Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mzigo unaowakabili viongozi wa mitaa

Wenyeviti wa serikali za mitaa Jimbo la Nyamagana wakiwa wameinua mikono yao wakati wakiapa kiapo cha utiifu kazini. Picha na Anania Kajuni

Muktasari:

  • Wanahimizwa kutenda haki, kusimamia miradi ya maendeleo, kuepuka mabavu na kushirikiana na wananchi kwa utawala bora na utatuzi wa changamoto.

Dar/mikoani. Viongozi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji waliochaguliwa Novemba 27, 2024, wanatarajiwa kukabiliwa na kibarua kigumu katika utendaji wao katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Migogoro ya mipaka, ardhi, ndoa, mikopo umiza maarufu ‘kausha damu’ na usimamizi wa ulinzi katika jamii, kutenda haki, usafi wa mazingira, ubovu wa miundombinu ni miongoni mwa vibarua vinavyowasubiri wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Majukumu hayo yanakuja siku chache baada ya viongozi hao kutangazwa washindi katika uchaguzi uliohusisha vijiji 12,333, vitongoji 64,274 na mitaa 4,269 uliofanyika vizuri kwa asilimia 98 kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa.

Katika uchaguzi huo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeibuka na ushindi kwa asilimia zaidi ya 99 ikifuatiwa na vyama vya Chadema na ACT Wazalendo. Tayari viongozi hao wameanza kuapishwa na nasaha zimetolewa.

Baadhi ya wananchi wa mikoa mbalimbali waliozungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti wameeleza matarajio kutoka kwa wenyeviti wa mitaa, vijiji na vitongoji waliochaguliwa, huku viongozi hao na waliopita wakieleza mikakati yao na yale wanayokwenda kukumbana nayo.

Mwenyekiti mstaafu wa mtaa wa Mbalizi Road, jijini Mbeya (CCM), Noah Mwakifwila anasema jamii zinapitia changamoto mbalimbali, ikiwamo migogoro ya mara kwa mara ambayo sehemu kubwa ya utatuzi ni wenyeviti kabla ya kwenda ngazi za juu.

“Kero ni nyingi na wenyeviti ndio kimbilio, kuna ugomvi wa kifamilia, migogoro ya kimaslahi, mivutano ya kijamii lakini yote hayo mwenyekiti anapaswa kuwa katikati kwa kutumia busara kumaliza changamoto hizo,” anasema Mwakifwila.

Kwa upande wake, Mussa Mwambogolo aliyekuwa mjumbe katika Mtaa wa Tunduma wilayani Mbeya, anasema wenyeviti wanapaswa kutenda haki na kujali hisia za waliowapigia kura na kuwapa imani.

“Watende haki, wasilipize visasi, wananchi ndio waliamua kuwapa kura na kuwakopesha imani, hivyo wazingatie mahitaji yao kwa kuweka usawa ili kila mmoja asijutie kura yake,” anasema Mwambogolo.


Wasemavyo viongozi

Mkurugenzi wa Mji wa Geita, Yefred Myenzi anasema jambo kubwa analotegemea kwa viongozi hao ni ushirikiano wao katika kutekeleza majukumu ya Serikali, ikiwemo miradi ya maendeleo.

“Hawa ndio wako karibu na wananchi na wananchi wanawaamini wakiwapa ushirikiano itakua rahisi kwao kutekeleza miradi ya mendeleo. Unapokua na kiongozi mwenye maono hata kazi zinakuwa rahisi,” anasema Myenzi.

Katibu Tawala Wilaya ya Mbeya, Mohamed Aziz anasema matarajio yao kwa wenyeviti ni kusimamia haki, utawala bora na kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto za wananchi. 

“Msiende huko kuwa miungu watu kwa kushindwa kutatua migogoro ya wananchi hasa kwenye kugonga mihuri kwa kutaka malipo. Hatutakuwa tayari kuvumilia, tunaomba wananchi watoe taarifa inapotokea hali hiyo,” anasema Aziz.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha, Murtallah Mbillu anasema wanatarajia viongozi hao waliochaguliwa kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao na inakamilika kwa viwango vilivyowekwa.

