Mwitikio wa wanawake kupima afya ya uzazi uko chini Kibaha

Thursday October 14 2021
uzazi pc
By Mwandishi Wetu

Kibaha. Hali ya mwitikio wa wanawake kujitokeza kupima saratani ya mlango wa uzazi katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha Mkoa wa Pwani inaelezwa kuwa ni ya kusuasua ukilinganisha na matakwa na kanuni za afya.

Ili kulisaidia kundi hilo, Halmashauri ya Mji wa Kibaha kwa kushirikiana na wadau wa afya wameanza  kuwafanyia uchunguzi wanawake kama wana maambukizi ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi ambao unasababisha vifo.

Hayo yamebainishwa jana Oktoba 13 mjini hapa na Mratibu wa Afya ya Uzazi wa Kibaha Mji, Prisca Nyambo alipozungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema kuna changamoto kwa wanawake wengi kutofanya uchunguzi afya ya uzazi.

"Ugonjwa huu kwa asilimia 70 unaambukizwa na kurusi na ili kumsaidia mwanamke katika tatizo hilo ni kumfanyia uchunguzi na akibainika na dalili hizo mapema anapata matubabu kiurahisi," amesema.

Akifafanua zaidi, Nyambo amesema kwa baadhi ya watu, ugonjwa huo hauonyeshi dalili zozote hali ambayo inawafanya wengi wao kutokujua kama wana tatizo hilo na wanapokuja kugundua tayari wanakuwa wameathirika.

Mmoja wa wanawake waliofanyiwa uchunguzi kwenye Zahanati ya Visiga, Fatuma Said amesema kuwa amepima na amejikuta yuko salama na kuwataka wanawake kujitokeza kufanyiwa uchunguzi ili kuwa na uhakika wa afya zao.

Advertisement

Amesema kuwa kutokana athari za ugonjwa huo ni vema wanawake wakajitokeza kupima afya zao kwani itawasaidia kupata matibabu mapema kama watagundulika na tatizo na kama hawaambukizwa basi watajua namna gani ya kujilinda ili wasipate maambukizi hayo.

Kwa upande wake Diwani wa Viti Maalumu Tarafa ya Kongowe, Dorice Michael akizungumza baada ya kufanyiwa uchunguzi kwenye zahanati ya Visiga amesema kuwa ameamua kuungana na wanawake ili kujua afya yake huku akiwahimiza wengine kujitokeza kufanya hivyo.

Advertisement