Naibu Waziri Ndejembi ataka halmashauri zipande miti

Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Deogratius Ndejembi akiongoza shughuli ya usafishaji mazingira katika mitaa ya Mwanga baa jijini Dodoma.

Muktasari:

  • Wakati wiki ya mazingira ikiendelea huku wadau wakifanya usafi katika maeneo mbalimbali, Serikali imezitaka halmashauri nchini kupanda miti kwenye miradi.

Dodoma. Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (Tamisemi), Deogratius Ndejembi ameziagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha zinapanda miti kwenye maeneo wanayopeleka miradi ya upimaji wa viwanja.

 Ndejembi ameyasema hayo leo Juni 3, 2023 wakati wa shughuli za usafi katika eneo la Mwanga bar ikiwa ni wiki ya mazingira itakayofikia kilele chake Juni 5, 2023.

“Hapo zamani tulikuwa tunaona eneo likipangwa Area C, D, Nkuhungu na maeneo mengine miundombinu ilivyokuwa inapelekwa na mamlaka husika ilikuwa inapanda miti. Anayejua vizuri maeneo hayo yamejaa miti,” amesema.

Amewaagiza manispaa na majiji ikiwemo la Dodoma kuhakikisha wanapanda miti katika maeneo au viwanja wanavyogawa na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) kumaliza kwa kupitisha barabara.

 “Miti itapendezesha na kutunza mazingira, uwezo huo mnao, walivyokuwa CDA (Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma) walikuwa na maboza bustani walikuwa na miti wanapanda na wanamwagilia. Mlipoachiwa wenyewe mmepima viwanja tu mmesahau suala zima la utunzaji wa mazingira na upandaji wa miti,” amesema.

Ameagiza jiji la Dodoma kujielekeza katika upandaji wa miti maeneo ambayo barabara inapita na maeneo ya wazi.

Aidha, amewaagiza viongozi wa serikali za mitaa, kata na tarafa  kuhamasisha Jumamosi iliyopangwa kwa ajili ya usafi, inazingatiwa katika maeneo yao.

“Tusiache likawa jukumu la mwingine na mwingine, ataona ni jukumu la mwingine. Viongozi wetu katika mitaa, kata na maofisa tarafa, tuhakikishe mwendelezo wa usafi siku za Jumamosi na si kwa Dodoma tu iwe kwa nchi nzima ili tuweke miji yetu misafi,”amesema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema kuanzia wiki hii watafuatilia changamoto ya utiririshaji wa maji kutoka vyooni jijini Dodoma na kuwachukulia hatua wahusika.