Kwenye kesi za ardhi hasa kugombea mipaka, anasema anatarajia wenyeviti wa vijiji na vitongozi watasaidia kumaliza migogoro hiyo mapema kwa sababu wao ni rahisi kuwashawishi wananchi waliowachagua.

“Kuhusu mikopo umiza, natarajia wao ndio wanaandika barua za utambulisho kabla mtu hajapewa mkopo na kuthibitisha ni mkazi wa eneo husika,” anasema Mbillu.

Msimamizi msaidizi wa uchaguzi jimbo la Nyamagana anayekaimu ukurugenzi wa Jiji la Mwanza, Peter Juma anasema viongozi hao ni muhimu katika jamii hasa katika utekelezaji wa sheria, kanuni na maendeleo ya jamii sambamba na ulinzi na usalama.

“Kwenye kamati ya maendeleo ya mtaa jinsi ilivyo kwa muundo wake halmashauri inapofanya kazi watekelezaji wakubwa ni viongozi wa serikali za mitaa.   Mwenyekiti wa mtaa ni mmoja ya mjumbe wa kamati ya usalama na maendeleo katika jamii,” anasema.

Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanza Mjini, Nyamisango Bulemo akizungumza na viongozi baada ya kuwaapisha amewataka kutotumia mabavu ili kupata heshima kwa wananchi.

“Nawasihi mnapokwenda kutekeleza majukumu yenu msitafute heshima kwa mabavu, wengine watakujaribu kwa kukuonyesha dharau, lakini hata wakifanya hivyo bado haitakuondolea cheo chako au kukupelekea kufanya uamuzi kimabavu, kuna muda kupitia kazi na uamuzi wako watakuheshimu,” anasema Bulemo.


Wasemacho wananchi

Mkazi Sokoine jijini Mbeya, Adam Mwasambili amewataka wenyeviti kutokuwa sehemu ya migogoro, ikiwemo kujimilikisha mali za wananchi au kuwa chanzo mvutano kwa jamii.

“Watimize wajibu wao kama walivyoahidi kwenye kampeni. Migogoro ya ardhi, mali na ubabe isiwe sehemu ya majukumu yao kwa sababu baadhi wanatumia nafasi zao kusababisha mivutano,” anasema Mwasambili.

Baadhi ya wananchi wa jiji la Arusha wanasema wenyeviti wa mitaa, vijiji na vitongoji wana wajibu wa kupewa elimu ili kutambua majukumu yao ambayo ni kusimamia huduma za kijamii, ikiwemo elimu na afya.

Mkazi Mtaa wa Olorien, Kata ya Moshono, Irene Josephat, anasema kwa kuwa viongozi hao hubadilishwa kila mara, ni muhimu wakapewa elimu kuhusu wajibu na majukumu yao.

“Naona elimu ni muhimu zaidi kwa viongozi hawa, wanabadilika kila mara, wengine wanateuliwa na vyama vyao na kugombea au kutokana na ushawishi wao kwa jamii ila hawajui majukumu yao ni muhimu kukumbushwa,” anasema Josephat.

Jambo hilo liliungwa mkono na mkazi wa Musoma, Amina Sadiki aliyependekeza viongozi hao kupewa mafunzo ya mara kwa mara yatakayowasaidia kuleta ufanisi katika majukumu yao.

“Unajua hawa wanapokea kesi tofauti tofauti kama vile migogoro katika jamii au familia, migogoro ya ndoa, wao ndio wahusika wa kwanza kwenye suala la ulinzi na usalama wa maeneo.

“Pamoja na mambo mengine, baadhi yao hawana taaluma yoyote, hivyo wakipata mafunzo ya mara kwa mara yatawasaidia kutimiza wajibu wao wa kiuongozi,” anasema Amina.

