Nabii GeorDavie: Msiba wa Nisher umeniachia deni kwa vijana
Muktasari:
- Mwili wa Nick Davie maarufu Nisher aliyefariki dunia Desemba 12, 2023 umezikwa leo Jumamosi Desemba 16, 2023 huku baba yake mzazi, Nabii Dk GeorDavie akisema umemuachia deni kubwa kwa vijana la kuwasaidia.
Arusha. Nabii Dk GeorDavie, amesema kifo cha mwanaye Nick Davie maarufu Nisher, kimemuachia deni kubwa na anasikia moyoni vijana wanataka kusaidiwa.
"Nitaendelea kuwasaidia vijana kwa kila hali hata kwa fedha," amesema leo Ijumaa, Desemba 16, 2023 wakati wa maziko ya Nisher aliyekuwa msanii na mtayarishaji wa video za nyimbo za muziki wa kizazi kipya.
Maziko ya Nisher aliyefariki dunia Desemba 12, 2023, akiwa anapatiwa matibabu jijini Arusha, yalifanyika nyumbani kwa baba yake eneo la Kisongo wilayani Arumeru.
Maziko hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, siasa, kiserikali na wasanii.
Nabii GeorDavie amesema amejifunza kuwa watu ni vizuri, kwani unaweza kuwa na fedha lakini kama hauna watu ni bure, hivyo akashauri uwekezaji katika watu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella akizungumza kwa niaba ya Serikali katika msiba huo uliofanyika katika Nyumba ya Matamko ya Kanisa la Ngurumo za Upako, amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa pole kwa familia na ameahidi atakapokwenda Arusha, atamtembelea Nabii GeorDavie kutoa pole.
"Dk GeorDavie anatusaidia Serikali, kwani ni kiongozi ambaye anarejesha utulivu kwa watu na sehemu yoyote yenye utulivu na amani ni lazima Serikali ifike," amesema.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema Nisher alikuwa na mchango mkubwa kwa vijana.
Amesema Nisher amefariki dunia akiwa na umri mdogo wa miaka 34 kwa kuwa wastani wa Watanzania kuishi ni miaka 69, lakini amefanyakazi kubwa.
Mbunge wa Arusha, Mrisho Gambo pia alishiriki katika msiba huo na kutoa pole kwa familia.
Msanii Bernard Paul maarufu Ben Paul, akitoa salamu kwa niaba ya wenzake amesema wameondokewa na mwalimu, mtu wa kupigiwa mfano na mwanamapinduzi katika tasnia ya muziki.
"Kupitia Nisher wamezaliwa wasanii wengi, napenda kuamini ninachosema Nisher ananisikia, nasema asante kwa maisha yako," amesema.
Akisoma wasifu wa Nisher, dada yake, Monica Davie amesema alizaliwa Julai 8, 1989 akiwa mtoto wa kwanza wa Dk GeorDavie.
Amesema Nisher ameacha wadogo zake, Anna, Monica na Kenny Davie.
Monica amesema Nisher alianza kuumwa mwishoni mwa Novemba na madaktari walihangaika kuokoa maisha yake lakini alifariki dunia Desemba 12, 2023.
Monica amesema Nisher alisoma jijini Arusha na Marekani masuala ya uandaaji na uongozaji video, akiwa msanii, mtangazaji na mwigizaji.
Nisher alifanya kazi za kundi la Weusi la Arusha, Joe Makini, Fide Q, Ben Paul, Baraka the Prince na wengine wengi.