NacoNGo yasitisha kampeni ya changia Hanang

Muktasari:

  • Baraza la Asasi za Kiraia lasitisha kampeni yake ya kukusanya michango kwa ajili ya watu walioathirika na maporomoko ya matope yalitokea Desemba 3, 2023; wilayani Hanang, mkoani Manyara na kusababisha vifo vya watu 80 na kujeruhi wengine 116, huku mali na miundombinu mbalimbali vikiharibika.

Arusha. Kampeni ya ‘Changia Hanang’ iliyokuwa ikiendeshwa na Baraza la Asasi za Kiraia nchini (NacoNGo), kwa kushirikia na wadau wengine, imesitishwa huku utaratibu mwingine kuhusu michango hiyo, ukitangazwa.

Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu wa NacoNGo, Revocation Sono aliyoitoa leo Desemba 8, 2023. Sono  amesema maamuzi hayo yamezingatia simu mbalimbali zilizopigwa kwake na hali halisi katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa Sono, imeelekezwa kuwa wenye michango ya kifedha watatakiwa kuzifikisha kwa waathirika kupitia akaunti maalumu ya maafa inayoendeshwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, na wenye vifaa wametakiwa kuvipeleka katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Hanang.

Kampeni ya NaCoNGo ilikuwa inaangalia uwezekano wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), kujiratibu kupitia mtandao wake, ili kukusanya fedha na misaada mbalimbali ambayo ingepelekwa idara kama fungu la asasi za kiraia, ili iwasaidie waathirika.

"Tunasikitika kutangaza kusitishwa kwa  mchakato huu, tunaelewa juhudi za  kila azaki kutala kuchangia na tunapenda kutoa shukurani zenu kwa msaada wenu usio na ukomo," imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Hata hivyo wakati mchakato huo  unasitishwa tayari asasi tatu zilikuwa zimejitokeza kuchanga kiasi cha Sh4.5 milioni huku matarajio yakiwa kukusanya zaidi ya Sh100 milioni.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Sono hakutaka kuweka wazi watu waliompigia simu wala kueleza alichoambiwa, isipokuwa amesisitiza juu ya NacoNGo kutokusanya tena michango kama ambavyo ilikuwa inafanya.

"Ambao watataka kuchangia, wanatakiwa kupeleka michango akaunti ya maafa moja kwa moja na vifaa kwa mkuu wa wilaya," amesema.