Naye, Saitoti Laizer, mkazi wa Mtaa wa Oloresho, anasema viongozi wa serikali za mitaa wanatakiwa kuwa na posho za uhakika ili kupunguza vitendo vya ubadhirifu.

“Wengine wanajiingiza kuuza ardhi za watu kwa sababu tu hawana uhakika wa mwisho wa mwezi, sasa wakiwa na posho hata kama kidogo zitawasaidia kutekeleza wajibu wao,” anasema Laizer.

Mkazi wa mtaa wa Ibanda kata ya Nyegezi jijini Mwanza, Tumaini Bujora, anasema, “binafsi ningependa waanze na suala la ulinzi na usalama ndani ya mtaa wetu, suala hili limekuwa changamoto watu wanaporwa mali zao.”

Pia, wananchi wa mitaa mbalimbali ya Mji wa Geita wanasema matumaini yao kwa viongozi hao ni  kupeleka kilio chao cha ubovu wa barabara na kero ya uhaba wa maji ili zitafutiwe ufumbuzi.

Mkazi wa Mtaa wa14 Kambarage wilayani Geita, Jumanne Maulid anasema barabara nyingi za mtaa huo zimeharibika na hazijafanyiwa matengenezo, licha ya kulalamika mara kwa mara.

Wakazi wa Jiji la Dodoma wamesema wana imani na viongozi wao wa serikali za mitaa waliowachagua kuwa watawasaidia kutatua changamoto walizonazo, ikiwemo kuondoa migogoro ya ardhi na kuimarisha usalama kwenye mitaa yao.


Umuhimu wa wenyeviti

Mhadhiri wa Chuo cha Serikali za Mitaa (Hombolo) jijini Dodoma, Paulo Faty anasema viongozi wa mitaa, vijiji na vitongoji ni muhimu kwa sababu maelekezo yote ya Serikali yanayoshuka chini watekelezaji ni wenyeviti hao.

"Iwe miradi ya maendeleo, shughuli za usalama au kutoa huduma hawa (wenyeviti) ndio wanaomgusa mwananchi mmoja baada ya mwingine, kwa kutumia takwimu sahihi wanasimamia maendeleo na utoaji wa huduma ya ulinzi na usalama," anasema Faty.

Faty anasema mwenyekiti wa kijiji ni muhimu, kwanza ni mwenyekiti wa serikali ya kijiji na mkutano wa kijiji unaotoa uamuzi kama Serikali.

"Mkutano mkuu wa kijiji ni Serikali iliyokamilika, inaweza ikatunga sheria ndogo za ukusanyaji wa mapato, uamuzi wa mipango ya maendeleo, kwa wenyeviti wa vijiji ni watu muhimu.

"Mwenyekiti wa kijiji ni mlinzi wa amani, ndio maana masuala yote yanayoleta uvunjifu wa amani, ikiwemo ndoa na migogoro ya ardhi yanasimamiwa na wao. Kwa hiyo, hawa ni watu muhimu na uchaguzi wao ni muhimu,"

Faty anasema pia wenyeviti wa vijiji wamekasimiwa majukumu mengi wakisaidiana na wenyeviti wa vitongoji ambao ni wajumbe namba moja kwenye serikali ya kijiji.

"Mara nyingi masuala makubwa kama ya ardhi yanatakiwa kufanyiwa uamuzi kwenye mkutano mkuu wa kijiji kwa sababu ndio mkutano wenye haki na wananchi wote wenye miaka 18 wanatakiwa kushiriki," anasema.

Kuhusu wenyeviti wa mitaa, Faty anasema mwenyekiti wa mtaa anaongoza kamati ya mtaa ambayo ni chombo kinachokutana mara nne kwa mwaka kuweka vipaumbele vya maendeleo na huduma za jamii katika eneo husika.

