Mzee mbaroni akituhumiwa kulawiti watoto wa shule

New Content Item (1)

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Issa Suleiman

Muktasari:

  • Mzee mwenye umri wa miaka 59 akamatwa kwa tuhuma za kuwalawiti watoto wawili wa miaka minane, alikuwa akiwalaghai wanapotoka shule na kuwapeleka kwenye pagale.

 Mtwara. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara linamshikilia Abdallah Hassan (59) mkazi wa Mtaa wa Kiyangu Maduka Makubwa mjini Mtwara kwa tuhuma za kuwalawiti kwa nyakati tofauti, watoto wawili wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Mtwara Mjini.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Machi 15, 2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Issa Suleiman ameeleza kuwa tukio hilo limekuwa likifanyika kwenye nyumba ambayo haijaisha wakati watoto hao wakitokea shuleni.

Amesema watoto hao wa kiume wenye umri wa miaka minane wamekuwa wakifanyiwa kitendo hicho kwa nyakati tofauti, baada ya mtuhumiwa kuwalaghai na kuwapeleka katika pagale hilo.

Suleiman amesema Machi 13 majira ya saa 11 jioni ndipo ilibainika kuwa mtuhumiwa huyo amekuwa akitekeleza tukio hilo.

“Hawa watoto wakati wanatoka shuleni kurejea nyumbani, ndipo aliwachukua kisha kuwapeleka katika jengo ambalo linaendelea kujengwa eneo la Maduka Makubwa na kuwafanyia vitendo hivyo vya udhalilishaji,” amesema Suleiman.  

Baada ya tukio hilo kubainika, watoto hao walipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara Ligula kwa ajili ya uchunguzi na matibabu na ilibainika kuwa ni kweli wanafanyiwa vitendo hivyo.

Kamanda Suleiman anasema kwa sasa hali zao za kiafya zinaendelea vizuri na mtuhumiwa ambaye amekamatwa atafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Maduka makubwa Zuwena Kasimila  amesema alipopata taarifa, aliwahi eneo la tukio na kuangalia mazingira hayo.

“Nilikuwa nyumbani nikaambiwa kuna mtu amekamatwa katika mtaa wangu, nikaamua kufuatilia nijue nini tatizo ambapo niliambiwa amewalawiti watoto wadogo wa miaka nane. Nilienda kwenye eneo la tukio niliangalia mazingira yanashtua kidogo,” anasema.

Asha Abdallah mkazi wa Mtwara Mjini anasema tukio hilo ni la kusikitisha na kuogopesha kwa wazazi kwa kuwa itawapa wakati mgumu wa malezi kwa watoto.

“Hivi jamani wapi salama kwa watoto wetu, ina maana hawana usalama kwa nini jamii tusiungane ili kupinga vitendo kama hivi ambavyo vinaenda kuwaharibu watoto wetu,” amesema Asha.

Naye Abdulah Mkamba, pia mkazi wa mjini Mtwara amesema “tunaomba jambo hili lifanyiwe uchunguzi na akibainika achukuliwe hatua ili iwe ni funzo kwa wengine. Hivi vitendo si salama kwa jamii yetu, ni vema wananchi wakatoa taarifa pale wanapoona kuna changamoto yoyote au wanahisi jambo lolote kwa kuwa hili janga ni kubwa linaweza kumtokea yeyote katika familia zetu,” amesema Mkamba.