Necta kufuatilia madai mwanafunzi kubadilishiwa namba ya mtihani

Muktasari:

Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limesema linafanyia kazi tuhuma alizozitoa mwanafunzi wa shule ya msingi Chalinze Modern Islamic, Mkoa wa Pwani, Iptisum Slim aliyedai kubadilishiwa namba yake ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi Oktoba 5-6, 2022.

  


Dar es Salaam. Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limesema linafanyia kazi tuhuma alizozitoa mwanafunzi wa shule ya msingi Chalinze Modern Islamic, Mkoa wa Pwani, Iptisum Slim aliyedai kubadilishiwa namba yake ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi Oktoba 5-6, 2022.

Kupitia video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii mwanafunzi huyo mhitimu wa darasa la saba, 2022 amemuomba Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda kuingilia kati madai ya kufanya mtihani na namba ambayo si yake.

Leo Oktoba 14 kupitia taarifa iliyotolewa na Afisa Habari na Uhusiano Necta, John Nchimbi imeeleza baraza hilo linafanyia kazi taarifa hiyo ili mwanafunzi huyo apate haki yake.



“Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) limeona taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha mtahiniwa Iptisum Suleiman Slim wa Shule ya Msingi Chelinze Modern Islamic ‘Pre and Primary School akisema kwamba alibadilishiwa namba yake ya mtihani wakati akifanya mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi uliofanyika tarehe 5 na 6 Oktoba 2022.

“Baraza linaifanyia kazi taarifa hiyo kuhakikisha mwanafunzi huyo anapata haki yake,”imeeleza taarifa hiyo.

Iptisum kupitia video hiyo alionekana akiomba msaada huku akieleza, siku ya mtihani wa taifa alivyoingia darasani alipangiwa namba 40 na wakati karatasi ya kusaini ilivyopita alisaini namba 39.

Ameeleza kuwa baada ya kufanya mitihani mitano kupitia namba 40 ambayo si yake alihamishiwa namba 39 ambayo ni yakwake.

“Baada ya mtihani kuisha baadhi ya wanafunzi tuliitwa na mwalimu mkuu tukaambiwa yale yaliyotokea yasisikike sehemu nyingine yaishie palepale.

“Naomba msaada nisaidiwe kisheria kupata haki majibu yangu yarudi kwenye namba yangu kwa sababu mtoto niliyemfanyia mtihani anashika nafasi ya chini na mimi nashika nafasi za juu hata Mtihani wa Moko wilaya nilishika nafasi ya kwaza,”ameeleza mtoto huyo.


Pia kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima ameandika

 

“Mtoto wetu mpendwa sana, kwanza pole kwa mtihani, hongera kumaliza darasa la saba. Badala ya kumaliza upumzike wamekutengenezea jambo. Kwa nafasi yako kama mtoto iwapo hili limetokea nao ni ukatili kwa mtoto.

“Waziri wa Elimu na NECTA wapo pamoja na wewe mtoto mzuri kuchunguza hili Ili haki itendeke.

 “wizara yenye dhamana na maendeleo ya watoto jicho letu, sikio letu na mguu wetu vipo walipo watoto wanaolalamika kwa chochote hivyo, katika hilo tunaungana na wizara ya Elimu hadi tuone mwisho wa hii hoja” Dk Gwajima ameandika.