Nafasi zatangazwa JWTZ, ndoa kizuizi

Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Kanali Gaudentius Gervas Ilonda akitoa taarifa ya nafasi za kujiunga na Jeshi hilo wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo Machi 09, 2023 Jijini Dodoma.

Muktasari:

  • Jeshi la Wananchi Tanzania limetangaza nafasi za kujiunga na jeshi hilo ambapo ngazi ya chini kabisa ni wale waliomaliza kidato cha nne na kikwazo kilichotajwa usiwe na hatia.

Dodoma. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetangaza nafasi za kujiunga na jeshi hilo kwa vijana wa kitanzania wenye elimu kuanzia kidato cha nne hadi shahada ya uzamili ambao wamemaliza mkataba wa mafunzo ya kujitolea JKT na kurudishwa majumbani.

Nafasi hizo zimetangazwa leo Alhamisi, Machi 9,2023 na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano JWTZ, Luteni Kanali Gaudentius Ilonda wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari, Jijini hapa.

Luteni Kanali Ilonda amesema mwenye nia ya kuandikishwa katika Jeshi hilo anatakiwa awe raia wa Tanzania wa kuzaliwa mwenye kitambulisho cha Taifa.

Pia sifa zingine awe na umri wa miaka 18 hadi 26 kwa wenye elimu ya kidato cha nne hadi kidato cha sita na umri usiozidi miaka 27 wenye elimu ya juu.

Amezitaja sifa zingine ni awe na afya nzuri na akili timamu, Mtanzania mwenye tabia na nidhamu ambaye hajapatikana na hatia ya makosa ya jinai mahakamani na kufungwa.

Vilevile awe na cheti halisi cha kuzaliwa, shule na taaluma, asiwe ameoa au kuolewa.

"Pia awe hajalitumikia Jeshi la Polisi, Magereza, Chuo cha mafunzo au kikosi Maalum Cha kuzuia Magendo (KMKM). Awe amehitimu mafunzo ya JKT kwa mkataba wa kujitolea miaka miwili na kutunukiwa cheti,"amesema Luteni Kanali Ilonda.

Luteni Kanali Ilonda amesema maombi yaandikwe kwa mkono na yawasilishwe Makao Makuu ya JWTZ Dodoma kuanzia leo hadi Machi 20 mwaka huu.

Hata hivyo, ametoa angalizo kwa matapeli kwa kudai Jeshi lipo makini na litawachukulia hatua kali wale watakaohusika na utapeli kupitia mamlaka husika.