"Wakishakubaliana wanaihitisha mkutano wa wananchi wa mtaa husika na mapendekezo yao wanapeleka katika baraza la kata linalochakata na kupeleka katika baraza la madiwani la jiji, halmashauri au manispaa," anasema Faty.


Wenyeviti waliochaguliwa

Mwenyekiti wa Mtaa wa Igodima jijini Mbeya, Eliud Semle anasema atapambana kumaliza au kupunguza migogoro ya ardhi, akisema ikionekana kumzidi nguvu ataiwasilisha katika baraza la kata.

“Haikuwa kazi rahisi kurejea kwenye kiti, lakini kutokana na kazi nzuri niliyoifanya wananchi wamenirejesha, nitasimamia haki, misingi na uwajibikaji hasa kwenye eneo la migogoro ya ardhi na ushirikishaji wananchi,” anasema Semle.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Bugosi katika halmashauri ya Mji wa Tarime mkoani Mara, William Ghati anasema licha wenyeviti wa mitaa kukabiliwa na changamoto nyingi, wengi wao wamekuwa wakijitahidi kutekeleza majukumu yao.

Ghati anasema hivi sasa kumekuwepo na ongezeko la kesi zinazohusu masuala ya mikopo hasa ile umiza, jambo linaloleta changamoto kubwa katika utatuzi wake.

“Kuna wale wanaokuja unawajazia fomu au kuwaandikia barua za utambulisho, sasa wakishachukua mkopo wakashindwa kurejesha yule mkopeshaji anakuja kwako mwenyekiti umsaidia ili kuirejesha hapo ndio panakuwa na mtihani,” anasema Ghati.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyang'wena katika halmashauri ya manispaa ya Musoma, Selemani Makanja aliungana na Ghati kuhusu mikopo umiza, akisema bado ni janga kubwa linalohitaji ufumbuzi wa kudumu wa haraka.

Kwa mujibu wa Makanja, katika kipindi chake kilichopita cha uongozi suala hilo limekuwa changamoto kubwa huku waathirika wakuu wakiwa kinamama.

Makanja anaishauri Serikali kuweka mazingira wezeshi kwa kinamama kupata mikopo inayotolewa na halmashauri, akisema masharti yaliyopo bado yanawaweka katika wakati mgumu kunufaika na fursa hiyo ya mikopo isiyokuwa na riba.

Mwenyekiti wa mtaa wa Compaund Mjini Geita, Seif Rajabu anasema ni wajibu wake kuwatumikia kwa moyo wote wananchi, akisema jambo atakaloanza ni changamoto ya ubovu wa barabara na maji.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mahina, jijini Mwanza (Chadema), Bulabo Paul anasema mbali na kupitia changamoto nyingi wakati wa kinyang'anyiro hicho, anaahidi kushirikiana na viongozi wa vyama vingine kuleta maendeleo ya eneo hilo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Nzuguni B jijini Dodoma, Isaya Wami anasema eneo hilo limekuwa na migogoro mingi ya ardhi kwa kuwa bado halijarasimishwa, hivyo wanashindwa kupitisha miundombinu ya maji na umeme.

“Kwa yale ambayo yapo ndani ya uwezo wetu tutayatekeleza, lakini kuna yale yapo Serikali Kuu tutashirikiana nao kuhakikisha yanatekelezwa kwa maslahi ya wananchi wetu,” anasema na kuongeza;

“Kikubwa tunachohitaji ni kushirikishwa kila hatua ya utekelezaji wa miradi hiyo.”

Mwenyekiti wa Mtaa wa Msangalalee Magharibi Kata ya Dodoma Makulu, Leonard Ndama anasema amejipanga kuzitatua changamoto zote za wananchi kama alivyoahidi kwenye kampeni za uchaguzi zilizomwezesha kupata nafasi hiyo.

  

Imeandikwa na Bakari Kiango (Dar), Saddam Sadick (Mbeya), Rachel Chibwete (Dodoma), Beldina Nyakeke (Mara), Janeth Mushi (Arusha)

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.