyakati tofauti, (Baba yake) John Rupia amekuwa mwasisi wa chama cha TAA (Tanganyika African Association), Tanu, (Tanganyika African National Union) na AA (African Association (AA) na alishiriki katika baraza maarufu la wazee wa Tanu wakati huo akiwa pamoja na kina Mzee Mwinyikambi, Tambaza, Mshume, Chamwenyewe, Haidar Mwinyimvua na Rajab Diwani.

Walipotoka TAA na kuanzisha Tanu, John Rupia alipewa nafasi ya kuwa Makamu Mwenyekiti chini ya uongozi wa Julius Nyerere, akiwa na kadi namba 7. Baba yake, John Rupia, alikuwa Makamu wa Rais wa Tanu ilipoanzishwa Julai 7, 1954 wakati Mwalimu Julius Nyerere akiwa Rais wa chama hicho. Amos Kissenge alikuwa Naibu Katibu wa uenezi wa Tanu; Mzee Jumbe Tambaza, mjumbe wa baraza la wazee wa Tanu; Juma Selemani, kijana maarufu kwa jina la utani, “Juma ‘Mlevi,” katibu wa Kundi la Bantu.

Kwa kuwa mama yake alifariki dunia wakati Paul akiwa bado ni mtoto, Mzee John Rupia alilazimika kufanya mpango wa kupata vyumba maalumu katika Shule ya St. Andrew, Minaki ambako alipata elimu yake ya msingi na sekondari.

Alipata elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari ya Aga Khan ya mjini Dar es Salaam. Baadaye, mwaka 1957, chama cha Tanu kilipata ufadhili wa masomo kuruhusu wanafunzi kwenda kusoma nchini Liberia.

Miongoni mwa wanafunzi waliopata nafasi hiyo ni Paul. Huko alijiunga na na chuo cha Cutington, Liberia na kisha Chuo Kikuu cha New York, Marekani.

Kwa mujibu wa kitabu ripoti ya wanavyuo ya mwaka 1960 inayoitwa ‘Statistics of Land-grant Colleges and Universities’, zilizotayarishwa katikati ya mwaka 1959 zilionyesha wakati huo kulikuwa na Waafrika 70 wa Tanganyika wenye shahada na Waafrika 44 wa Tanganyika wenye stashahada.

Kutoka Makerere kulikuwa na wahitimu wa Tanganyika 12 mwaka 1955, 20 mwaka 1956, 20 mwaka 1957, 15 mwaka 1958, na 32 mwaka 1959.

Ripoti hiyo inasema: “Wanafunzi wote isipokuwa mmoja kati ya 12 wa Liberia waliofadhiliwa na Tanu, ambayo pia imefadhili wanafunzi nchini Uingereza, Marekani na nchi nyingine.” Miongoni mwa hao ni Paul Rupia.

Baada ya kumaliza chuo alijiunga na Wizara ya Mambo ya Nje mwaka 1963 na kupitia teuzi mbalimbali ikiwamo mwaka 1976 alipoteuliwa kuwa mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.

Mwishoni mwa mwaka huo wa 1976 aliteuliwa na Mwalimu Nyerere kuwa Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) mjini Addis Ababa, kabla ya mwaka 1980 kuteuliwa kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.

Miaka mitatu baadaye, 1984, Rupia alirejea Tanzania na kuteuliwa na Mwalimu kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje.

Alikaa katika wadhifa huo hadi mwaka 1986 wakati Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, alipomteua kuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo, Balozi Rupia aliendelea na wadhifa huo hadi alipogombea ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 na kuchaguliwa kuwa mbunge wa Jimbo la Ukonga, Dar es Salaam, kabla ya kupoteza kiti hicho katika uchaguzi wa mwaka 2000.

Balozi Rupia ameacha mjane Rose Rupia na watoto Peter, Suzan, Pauline na Simon.