Mzazi afunguka mwanaye kubadilishiwa namba ya mtihani

Muktasari:

Atwiya Mohamed, mzazi wa mwanafunzi Iptisum Suleiman Slim wa Shule ya Msingi Chalinze Modern Islamic Pre and Primary ya mkoani Pwani aliyebadilishiwa namba ya kufanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba ameeleza mkasa ulivyokuwa na uchungu aliopitia mwanaye kabla ya kutoboa siri hiyo.

Dar es Salaam. Atwiya Mohamed, mzazi wa mwanafunzi Iptisum Suleiman Slim wa Shule ya Msingi Chalinze Modern Islamic Pre and Primary ya mkoani Pwani aliyebadilishiwa namba ya kufanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba ameeleza mkasa ulivyokuwa na uchungu aliopitia mwanaye kabla ya kutoboa siri hiyo.

Mama huyo anayeishi Kimara Dar es Salaam, alisema alibaini tatizo hilo baada ya kumuona mtoto wake hana furaha na alikuwa akilia kwa siku tatu tangu walipotoka kwenye mahafali yaliyofanyika Oktoba 8, 2022 shuleni hapo.

Juzi video iliyosambaa kwenye mitandao ya jamii ilimwonyesha Ipstisum akieleza jinsi msimamizi wa mitihani wa darasa la saba uliofanyika Oktoba 5 na 6, 2022 alivyombadilishia namba yake ya 39 na kumtaka atumie 40 na baadaye mwalimu wa shule hiyo (amemtaja kwa jina) aliwataka baadhi ya wanafunzi kutotoa siri ya kilichotokea.

Katika video hiyo, Iptisum amemwomba Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amsaidie apate haki yake baada ya kufanyishwa mtihani kupitia namba ya mwanafunzi aliyekuwa akifanya vibaya darasani.

Mwananchi limebaini kuwa suala hilo lilianza kujulikana siku ya mahafali ambapo mtoto huyo hakutaka kushiriki.

Mkasa wa mtoto huyo unasimuliwa na mama yake Atwiya Mohamed, mkazi wa Kimara Dar es Salaam aliyeshuhudia mahafali ya Oktoba 8, 2022 yakigeuka shubiri baada ya mwanaye kutotaka kushiriki jambo lolote.

“Aliponiona akaniambia hataki kukata keki, nilimuuliza hutaki kumlisha hata mwalimu wako, akaniambia sitaki kumlisha hata mwalimu mmoja tuondoke, nilianza safari ya kurudi naye Dar es Salaam akiwa kwenye kiti cha nyuma cha gari, baada ya muda alianza kulia kwa kwikwi, nilipomgeukia akajifanya yupo sawa, nikamuuliza ana shida gani akaniambia yupo sawa,” alisema.

Siku tatu baada ya mahafali, Iptusm alimweleza mama yake kinachomuumiza.

“Niliwaza vitu vingine kwasababu ni mtoto wa kike, nilitaka kumpeleka hospitali, alinifuata akaniambia ‘mama kuna kitu nataka kukuambia kimenishinda,’ akaniambia mimi sikufanyia mtihani namba yangu ambayo ni 39 lakini mimi nilifanyia mtihani namba 40,” alisimulia mama huyo.

Baada ya mtoto huyo kutambua namba si yake aliwasiliana na wasimamizi wa mitihani na kuambiwa asiwe na wasiwasi hilo ni jambo dogo litashughulikiwa Baraza la Taifa la Mitihani (Necta).

“Baada ya kufanya mitihani mitano akarudishwa kwenye namba yake 39 kumalizia mtihani uliobaki, anasema alilia sana mpaka wanafunzi wenzake wakawa wanamuangalia, msimamizi akamfuata akamuambia asiwe na wasiwasi, baada ya kumshirikisha mwalimu mkuu akaambiwa asiwe na wasiwasi itaenda kubadilishwa Necta,” alisema.

Mama huyo alisema juhudi za kuwasiliana na uongozi wa shule hiyo kupata ufafanuzi ziligonga mwamba kwa kukatiwa simu.

“Siku moja saa tano usiku nikafuatwa na walimu wa Chalinze na mkurugenzi wao wakataka kuongea na mimi, nikawaambia hapana baba yao hayupo, wakaniambia haina shida watamsubiri hata saa nane, baba wa mtoto alivyokuja wakatuomba msamaha wakisema watafidia,” alieleza.

Mama huyo aliwasiliana na mwanasheria wake kuomba ushauri na aliambiwa aende Necta.

“Baada ya kuwasiliana mtu wa moja akaniambia nimrekodi video mtoto wangu nimtumie, hiyo ilikuwa Oktoba 11, 2022 nikafanya hivyo, sijajua aliyesambaza lakini mitandao ya kijamii ina nguvu kubwa imenisaidia,” alisema.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule aliyetambulika kwa jina moja la Salum alikiri kuwepo kwa malalamiko hayo, huku akidai mwenye mamlaka ya kuzungumza ni Mwalimu Mkuu na Mkurugenzi ambao Mwananchi liliwatafuta bila mafanikio.

Tamko la Serikali

Kufuatia malalamiko hayo, Necta ilitoa taarifa suala hilo linafuatiliwa na litahakikisha mwanafunzi huyo anapata haki yake.

Akizungumzia sakata hilo, Naibu Katibu Mkuu (Elimu) Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Charles Msonde alisema tayari Serikali inafanyia kazi tuhuma hizo.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania (Tamongsco), Leonard Mao alitaka ufanyike uchunguzi huru ili ijulikane tatizo ni kwa mwalimu mkuu wa shule husika au Necta.