Naibu Waziri amwaga chozi jukwaani akidai kukwamishwa jimboni

Mbunge wa Bukoba Mjini na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Steven Byabato akiwa amepiga magoti alipohutubia wananchi wakati wa hafla ya uzinduzi na kukabidhi mradi wa ujenzi wa Stendi Kuu mjini Bukoba kwa mkandarasi.
Muktasari:
Mbunge Byabato aliyechaguliwa kuwakilisha jimbo la Bukoba mjini uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 alimwaga machozi Oktoba 16, 2023 wakati wa hafla ya uzinduzi na kukabidhi mradi wa ujenzi wa ukarabati wa Stendi Kuu mjini Bukoba kwa mkandarasi.
Bukoba. Kwa wengi, tukio la mbunge wa Bukoba Mjini, Steven Byabato (CCM) kumwaga chozi jukwaani alipohutubia wapigakura wake linaweza kuchukuliwa kuwa ni joto la kisiasa Taifa linapokaribia chaguzi kuanzia wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Japo ni haki ya kikatiba ya uhuru wa maoni na mawazo kwa mujibu wa Ibara ya 18 (a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977; lililo la wazi na kweli ni kwamba Byabato ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amemwaga machozi jukwaani akidai baadhi ya watu wanamkwamisha
Tukio lilivyokuwa
Mbunge Byabato aliyechaguliwa kuwakilisha jimbo la Bukoba mjini uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 alimwaga machozi Oktoba 16, 2023 wakati wa hafla ya uzinduzi na kukabidhi mradi wa ujenzi wa Stendi Kuu mjini Bukoba kwa mkandarasi.
Akihutubia umati wa uliojumuisha wananchi, viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wa Kiserikali, Byabato akiwa amepiga magoti alishindwa kuzuia hisia zake na kuanza kuzungumza kwa sauti ya kutetemeka, hali iliyowalazimu baadhi ya viongozi kutoka meza kuu kwenda kumtuliza na kumnyanyua kutoka ardhini.
Hata baada ya kunyanyuka na kukabidhiwa chupa ya maji ya kunywa ambayo hata hivyo aliyaweka kando bila kuyanywa, mbunge huyo ameuomba umma wa wana Bukoba kumuunga mkono katika jitihada za kusukuma gurudumu la maendeleo ya jimbo hilo badala ya hali ya sasa ya baadhi kumkwamisha.
‘’Mimi nawaomba ndugu zangu, tusaidiane tusogeze Bukoba yetu mbele…tusikwamishane. Hizi kazi nafanya siyo zangu mimi, ni kazi zenu ninyi mmenituma….kwanini unikwamishe?’’ amesema Byabato kwa sauti ya kutetema akiwa amepiga magoti mbele ya wananchi
Bila kutaja wanaomkwamisha na jinsi anavyokwamishwa, mbunge huyo ameongeza; ‘’Hii Bukoba ni ya kwetu sote, tusaidiane tuipeleke mbele tumechelewa…..maneno yanakwaza na yataturudisha nyuma,’’
Byabato aliyechaguliwa kwa mara kwanza kuwakilisha jimbo hilo mwaka 2020, amewahakikishia wananchi kuwa ataendelea kutekeleza bila hofu majukumu yake yote ya kibunge ikiwemo kusukuma utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hata kama kwa kufanya hivyo kutamfanya akose ubunge uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
‘’Mimi ubunge sikuzaliwa nao…nautaka, naupenda na nitautumikia kufa na kupona. Mmenipa miaka mitano, mnisaidie niukamilishe. Mkiniona nafaa nipeni tena. Mkiona sifai sawa. Lakini ninachoahidi sitaacha kufanya (shughuli za maendeleo) eti nitakosa ubunge…haki ya Mungu mimi siache, nitafanya. Kama naukosa ubunge 2025 kwa sababu stendi imejengwa Bukoba mjini, niko tayari,’’ amesisitiza
Ameongeza; ‘’Kama kufanya stendi nzuri iwepo Bukoba mjini itanifanya niukose ubunge (mwaka) 2025, sawa….ubunge waninyime, stendi ipo mtanikumbuka,’’
Miradi ya maendeleo
Pamoja na ujenzi wa Stendi Kuu ya Bukoba utakaogharimu zaidi ya Sh3.1 bilioni, miradi mingine ya maendeleo inayotekelezwa jimbo la Bukoba mjini inayohusisha baadhi ya nyumba na makazi ya watu kuboolewa ni upanuzi wa eneo korofi la barabara katika kona ya Nyangoye Mtaa wa Hamugembe.
Licha ya kuwa na barabara finyu, eneo la kona ya Nyangoye pia lina mteremko mkali unaosababisha ajali za barabarani kutokana na madereva kushindwa kumudu kasi ya magari na hivyo kusababisha madhara kadhaa ikiwemo vifo, majeruhi na uharibifu wa vyombo na miundombinu ya barabara.
Licha ya kukubaliana na umuhimu wa miradi hiyo, baadhi ya wananchi wanaoishi maeneo ya miradi wanalalamikia kukosa fidia ya mali na nyumba zao wanazodai kujenga na kuishi kwa zaidi ya miaka 50 iliyopita.
Redemtus Muganyizi, mkazi wa Hamugembe amesema kiuhalisia, hakuna mwananchi anayepinga kupanuliwa kwa barabara eneo la kona ya Nyangoye, bali kinachoibua malalamiko yanayoweza kutafsiriwa kama kupinga mradi ni baadhi ya watu kukosa fidia ya nyuma na mali zao.
‘’Kuna watu wameishi pale zaidi ya miaka 30 iliyopita…sasa kuambiwa kwamba ni nyumba 25 peke ndizo zitafidiwa ni sawa na kuwanyima haki wengine. Serikali iliangalie hili kwa jicho la huruma,’’ amesema Muganyizi
Akizungumzia malalamiko hayo, Byabato amesema anaguswa na suala la baadhi ya wananchi kukosa sifa ya kulipwa fidia, lakini yeye binafsi hausiki wala kunufaika kwa namna yoyote wananchi wanapokosa fidia.
‘’Mimi Rwamishenyi ni kwetu mimi…mimi ukibomolewa nyumba yako napata faida gani,’’ amehoji Byabato akiwa amepiga magoti mbele ya wananchi
Amewaomba wananchi kuunga mkono utekelezaji wa mradi hiyo ukiwemo ule wa kupunguza ufinyu wa barabara na mteremko mkali eneo la Nyangoye uliotokana na maombi yake kwa Makamu wa Rais Dk Phillip Mpango wakati wa ziara yake mjini Bukoba.
Ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Bandari ya Bukoba hadi mzunguko wa Barabara ya Rwamishenyi pia utahusisha kubomolewa kwa baadhi ya nyumba ambapo kwa mujibu wa taarifa kutoka Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) Mkoa wa Kagera, ni nyumba 42 pekee ndizo zitafidiwa.