Mzazi aliyezabwa vibao na muuguzi afunguka

Rukwa. Zulfa Said (28), aliyeripotiwa hivi karibuni kupigwa makofi na muuguzi wa zamu baada ya kujifungua sakafuni katika kituo cha afya Mazwi kilichopo mjini Sumbawanga mkoani Rukwa, ameitaka mamlaka husika kuchukua hatua sitahiki ili iwe fundisho.

Serikali ilishaanza kuchukua hatua juu ya suala hilo, ambapo Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto, Dk Dorothy Gwajima hivi karibuni aliliagiza Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania (TNMC) kuchukua hatua.

Tayari mtumishi huyo, Valentine Kinyaga amesimamishwa kazi, wakati suala hilo likichunguzwa na uongozi wa Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa.

Pia ujumbe wa Chama cha Wauguzi na Wakunga Tanzania (TANNA) upo mkoani Rukwa kufuatilia suala hilo.

Akizungumza na Mwananchi juzi jioni akiwa nyumbani kwake, mwanamke huyo aliyejifungua wiki iliyopita alisema kitendo alichofanyiwa si cha kibinadamu na hakivumiliki.

Muuguzi huyo Kinyaga alipotafutwa na Mwananchi jana alieleza hataki kuzungumzia suala hilo, kwani tayari ameongea na uongozi wa chama cha wauguzi ingawa amekanusha kufanya kitendo hichoe.

“Sikumpiga makofi mgonjwa huyo, kama kweli jambo hilo lingetokea asingekuwa salama kwa hali aliyokuwa nayo na mtoto mchanga,” alieleza Kinyaga kwa kifupi na kukata simu.

Zulfa akisimulia chanzo cha mkasa huo alisema alifika hospitali akiwa na hali mbaya ambapo pamoja na kuomba msaada zaidi ya mara mbili kwa muuguzi huyo, hakusikiliza kilio chake. “Sikupewa ushirikiano huo na nikajikuta najifungulia sakafuni na baadae nikajikuta naambiwa lugha chafu na kipigo juu yake.

“Wakati natoka nyumbani nilikuwa na dalili zote za kujifungua, kwani chupa ya uzazi ilikuwa imepasuka, lakini nikipofika hospitali nilipimwa na kuelezwa siwezi kujifungua muda huo na niondoke kwenye chumba cha kujifungua (Labour) na badala yake niende chumba cha kusubiria,” alieleza mama huyo.

“Nilivumilia kwa muda na kuomba tena msaada, lakini nilipuuzwa, damu zilianza kutoka sehemu za siri na ghafla nikaona mtoto anataka kutoka ndio nilipotandika kanga chini na kujifungua,” alisema na kuongeza kuwa ilimchukua muuguzi huyo kati ya dakika 10 hadi 15 hadi kufika na kumpa huduma, huku mtoto akipigwa na baridi. Zulfa alisema muuguzi huyo alimpiga makofi sehemu mbalimbali mwilini kwa muda mrefu.

Mama mzazi wa dada huyo, Anna Mkusa alidai mwanae hakumwelezea tukio hilo lakini mjamzito mmoja wodini hapo alimweleza, ndipo alipowasiliana na ndugu zake na jirani yake, Pendo Issa ambaye alimsindikiza hospitalini hapo na waliripoti suala hilo.

Ujumbe wa TANNA ukiongozwa na Makamu wa Rais, Ibrahim Mgoo umefika Rukwa na kukutana na uongozi wa Idara ya Afya Manispaa ya Sumbawanga, kituo cha afya Mazwi na muuguzi Kinyaga na Zulfa.