Mzee wa miaka 72 ajiua, kisa kushtakiwa na mkewe

Mzee wa miaka 72 adaiwa kujinyonga

Muktasari:

  • Mkazi wa Kijiji cha Lyamungo Sinde, Zephania Lyimo (72) anadaiwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya manila kwa madai ya kukasirishwa na mkewe kumshtaki polisi.

Hai. Mkazi wa Kijiji cha Lyamungo Sinde, Zephania Lyimo (72) anadaiwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya manila kwa madai ya kukasirishwa na mkewe kumshtaki polisi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Ronald Makona alidai kuwa Lyimo alikutwa amejinyonga kwa kamba sebuleni kwake Januari 31 mwaka huu, lakini ndugu wanadai kiini ni tukio hilo la mkewe, Mary.

Kamanda Makona alisema juzi kuwa mzee huyo alikutwa ananing’inia na hakuacha ujumbe wowote unaoelezea sababu za kuchukua uamuzi huo.

“Alikuwa amefunga kamba hiyo kwenye kenchi ya paa la sebuleni, taarifa ya chanzo cha kuamua kufanya hivyo hazikujulikana mara moja,” alisema kamanda huyo wa polisi.

Hata hivyo, mke wa marehemu, Mary Lyimo alisema alifikia uamuzi wa kumpeleka mumewe katika dawati la jinsia Kituo cha Polisi Hai baada ya kuishi miaka mingi akiteseka kwa vipigo.

Alidai kuwa alifika polisi na kujieleza kisha mumewe aliitwa Januari 27 na kusomewa mashtaka ambayo ni kumpiga mkewe na kumfungia nje mara kwa mara.

“Kwa kuwa mume wangu ni mkorofi alikuwa anakataa kuwa hanifanyii ukatili huo, yule askari alisema akachapwe viboko, ili atulie na ndipo walipomchukua na kwenda kumweka rumande,”alidai mwanamke huyo.

“Baada ya saa saba kupita, mkwe wangu ambaye ni mume wa mwanangu anayeishi Arusha alipigiwa simu na kuja kumwekea dhamana, tukasuluhishwa, tukaambiwa Ijumaa ya Januari 29 turudi kueleza kama tumeelewana,” alidai Mary.

Alidai kuwa siku hiyo mume wake alishindwa kwenda kwa kuwa alikuwa amekunywa pombe nyingi na alitapika, hivyo alilazimika kubeba matapishi ya mume wake kama kielelezo kwenda kuonyesha askari wa dawati ili asiwekwe rumande.

Mwanamke huyo alidai kuwa siku ya Jumapili ambayo ndio siku mume wake alijinyonga, waliamka na kuchemsha chai na maji ya kuoga lakini, mumewe alimwambia aende kanisani.

“Nilikwenda kanisani kama kawaida. Niliporudi nyumbani nikaingia jikoni nikapika, nilikuwa bado sijaingia sebuleni kwa sababu nilikuwa nasikia sauti ya TV nikajua anaangalia movie (sinema) kama ilivyo kawaida yake,” alisema Mary.

“Chakula kilipoiva nilimpelekea ndio nikakuta ameninginia na kamba sikuelewa nikatoka nje kwenda kumuita kaka yake sikumkuta nikaanza kupiga kelele watu wakaja.

“Kwa kuwa amekuwa akinitamkia ataniua halafu ajiue, sijashanga (kujinyonga) kwa kuwa amekuwa akizungumza maneno hayo mara kwa mara, ndio maana nikaamua kwenda kuripoti katika dawati la jinsia polisi.”

Elifas Lyimo ambaye ni kaka wa marehemu alidai kuwa mdogo wake alikuwa na ugomvi wa mara kwa mara na mke wake.

Alidai kuwa anaamini kilichomkwaza mdogo wake hadi kufikia hatua ya kujinyonga ni baada ya mke wake kumpeleka polisi na kuandika maelezo ya kumdhalilisha.

Alidai mdogo wake aliporudi kutoka dawati, alimwambia, “sijawahi kudhalilishwa hivyo tangu nimezaliwa ikilinganishwa na umri wangu mkubwa, huyu mwanamke maneno aliyoenda kuanika hayafai kabisa.”

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Geoffrey Muro alidai kuwa ugomvi wa marehemu na mke wake ameshausuluhisha mara nyingi na walitambua mke hayuko vizuri kutokana na namna alivyokuwa akijieleza.

Muro alisema alimshauri Lyimo ampeleke mke wake hospitali kwa ajili ya kuangaliwa afya yake.